TET yazindua maabara mbili za kompyuta Tanga

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), imezindua maabara ya Kompyuta ya vifaa vya kisasa vyenye gharama ya Sh milioni 235.5 katika shule mbili wilayani Lushoto, mkoani Tanga.

Shule hizo ni Sekondari ya Magamba na Shule ya Msingi Shukilai ambapo maabara hizo zinalenga kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ufundishaji na ujifunzaji.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Baraza la TET, Profesa Maulid Mwatawala amesema uwepo wa maabara hizo ni kuunga mkono kwa vitendo utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 ambayo inasisitiza matumizi ya teknolojia ya habari kwa kiasi kikubwa katika ujifunzaji kwa wanafunzi.

“Sera hii ya elimu imesisitiza matumizi ya Tehama katika kujifunza sanjari na utoaji wa mafunzo na sasa tumekuja katika shule hizi mbili kutoa vifaa hivyo kwa ajili ya kuchagiza utekelezaji wa sera hiyo kwa vitendo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba amesema maabara hizo zimepatikana kwa ushirikiano wa TET na Korea ya Kusini kupitia programu ya KLIC (Korean e-Learning Improvement Cooperation) ambapo pia ni mwendelezo wa matukio kuelekea Maadhimisho ya Miaka 50 ya TET iliyozinduliwa rasmi Machi 7, mwaka huu na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa jijini Dar es Salaam.

“Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuimarisha uhusiano mzuri kati ya Tanzania na nchi mbalimbali ikiwemo Korea ya Kusini ambao umefanikisha TET kuingia makubaliano ya ushirikiano huu uliosaidia kupatikana kwa vifaa hivi vya TEHAMA.

“Programu ya KLIC ina lengo la kuwajengea uwezo walimu katika kufundisha kwa kutumia TEHAMA na kuhakikisha kuwa shule zetu zinakuwa na vifaa vya kisasa vya kielektroniki kwa ajili ya kujifunza na kufundishia. Program hii ni ya miaka mitano na ilizinduliwa rasmi Mwaka 2022,” amesema Dk. Aneth.

Amesema katika kipindi cha miaka minne tangu kuzinduliwa kwake mambo mbalimbali yamefanyika ikiwamo washiriki 80 wakiwamo wakuza mitaala 40 na walimu wa shule za msingi na sekondari 40, walipata mafunzo ya namna ya kuandaa maudhui ya kidigitali na kutumia TEHAMA katika kufundishia na kujifunzia.

“Mafunzo hayo yalitolewa kwa njia ya mtandao kupitia walimu wabobezi wa Taasisi ya Kielimu ya Mji wa Gwangju Korea Kusini. Mwaka 2023 washiriki 18, walimu 11 na wakuza mitaala 07 walishiriki. Mwaka 2024 washiriki 23, walimu 20 , wakuza mitaala watatu waliwezeshwa na Mwaka 2025 tunatarajia kuwawezesha washiriki wengine 20, ambapo walimu ni 10 na wakuza mitaala 10,” amesema.

Dk. Aneth amesema pamoja na mafunzo hayo, shule zinazoshiriki katika mradi huo zimekuwa zikipokea vifaa mbalimbali vya TEHAMA ambapo amezitaja shule ambazo zimekwisha nufaika na programu hiyo ni shule ya ya Msingi Tegeta A na Sekondari Kimbiji za Mkoa wa Dar es Salaam, Mabatini Sekondari na Mkombozi shule ya msingi zilizoko za Mkoa wa Njombe.

Pamoja na mambo mengine, Dk. Aneth ametaja vifaa vilivyotolewa katika Shule za Magamba na Shukilai ni Seti ya Kompyuta 26, Monitor 26, mashine ya kurudufu moja, projekta skrini moja, projekta moja, madawati ya wanafunzi 13. viti vya wanafunzi 25, dawati la mwalimu moja. kiti cha mwalimu kimoja, lectern ya mwalimu moja, podium ya kidigitali , UPS 26 mausi ya mwalimu isiyo ya waya moja, kibodi ya mwalimu isiyo ya waya moja, pointa moja na mplifaya ya kisasa moja.

Licha ya utoaji wa vifaa, programu ya KLIC imewapatia walimu fursa ya kuhudhuria mafunzo ya muda mfupi nchini Korea Kusini ambapo mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea weledi na kuwawezesha kuleta mbinu bunifu darasani ambapo kwa mwaka huu, walimu kutoka Magamba Sekondari na Shukilai Sekondari watapata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo, hatua itakayosaidia kuboresha matumizi ya TEHAMA.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Tanga, Aileen Makungu alisema kuwa maabara hizo zitasaidia walimu kufundisha watoto wengi kwa wakati mmoja hususani katika shule zenye changamoto ya uhaba wa walimu.


 

Related Posts