Dar es Salaam. Katika muktadha wa maendeleo ya elimu na ajira, mjadala mjadala mzito kwa sasa nchini ni dhana ya usomi na nafasi ya elimu ya ufundi stadi.
Kwa muda mrefu, mfumo wa elimu nchini umeelemea zaidi katika usomi wa nadharia, hali ambayo imewafanya wahitimu wengi wa elimu ya juu kukosa ujuzi wa vitendo unaohitajika kwenye soko la ajira.
Hii imesababisha changamoto ya ajira kwa vijana wengi, huku fursa nyingi za kazi zikiendelea kuhitaji watu wenye ujuzi wa kiutendaji, badala ya maarifa ya kinadharia pekee.
Kutokana na mabadiliko ya mahitaji ya soko la ajira, elimu ya ufundi stadi imeanza kupewa kipaumbele kama suluhisho la tatizo hili.
Kupitia taasisi kama Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), Serikali inahamasisha vijana kupata ujuzi wa vitendo unaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri, juhudi zinazolenga kuwapa vijana maarifa yanayowawezesha kushindana katika uchumi wa sasa, ambapo ujuzi wa kiufundi unazidi kuwa hitaji muhimu kwa maendeleo binafsi na ya taifa kwa ujumla.
Mwanzoni mwa wiki hii, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa ziarani wilayani Nzega mkoani Tabora alizungumzia umuhimu huo, na kuibua mjadala mkubwa, uliojengwa kwenye dhana ya usomi na elimu ya Veta.
“Veta ile si tu kwa kijana wa darasa la saba, hata wewe uliyemaliza digrii, mtaalamu wa kompyuta, nenda kajifunze kushona nguo uwe fundi cherehani, nenda kajifunze ufundi umeme uwe fundi umeme,” alisema Majaliwa.
Waziri Mkuu aliongeza: “Kwa hiyo, mwanafunzi wa chuo kikuu anaweza kwenda kusoma Veta kwa sababu pale anasomea ufundi na ndiyo malengo ya Serikali ya kutoa fursa ya watu kusomea ujuzi na ufundi, ili uwasaidie kujianzishia shughuli za kiufundi ambazo zitakuletea kipato na kuendesha maisha yako.”
Kauli hiyo, iliibua mjadala na wapo walioipokea kwa mtazamo hasi, kwamba Serikali inaishusha hadhi elimu ya chuo kikuu.
Hii ni kutokana na dhana potofu kwamba elimu ya ufundi stadi ni kwa waliokosa fursa ya kusoma elimu ya juu, mtazamo ambao wadau wa elimu wanasema unapaswa kubadilika.
Kwa mujibu wa wadau, elimu ya ufundi si mbadala wa elimu ya juu, bali ni nyenzo muhimu inayoweza kusaidia hata wahitimu wa vyuo vikuu kupata maarifa ya vitendo kuwawezesha kujiajiri, kuajiriwa kwa urahisi au kuajiri watu wengine.
Wanaeleza mara nyingi wahitimu wa elimu ya juu huwa na ujuzi wa nadharia, lakini wanaukosa ule wa vitendo, unaohitajika kwenye soko la ajira.
Wadau hao wanaona vyuo vya ufundi stadi vinatoa maarifa ya vitendo yanayoweza kuwa suluhisho la changamoto ya ajira, hasa kwa wahitimu wa vyuo vikuu wanaokumbana na ugumu wa kupata kazi.
Kwa nyakati tofauti imetamkwa kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na vijana zaidi ya 850,000 wanahitimu masomo kila mwaka na kuingia kwenye soko la ajira lakini ni asilimia tano ndio wanaopata ajira ya kudumu na asilimia 35 wakijikita katika kilimo.
Kutokana na uwepo wao mitaani, nafasi chache za ajira zinapotangazwa na Serikali idadi kubwa hujitokeza kuziomba kama ilivyokuwa kwa watu 135,027 waliojitokeza kuomba nafasi 1,596 zilizotangazwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Februari 6, mwaka huu.
Hali kama hiyo ilijitokeza kwa kada ya elimu mapema mwaka huu na mara kadhaa Uhamiaji.
Hivi karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alisema wasailiwa 201,707 waliomba ajira kwa kada ya ualimu, huku nafasi zilizotangazwa zikiwa 14,648 pekee.
Kwa kuzingatia hilo, wadau wanashauri uwekezaji zaidi katika elimu ya ufundi stadi ili kutoa fursa kwa wahitimu wa elimu ya juu na ngazi nyingine za elimu kupata ujuzi wa vitendo, jambo litakalowasaidia kujitegemea kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Hilo linaungwa mkono na Meneja Uhusiano wa Veta makao makuu, Sitta Peter aliyelieleza Mwananchi kuwa kutokana na changamoto ya ajira, suluhisho ni kujiajiri badala ya kuendelea kusaka ajira.
“Katika kujiajiri, eneo ambalo lina fursa ni ufundi stadi kwa sababu mtu mwenye ujuzi ana fursa ya kujiajiri au kuajiriwa,” amesema.
Amesema mhitimu wa chuo kikuu ana fursa ya kujiajiri kwenye ufundi stadi kwa sababu tayari ana maarifa na mawazo mapana aliyoyapata chuoni, hivyo kupata urahisi kuanzisha mradi na kuuendesha vyema akipata ujuzi kutoka Veta.
“Veta tunawapokea vijana wengi wenye elimu ya juu ambao wanakuja kupata mafunzo ya muda mfupi, wanakwenda kuanzisha viwanda vyao.
“Tuna watu wamekuja kusomea useremala na wana elimu ya vyuo vikuu ili anapoanzisha kampuni mafundi wasimdanganye kwenye suala la vipimo na vifaa vinavyohitajika,” amesema.
Peter amesema si ajabu tena kwa mhitimu wa elimu ya juu kusoma Veta kwani zipo fani zaidi ya 80 ambazo zitamwezesha kujiajiri na kuajiri wengine.
Gregory Mlay, mhitimu wa shahada ya kwanza ya Tehema kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliyepata ya digrii pili nchini Japan, anasema baada ya kumaliza elimu ya juu alienda Veta kupata ujuzi.
“Niliona elimu yangu naweza kwenda kuitumia kwenye biashara ya mtu mwingine, lakini nilitaka kuanzisha kiwanda changu, hivyo nikaona niende Veta,” amesema.
Kwa sasa Mlay anaendeleza kampuni aliyoanzisha ya Fay Fashion inayojishughulisha na utengenezaji wa mabegi, mikanda, pochi na nguo kwa kutumia malighafi ya ngozi.
Mwanasiasa na waziri wa zamani, Profesa Anna Tibaijuka kupitia mtandao wa kijamii wa X ameunga mkono kauli ya Majaliwa akieleza umuhimu wa mafunzo ya Veta hata kwa wahitimu wa elimu ya juu.
Amesema elimu ya ufundi ni muhimu na ni ya kawaida katika nchi zilizoendelea.
Hata hivyo, Mtunzi wa vitabu na mdau wa elimu nchini, Richard Mabala amesema watu bado wana mtazamo hasi kuhusu mafunzo ya Veta kuwa ni ufundi wa hali ya chini.
Amesema mtazamo huo si sahihi, kwani mafunzo ya vyuo vya kati yapo ya aina mbalimbali.
“Lazima kujifunza kufanya vitu kwa vitendo, watu wawe huru kufuata vipaji vyao. Hakuna ubaya wa mtu kusoma Veta, wenye digrii Veta ndiyo ingekuwa chaguo lao la kwanza, ila walichagua chuo kikuu haraka kwa sababu kuna ufadhili wa Serikali,” amesema.
Mdau wa elimu Cathleen Sekwao vilevile amesema wahitimu wa vyuo wanapata nadharia zaidi, hivyo kupata ujuzi kupitia Veta si jambo la ajabu.
“Mara nyingi tumezoea wanaomaliza elimu ya msingi au wale ambao hawana cha kufanya ndio wanaenda Veta, sasa tukipanua wigo wa Veta kila mtu aende kusoma hata wenye elimu ya juu waende kuongeza ujuzi kama ziada,” amesema.
Amesema kupata ujuzi Veta si kwa ajili ya kuajiriwa au kujiajiri pekee, bali katika maisha ya kawaida ujuzi alioupata mtu unaweza kumsaidia popote.
“Kama una shahada na huna kazi unaweza kujiongeza kupata ujuzi mwingine na ukajiajiri kwa kufungua ofisi yako na kuanza kufundisha kupitia ujuzi ulioupata,” amesema.
Kwa mtazamo mwingine, Dk Edward Ngailo amesema mafunzo ya Veta lengo lake ni kutoa watenda kazi, tofauti na vyuo vikuu, ambavyo hutoa wasimamizi.
“Chuo kikuu hakitoi watenda kazi bali wasimamizi, ndiyo maana Veta wanaiita vyuo vya kati kwa maana watu wametoka kidato cha nne au cha sita wanakwenda huko, wakimaliza wanaenda chuo kikuu. Elimu ya Veta ni vitendo zaidi na chuo kikuu inakuwa nadharia,” amesema.
Dk Ngailo amesema mwanafunzi anapomaliza chuo kikuu na kurudi kupata mafunzo Veta, maana yake chuo alichohitimu hakijamsaidia kuwa mshindani sokoni.
Amesema inapotokea wahitimu wa vyuo kurudi kupata ujuzi Veta ni taa nyekundu kwa vyuo vikuu kutathmini mitalaa yake wapi wanapwaya.
“Kwa jicho lingine hii ni changamoto kwa vyuo kujitathmini, pia tunapaswa kupunguza idadi ya wanafunzi tunaowadahili kwenda vyuoni, tuwekeze zaidi kwenye vyuo vya kati,” amesema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Lawi Yohana amesema suala la ujuzi lipo kwenye sera ya elimu toleo la mwaka 2023 ambako ilisisitiza ujuzi na maarifa.
“Maana yake ni kwamba, endapo mtu yeyote atahitaji ujuzi au maarifa yoyote ambayo yanaweza kupatikana chuo cha Veta, basi aende akaupate. Ujuzi na maarifa anayopata mtu Veta vitamwezesha kujiajiri na kuajiri wengine,” amesema.
“Watu wanafikiri Veta ni ufundi boma tu, hapana. Kuna masuala ya muziki, ushonaji na uchoraji, vipo vitu vingi, wapo watu wana shahada lakini wanakwenda kuongeza maarifa na ujuzi na kwenda kuutumia kwenye kazi zao,” amesema.