Profesa Janabi rasmi kuwania ukurugenzi WHO, kuchuana na hawa

Dar es Salaam. Profesa Mohamed Janabi, ametangazwa rasmi kuwa mmoja wa wagombea watano kwa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Taarifa hiyo imetangazwa rasmi katika mtandao wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika na sasa umma unaweza kusoma wasifu wa kila mgombea kwa lugha tatu (Kiingereza, Kifaransa na Kireno).

Kwa mujibu wa tangazo lilitolewa na Ofisi ya WHO ya Kanda ya Afrika, majina ya wagombea hao watakaoshiriki katika mchakato wa uchaguzi Mei 18, 2025, yalichakatwa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Janabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), anawania nafasi hiyo akiwa sambamba na wagombea wengine wanne wote kutoka nchi za Afrika Magharibi.

Orodha ya wagombea inajumuisha Dk N’da Konan Michel Yao kutoka Ivory Coast, Dk Dramé Mohammed Lamine kutoka Guinea, Dk Boureima Hama Sambo kutoka Niger na Profesa Mijiyawa Moustafa kutoka Togo.

Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Dk Faustine Ndugulile aliyefariki dunia Novemba 27, 2024 wakati akijiandaa kuanza kazi hiyo rasmi Machi, 2025. Baada ya kifo hicho Tanzania ilipendekeza Profesa Janabi kupeperusha bendera ya Tanzania kwa mara nyingine.

Uteuzi wa mbeba bendera wa Tanzania, ulitangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa uzoefu wa Profesa Janabi katika sekta ya afya unamfanya kuwa mgombea mwenye sifa stahiki kwa nafasi hiyo muhimu kimataifa.

Kwa mtazamo wa wengi, Profesa Janabi ni kiongozi wa afya mwenye ushawishi mkubwa, akichangia maendeleo ya tiba, elimu ya afya na utawala wa sekta ya matibabu, sio tu Tanzania bali pia kimataifa.

Ikiwa atapata nafasi hiyo ndani ya WHO, atakuwa Mtanzania mwingine aliyeandika historia katika sekta ya afya ulimwenguni.

Profesa Mohamed Yakub Janabi, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na msomi mashuhuri wa Tanzania, anaendelea kuandika historia katika sekta ya afya endapo ataaminiwa kama ambavyo Afrika ilimwamini hayati Dk Ndugulile.

Kwa sasa, anahudumu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) tangu Oktoba 2022 na pia ni Mshauri wa Rais wa Tanzania kuhusu afya na matibabu.

Profesa Janabi ana rekodi ya kitaaluma inayovutia, akiwa amepata elimu kutoka taasisi mbalimbali mashuhuri duniani. Alipata Shahada ya Udaktari wa Tiba (MD) kutoka Chuo Kikuu cha Matibabu cha Kharkiv, Ukraine. Aliendelea na Shahada ya Uzamili katika Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Queensland, Australia, chini ya Profesa Ian Riley.

Alihitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika magonjwa ya moyo na baadaye alifanya mafunzo ya kitabibu katika Chuo Kikuu cha Osaka, Japan, kupitia ufadhili wa Japan Society for Promotion of Science, chini ya Profesa Yuji Matsuzawa.

Uzoefu wa kitaaluma na utawala

Katika sekta ya afya, Profesa Janabi ameonesha weledi mkubwa katika nyadhifa mbalimbali:

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH tangu 2022.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) tangu 2015 hadi 2022, ambapo alihusika katika kuifanya JKCI kuwa moja ya vituo bora vya matibabu ya moyo Afrika Mashariki.

Daktari binafsi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete tangu mwaka 2005.

Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) tangu mwaka 2000.

Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tiba cha South Carolina, Marekani, tangu mwaka 2003.

Ushiriki katika tafiti na utawala

Mbali na utawala wa hospitali, Profesa Janabi ni mwanataaluma na mtafiti aliyebobea. Ni Mjumbe wa Baraza la Muhas, Mjumbe wa Bodi ya JKCI, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).

Amefanya tafiti mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwa Mtafiti Mkuu katika utafiti wa chanjo ya Ukimwi wa TaMoVac kati ya 1998 na 2002. Ameshachapisha zaidi ya makala 83 za kisayansi katika sekta ya afya.

Profesa Janabi ana uwezo wa kuwasiliana katika lugha nne ikiwamo lugha yake mama Kiswahili, Kiingereza, Kirusi na Kijapani, jambo linalomwezesha kushirikiana na wataalamu wa afya duniani. Pia, alihudumu kama Mkurugenzi wa Matibabu wa Madaktari Afrika, katika shirika la Marekani linaloshirikiana na mifumo ya afya ya Tanzania.

Related Posts