Rais Samia anavyopigania kuirejesha Tanga ya viwanda

Na: Dk. Reubeni Lumbagala

Mkoa wa Tanga una historia kubwa katika nchi yetu ya Tanzania. Moja ya historia kubwa ni kuwa mkoa uliokuwa na viwanda vingi katika miaka ya 1970 na 1980. Viwanda hivi vilikuwa nyenzo muhimu ya kuchagiza maendeleo ya Tanga kwa kuzingatia mnyororo mkubwa wa thamani uliopo kwenye viwanda. 

Ni katika viwanda hivyo ndipo kulipoibuka fursa za serikali kuongeza mapato, kuongezeka ajira, biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya sekta nyingine kama kilimo, biashara na miundombinu. Vilevile viwanda viliongeza uboreshaji wa huduma za kijamii kama umeme na maji ndani ya mkoa wa Tanga. Kiujumla, uwepo wa viwanda Tanga kuliambatana na neema kubwa na mafanikio tele.

Kufa kwa viwanda vingi mkoani Tanga kumezorotesha maendeleo na kusababisha wananchi wengi kupotezea ajira zao na serikali kukosa mapato yatokanayo na kodi viwandani. Kutokana na hali hii, juhudi za makusudi za kuirejesha Tanga ya viwanda inapaswa kuchukuliwa. 

Ni faraja kuona Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameonyesha nia njema ya kutaka kufufua viwanda, kutanua viwanda vilivyopo na kuongeza viwanda vipya Tanga kwa ushirikiano mkubwa na sekta binafsi ili Tanga ya viwanda isiwe jambo la historia tena wala la kutafuta kwa tochi bali liwe jambo halisi la kuonekana kwa macho ya kila mtu. Basi.

Akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Kiwanda cha Chokaa na Saruji cha Maweni Limestone Februari 27, 2025, jijini Tanga, Rais Samia alisema ” Sote tunakumbuka Tanga ya zamani, Tanga ya viwanda na Tanga ambayo ilikuwa inatupa fahari Wana Tanga kwamba sisi Wana Tanga ni watu wa viwanda, Kwa bahati mbaya Tanga ya viwanda ilipotea lakini dhamira ya serikali ni ile ile kuirudisha Tanga kuwa Tanga ya viwanda na hilo tunaendelea kulifanyia kazi.”

Februari 28, 2025, akiwa katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani Tanga katika viwanja vya CCM Mkwakwani, Rais Dk. Samia alirudia kauli yake ya kutaka kuirejesha Tanga ya viwanda huku akieleza matamanio yake ni kuona Tanga ya viwanda inarejea ili kuchochea maendeleo mkoani humo. 

“Ndoto yangu ni kufanya mkoa wa Tanga kuwa wa viwanda kwa kuweka sera thabiti zitakazovutia wawekezaji na kuhakikisha wananchi wananufaika na fursa za ajira,” amesema.

KIWANDA KIKUBWA CHA SUKARI YA VIWANDANI KUJENGWA TANGA

Februari 26, 2025, akiendelea na ziara yake wilayani Pangani mkoani Tanga, Rais Dk. Samia alieleza dhamira ya serikali ya kujenga kiwanda kikubwa cha sukari ya viwandani Tanga ili kukabiliana na uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi huku mashamba makubwa ya miwa yakitarajiwa kuanzishwa wilayani Pangani.

  “Pangani inabadilika na itaendelea kubadilika kwa sababu tunakwenda kuja na kilimo kikubwa cha miwa ndani ya Pangani na kiwanda cha sukari tunajenga Tanga Jiji. Tunajenga viwanda vingi vya sukari ili kujitosheleza mahitaji yetu na kuweza kuhifadhi sukari na kiwanda hicho kitajengwa karibu na Bandari ya Tanga na shamba litakuwa Pangani na kufungua fursa za ajira za Tanga,” amesema Rais Dk. Samia.

UMMY MWALIMU AOMBA VIWANDA VIFUFULIWE TANGA

Februari 28, 2025, ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya Rais Samia mkoani Tanga, katika viwanja vya CCM Mkwakwani, Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu, alipata wasaa wa kutoa salamu za wananchi wa Tanga Mjini ambapo alieleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa wananchi wake huku akitoa maombi kadhaa kwa Rais ili yafanyiwe kazi. Miongoni mwa maombi hayo ni ufufuaji wa viwanda Tanga ili kuongeza fursa za maendeleo mkoani humo.

 “Mama tunaomba utubebe, utushike mkono tufufue viwanda vya Tanga – kiwanda cha chuma, kiwanda cha mbolea, kiwanda cha saruji, kiwanda cha mablanketi na nguo, pamoja na viwanda vya sisal (katani/mkonge), vijana wetu, wakina baba, kina mama watapata ajira,” amesema Ummy Mwalimu.

Ombi la Mbunge Ummy Mwalimu la kukufua viwanda Tanga lilipata majibu mazuri kutoka kwa Rais Samia ambaye alisema ni matamanio yake kuiona Tanga ya viwanda ikirejea huku akieleza namna serikali yake ilivyoweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ili kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vingi. 

“Tanga ninayoitamani ni kuirudisha Tanga ya viwanda kama ilivyokuwa zamani hili ni tamanio langu kubwa na kuna hatua tunachukua tunalegeza masharti ya uwekezaji ili wawekezaji waje kwa wingi ili vijana wetu wapate ajira na Tanga kusiwe na watu wa kukaa vijiweni,” alisisitiza Rais Dk. Samia.

Sambamba na hilo, April 24, 2024, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa mkoani Tanga katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye mradi wa jengo la kitega uchumi la Halmashauri ya Jiji la Tanga alisema “Tumefufua viwanda vingi vya mkonge, zao ambalo lilikufa kabisa katika wilaya zote mkoani hapa, sasa Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia kuvifufua ili kuingia kwenye uchumi wa viwanda.”

Niendelee kusisitiza serikali, kuirejesha Tanga ya viwanda ili kuharakisha maendeleo ya mkoa na Taifa pia. Tanga bila viwanda, ni Tanga bila uchumi. Rais Dk. Samia hili la kuirejesha Tanga ya viwanda itafanya jina lako liandikwe kwa wino wa dhahabu katika mioyo ya Wana Tanga na itakuwa alama isiyofutika daima.

Maoni: 0620 800 462

Related Posts