Mkongomani Tabora kuiwahi Yanga | Mwanaspoti

KOCHA wa Tabora United, Mkongomani Anicet Kiazayidi anatarajiwa kuuwahi mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga utakaochezwa Aprili Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, baada ya kwenda kwao DR Congo kusoma.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Charles Obiny alisema licha ya kocha huyo kuondoka ila kuna uwezekano pia akauwahi mchezo na Yanga, unaotazamiwa kuleta ushindani mkubwa kutokana na timu hizo zilipokutana mechi ya mzunguko wa kwanza.

“Matumaini yetu hadi kufikia Aprili Mosi atakuwa amejiunga na timu, suala la yeye kufukuzwa kama linavyozungumzwa kwangu halijanifikia ila ninachotambua alituaga anakwenda kufanya kozi yake ya refreshi tu na wala sio vinginevyo,” alisema kiongozi huyo. 

Obiny raia wa Kenya, alisema hawana mpango wa kumfukuza kwani anaendelea kupigania malengo ya kikosi hicho ya kumaliza wakiwa nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi.

Anicet aliyezifundisha AS Vita Club, FC Simba Kolwezi, FC Les Aigles du Congo na Maniema Union za kwao DR Congo, tangu ajiunge na kikosi hicho Novemba 2, 2024, amepoteza michezo miwili tu ya Ligi Kuu Bara kati ya 14, aliyoiongoza.

Kocha huyo tangu ajiunge na timu hiyo akichukua nafasi ya Francis Kimanzi aliyetimuliwa Oktoba 21, mwaka jana kutokana na mwenendo mbaya, ameiongoza Tabora United michezo 14, ameshinda saba, sare mitano na kuchapwa miwili.

Katika michezo hiyo saba, Tabora ilizifunga Mashujaa FC bao 1-0, ikaifunga Yanga mabao 3-1, ikashinda 2-0, mbele ya KMC, na 2-1 dhidi ya Azam FC, ikaichapa Namungo FC 2-1, Kagera Sugar 2-1, kisha Dodoma Jiji bao 1-0, Februari 28, mwaka huu.

Michezo mitano ya sare ni dhidi ya Singida Black Stars ya mabao 2-2, Coastal Union (1-1), KenGold (1-1), Fountain Gate (0-0) na Tanzania Prisons (1-1), huku vichapo ni (3-0) dhidi ya Simba na (2-1) dhidi ya JKT Tanzania, Machi 7.

Mchezo wa mzunguko wa kwanza Uwanja wa Azam Complex, Tabora ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Yanga, Novemba 7, 2024, ikiwa ni kichapo kilichomfanya aliyekuwa Kocha wa Yanga, Muargentina Miguel Gamondi kuondolewa kikosini.

Related Posts