Dar es Salaam. Wakati jitihada zikifanyika kuhakikisha jamii inahamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeonyesha kuwapo ongezeko la mauzo ya mkaa nchini.
Ripoti ya BoT inayoangazia uchumi wa kikanda ya robo mwaka ulioishia Septemba, 2024 inaonyesha mkaa kuwa miongoni mwa mazao ya misitu ambayo mauzo yake yalifikia Sh5.73 bilioni ikiwa ni ongezeko kutoka Sh2.94 bilioni kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.
Kilichoonekana katika ripoti hii iliyochapishwa Machi mwaka huu kwenye tovuti ya BoT kimewafanya wadau wa uchumi kupendekeza njia zinazoweza kupunguza matumizi ya mkaa kuwa ni kutoa elimu zaidi kuhusu matumizi ya nishati safi kwa wananchi, kuangalia namna ya kupunguza bei na kurahisisha upatikanaji wake.
Mauzo hayo ya mkaa yaliyokuwapo Septemba 2024 ni ongezeko la zaidi ya asilimia 100 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia lakini ni pungufu kwa asilimia 39.30 ikilinganishwa na yale yaliyokuwapo katika robo ya mwaka ulioishia Juni 2024.
Kwa sasa Tanzania inahamasisha matumizi gesi ya kupikia, ikitekeleza mkakati kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanahamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Mkakati huo unakwenda sambamba na kampeni za ugawaji mitungi ya gesi kwa wananchi kuwawezesha kuhamia kwenye matumizi ya nishati hiyo badala ya mkaa na kuni.
Ripoti ya BoT inaonyesha mauzo makubwa ya mkaa yalifanyika katika kanda ya kusini mashariki ambako thamani ya jumla ilikuwa Sh3.68 bilioni ikiwa ni sawa na asilimia 64.22 ya mauzo yaliyofanyika nchi nzima.
Kanda ya kati ilifuatia ikiwa na mauzo ya mkaa ya Sh856.6 milioni, ya tatu ikiwa kanda ya kaskazini ikiwa na mauzo ya Sh775.6 milioni.
Kanda za ziwa na Dar es Salaam zilikuwa na kiwango kidogo cha Sh410.9 milioni na Sh12.6 milioni mtawaliwa.
Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka amesema bado Watanzania wengi wanaishi vijijini, hivyo kuna haja ya kuangalia namna ya kuleta hamasa kwenye matumizi ya majiko banifu yenye matumizi kidogo ya mkaa na kuni, ili kupunguza kiwango kinachotumika sasa.
Amesema hilo liende sambamba na kuongeza nguvu katika kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala, ikiwemo inayotokana na mabaki ya mimea na kilimo.
Kwa kufanya hivyo amesema kutapunguza matumizi ya mkaa unaotokana na miti moja kwa moja.
“Ni vyema mikakati inayowekwa iguse mijini na vijiji. Isikae mjini tu iguse mazingira halisi ili kuwe na njia halisi kulingana na maeneo husika, hii itasaidia kupunguza matumizi ya nishati isiyofaa na baadaye watu kutumia nishati safi,” amesema.
Amesema elimu inatakiwa iendelee kutolewa zaidi, akieleza mapokeo hayawezi kuwa ya ghafla kwani watu bado wanachanganya nishati zote majumbani kwa kuona baadhi ya vitu hawawezi kupika kwa gesi, ikiwemo maharage.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini Tanzania (Repoa), Dk Donald Mmari amesema jambo hilo ni ishara kuwa elimu haijawafikia wananchi wa vijijini hasa katika upande wa athari za kutumia mkaa.
“Bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuwashawishi wananchi. Kuwapa faida ni jambo la kwanza lakini upatikanaji wa nishati mbadala ni kitu kingine,” amesema.
Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora amesema ni vyema ufanyike utafiti kujua uwezo wa Watanzania ili bei ya nishati ya gesi iendane na hali zao.
Katika mtazamo mwingine amesema njia pekee inayoweza kusaidia kupunguza matumizi ya mkaa ni kufanya bei yake kuwa kubwa kuliko gesi.
“Gesi ni gharama kuanzia kuchakata na kusafirishwa lakini mkaa unapatikana karibu na bure, hadi tuwe na uwezo wa kufanya mkaa uwe na gharama kubwa kuliko gesi ndipo tunaweza kuona mabadiliko ya haraka ambayo hayatakuja leo. Watanzania tuko wengi, tunazidi kuzaliana na uwezo wetu wa kununua bado ni mdogo hali hii itafanya mabadiliko kuwa kidogokidogo,” amesema.
Profesa Kamuzora ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi amesema ni vyema tafiti kama hiyo ikafanyika kwa wafanyabiashara, wakiwamo mama lishe mijini kujua kati ya matumizi ya gesi na mkaa kipi kinampa ahueni anapotumia.
“Huenda mkaa bado unaonekana kuwa rahisi kuliko kutumia gesi, kampeni iendelee lakini pia tupambane kukuza vipato vya wananchi ili kuongeza njia ambayo tunaweza kufanya watu wapate kazi waweze kutumia gesi, ukimgawia leo (mtungi wa gesi) kesho ikiisha ataona bei ni kubwa na mkaa ni bei ndogo anarudi kwenye mkaa,” amesema.
Dk Mmari amesema ni vyema kuhakikisha katika maeneo mbalimbali hasa yale ya vijijini wananchi wanakuwa na uwezo wa kufikia nishati mbadala kwa urahisi na gharama zake ziwe nafuu.
“Hili litawezekana kwa kuangalia gharama katika uchukuzi, uzalishaji, teknolojia inayotumika katika uzalishaji ili watu wa vipato vya chini waweze kumudu gharama hizo,” amesema.
Dk Lutengano anazungumzia bei akisema iangaliwe. Amesema kupungua kwake kunaweza kufanya watu wengi zaidi kuhamasika kutumia gesi.
“Kodi ziangaliwe vizuri ili nishati iwe nafuu zaidi mtu atumie, kwani kugawa mitungi ni hatua moja ila kama gharama ni kubwa inafanya mtu abaki katika kitu ambacho ni nafuu. Ikiwa nafuu watu watatumia na kuchagua kulingana na kile ambacho wanafanya,” amesema.
Katika hatua nyingine, ripoti hiyo ya BoT inaonyesha kuendelea kuimarika kwa mauzo ya mazao mengine ya misitu, mbao ikiendelea kuwa kinara kwa kubeba asilimia kubwa ya mauzo katika robo ya mwaka iliyoishia Septemba 2024.
Hiyo ni baada ya kubeba asilimia 71.15 ya mauzo yote ikiwa na jumla ya Sh179.8 bilioni kati ya mauzo yote ya Sh252.78 bilioni.
Mauzo ya mbao ni pungufu kwa asilimia 13.34 ikilinganishwa na Sh207.59 zilizokuwapo kipindi kilichotangulia.
Nguzo za umeme, mauzo yake yalikuwa Sh33.92 bilioni ikiwa ni ongezeko kutoka Sh32.57 iliyokuwapo Septemba, 2024, mbao kwa ajili ya kutengenezea samani mauzo yake yalikuwa Sh708.5 milioni kutoka Sh419 katika kipindi kilichopita.
Mauzo ya magogo yalifikia Sh2.98 milioni kutoka Sh2.32 milioni, huku ya bidhaa nyingine za misitu yakifikia Sh29.29 milioni kutoka Sh29.42 milioni.