Mauaji ya wanawake yapungua kwa asilimia 81 Geita

Geita. Mauaji ya wanawake yanayotokana na matukio ya ukatili wa kijinsia mkoani Geita yamepungua kutoka vifo 37 mwaka 2023 hadi saba mwaka 2024 (sawa na asilimia 81).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema hayo leo Machi 15, 2024 wakati wa sherehe za mtandao wa Polisi wanawake mkoani humo.

Amesema mbali na kupungua mauaji ya wanawake, pia matukio ya ukatili wa kijinsia kwa ujumla yamepungua.

Polisi wanawake kutoka kwenye kikosi cha FFU wakionyesha ukakamavu wakati wa sherehe za mtandao wa Polisi wanawake Geita.

Amesema matukio ya ukatili wa kijinsia yamepungua kwa asilimia 44 kwa kipindi cha mwaka mmoja, kutoka matukio 95 mwaka 2023 hadi 53 mwaka 2024.

Amesema miongoni mwa matukio ya ukatili yaliyokuwa yameshamiri dhidi ya wanawake ni yanayotokana na kipigo kikihusisha wivu wa mapenzi, ambavyo vilisababisha wanawake kuuawa.

“Kwa kushirikiana na wananchi na dawati la jinsia, elimu imesaidia kupunguza matukio haya. Kwetu ni mafanikio makubwa. Tumepunguza zaidi ya asilimia 50 ya matukio ya ukatili wa kijinsia ambayo yalijumuisha kujeruhi, mimba za utotoni na kutelekeza familia,” amesema.

Amesema elimu ya kupinga ukatili inayotolewa na uimarishwaji wa ulinzi na usalama unaofanywa na polisi kwa kushirikiana na wananchi ni chanzo cha kupungua kwa matukio hayo.

Jongo amesema elimu juu ya haki za binadamu na madhara ya ukatili wa kijinsia imesaidia watu kubadili mtazamo potofu.

Askari wanawake wa Mtandao wa Polisi Chato wakiwa kwenye maandamano kusherehekea siku yao.

Sababu nyingine amesema ni kuimarishwa kwa madawati ya kijinsia kwenye vituo vya polisi, ambayo yamesaidia waathirika kuripoti matukio kwa urahisi na kupata msaada haraka.

Akizungumzia mtandao wa polisi wanawake katika kupunguza ukatili kwa jamii, amesema umesaidia kwenda nyumba kwa nyumba kuzungumza na wanawake na kuwajengea uwezo wa kujitambua.

Kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya mwaka 2023, watu wazima 22,147 waliripotiwa kuathiriwa na matukio ya ukatili wa kijinsia ambao kati yao wanawake ni 13,322 na wanaume ni 8,825.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa ya kutokomeza uhalifu hasa matukio ya mauaji yaliyokuwa yameshamiri ndani ya mkoa huo.

Related Posts