Tanzania kushirikiana na Barbados kukuza sekta ya utalii

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Mottley ambapo wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika makazi rasmi ya Waziri Mkuu, Mia Mottley, jijini Bridgestone, nchini Barbados.

Waziri Mkuu Mia amesema, kuna umuhimu wa kuwa na mkakati wa pamoja na kushirikiana kwa lengo la kukuza utalii kati ya Barbados na Tanzania na nchi za Afrika Mashariki kwa ujumla. Amesema kuna maeneo mengi ya vivutio vya utalii ambavyo vinaweza kuzinufaisha pande hizo mbili yakiwemo masuala ya ukarimu.

Maeneo mengine ya ushirikiano ni katika utoaji wa mafunzo ya ufundi kati ya nchi za Carib (Caribbean) akisisitiza kuwa umuhimu wa uboreshaji wa masoko na kubadilishana wataalamu katika sekta mbalimbali kwa makubaliano maalumu.

Aidha, amesema upo uhitaji wa wataalamu katika sekta ya maji na miundombinu, hivyo kuna uwezekano wa kubadilishana ili kujengeana uzoefu katika sekta mbalimbali kulingana na makubaliano yatakayofikiwa.

Kwa upande wake, Dk Biteko amesema mapendekezo hayo ni mazuri na yanaweza kuwa matokeo chanya baada ya kuchambuliwa na watalaamu katika sekta husika kupitia wizara zinazohusika na masuala ya kidiplomasia.

Dk Biteko amesema Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais, Samia Suluhu Hassan inaendeleza kampeni ya nishati safi ya kupikia, ambayo inalenga kuwawezesha asilimia 80 ya watumiaji wa nishati kuondokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi ifikapo mwaka 2034.

Katika utekelezaji wa mpango huo, amesema Tanzania inatembea kifua mbele kunadi mkakati huo wa miaka 10 ambao pamoja na mambo mengine unakusudia kupunguza madhara kwa watumiaji wa nishati isiyokuwa safi inayosababisha uchafuzi wa mazingira, magonjwa ya kupumua pamoja na vifo.

“Januari mwaka huu tumekuwa na mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika (M300) uliofanyika jijini Dar es Salaam ukilenga kuwawezesha watu milioni 300 barani Afrika wasiokuwa na umeme kupata haki hiyo, ikiwa ni miaka mitano kuanzia sasa na baada ya hapo itaweka namna ya kusonga mbele kulingana na matokeo yanayofikiwa” amesema Dk Biteko.

Dk Biteko amefafanua kuwa, hatua ya Tanzania kushiriki katika mkutano wa nishati endelevu kwa wote (SEforALL) uliofanyika nchini Barbados, ni kuthibitisha nia yake thabiti inayolenga matokeo chanya. Hivyo, amesema yapo maeneo mengi ya kushirikiana na kuwezesha wananchi wa pande zote mbili kupata maendeleo na ustawi wa pamoja.

Mkutano wa viongozi hao wawili umehitimisha ziara ya kikazi ya Dk Biteko na ujumbe wake nchini humo,  ambako alishiriki katika kongamano la kimataifa la nishati endelevu kwa wote pamoja na mikutano ya wadau mbalimbali,  iliyojikita katika uboreshaji wa sekta ya nishati kwa manufaa ya nchi hizo mbili.

Katika ziara hiyo, Dk Biteko, alifuatana na Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shaibu Hassan Kaduara, Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felichesmi Mramba na Mshauri wa Rais katika masuala ya Nishati na Maendeleo ya Jamii, Angellah Kairuki.

Related Posts