Trump, Iraq watangaza kumuua kiongozi wa Islamic State

Baghdad. Idara ya Ujasusi ya Iraq kwa kushirikiana na majeshi ya Muungano yanayoongozwa na Marekani imeendesha operesheni iliyofanikisha kuuawa kwa kiongozi wa kundi la Islamic State (ISIS) nchini Iraq na Syria.

Taarifa ya kuuawa kwa Abdallah Maki Mosleh al-Rifai, maarufu kama “Abu Khadija,” imetangazwa jana Ijumaa Machi 14,2025, na Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia al-Sudani, kupitia chapisho lake kwenye mtandao wa X (zamani Twitter).

“Iraq inaendelea kushinda vikosi vya giza na ugaidi,” ameandika al-Sudani katika taarifa iliyochapishwa kwenye X.

Kundi la ISIS linatajwa na Marekani kuwa kundi la wanamgambo na moja ya makundi ya kigaidi hatari zaidi nchini Iraq na duniani.

Katika jukwaa lake la Truth Social usiku wa Ijumaa, Rais wa Marekani Donald Trump alisema : “Leo, kiongozi mtukutu wa ISIS nchini Iraq ameuawa. Alifuatiliwa bila kuchoka na wapiganaji wetu hodari” kwa ushirikiano na serikali ya Iraq na serikali ya wapiganaji wa Kikurdi katika kanda hiyo.

Ofisa mmoja wa usalama alisema operesheni hiyo ilifanyika kwa kutumia shambulio la anga katika jimbo la Anbar, Magharibi mwa Iraq.

Ofisa mwingine alisema operesheni hiyo ilifanyika usiku wa Alhamisi, lakini kifo cha al-Rifai kilithibitishwa Ijumaa.

Vyanzo hivyo vilitoa taarifa hizo kwa sharti la kutotajwa majina kwa kuwa hawakuruhusiwa kulizungumzia hadharani.

Tangazo hilo lilikuja siku hiyohiyo ya ziara ya kwanza ya mwanadiplomasia mkuu wa Syria nchini Iraq, ambapo nchi hizo mbili ziliahidi kushirikiana katika kupambana na wapiganaji wa ISIS.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Fouad Hussein, alisema katika mkutano wa waandishi wa habari kuwa kuna changamoto za pamoja zinazokabili jamii za Syria na Iraq, hususan zinazosababishwa na magaidi wa ISIS.

“Maofisa walijadili kwa kina harakati za ISIS, iwe kwenye mpaka wa Syria na Iraq, ndani ya Syria au ndani ya Iraq” alisema Hussein, wakati wa ziara hiyo.

Hussein alitaja jengo maalumu la kuratibu operesheni lililojengwa kwa ushirikiano wa Syria, Iraq, Uturuki, Jordan na Lebanon katika mkutano wa hivi karibuni huko Amman, ili kukabiliana na ISIS huku akisema kuwa kitaanza kazi hivi karibuni.

Uhusiano kati ya Iraq na Syria umekuwa na mvutano fulani baada ya kuanguka kwa rais wa zamani wa Syria, Bashar al-Assad.

Al-Sudani aliingia madarakani kwa msaada wa muungano wa makundi yanayoungwa mkono na Iran, huku Tehran ikiwa mshirika mkuu wa Assad.

Rais wa mpito wa Syria kwa sasa, Ahmad al-Sharaa hapo awali alijulikana kama Abu Mohammed al-Golani na alipigana kama mpiganaji wa al-Qaida nchini Iraq, baada ya uvamizi wa Marekani wa 2003, kisha baadaye akapigana dhidi ya Serikali ya Assad nchini Syria.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa mpito wa Syria, Asaad Hassan al-Shibani, alisisitiza uhusiano wa kihistoria kati ya nchi hizo mbili.

“Katika historia yote, Baghdad na Damascus zimekuwa miji mikuu ya ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu, zikishirikiana katika maarifa, utamaduni na uchumi.

“Kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili hakuwezi tu kunufaisha watu wetu, bali pia kutachangia katika uthabiti wa eneo hili, kutufanya tusiwe tegemezi kwa nguvu za nje na kuwa na uwezo zaidi wa kuamua hatima yetu wenyewe,” aliongeza.

Operesheni na ziara hiyo zinakuja wakati ambapo maofisa wa Iraq wana wasiwasi juu ya kuzuka upya kwa mapigano ya ISIS kufuatia kuanguka kwa utawala wa Rais Assad nchini Syria.

Ingawa watawala wapya wa Syria wanaoongozwa na kundi la zamani la waasi la Hayat Tahrir al-Sham, wamekuwa wakifuatilia masalia ya ISIS tangu walipochukua madaraka, baadhi wana hofu kuwa kutakuwa na mvurugiko wa usalama unaoweza kuruhusu kundi hilo kujipanga na kurejea upya.

Marekani na Iraq zilitangaza makubaliano mwaka jana ya kumaliza operesheni ya kijeshi ya muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya ISIS nchini Iraq ifikapo Septemba 2025, huku vikosi vya Marekani vikiondoka katika baadhi ya kambi ambako wamekuwa wakikaa kwa miaka ishirini.

Wakati makubaliano hayo yakifikiwa, viongozi wa kisiasa wa Iraq walisema kuwa tishio la ISIS lilikuwa limedhibitiwa na hawakuhitaji tena msaada wa Washington kupambana na seli zilizobaki.

Lakini kuanguka kwa utawala wa rais Assad Desemba, 2024, kumesababisha baadhi ya viongozi kufikiria upya msimamo huo, ikiwa ni pamoja na wanachama wa Muungano wa Uratibu (Coordination Framework), muungano wa vyama vya Kisheia vinavyoungwa mkono na Iran, ambao ulimuweka Waziri Mkuu wa sasa wa Iraq, Mohammed Shia al-Sudani, madarakani mwishoni mwa 2022.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Related Posts