JUMATANO Machi 12, mwaka huu, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia alifanikiwa kupigiwa kura za ndio zilizomuwezesha kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Ushindi huo umemfanya Karia kuwa Mtanzania wa tatu kuhudumu katika nafasi hiyo akitanguliwa na hayati Said El Maamry na Leodegar Tenga ambao walipata fursa hiyo kwa nyakati tofauti.
Karia ameshinda nafasi hiyo akiwa mwakilishi wa Kanda ya Soka ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) na washindi wengine na kanda zao ni Samuel Eto’o (Uniffac), Kurt Okraku (Wafu B), Feizal Sidat na Samir Sobha (Cosafa) na Bestine Kazadi Ditabala (Uniffac).
Kwa mujibu wa katiba ya CAF, majukumu ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni kutekeleza sera na uamuzi wa mkutano mkuu, uongozi na utawala wa shirikisho hilo, kuchukua uamuzi wa masuala yote ambayo hayapo chini ya mamlaka ya mkutano mkuu wa CAF.
Pia hukaimisha majukumu kwa wanachama na watendaji wa shirikisho na kupendekeza ajenda za mkutano mkuu wa taasisi hiyo inayoongoza mpira Afrika.
Majukumu mengine ni kumuondoa mjumbe wa miongoni mwa kamati za kudumu za CAF, ndio wenye uamuzi wa mwisho wa masuala yote yanayohusu mashindano yaliyo chini ya shirikisho hilo, kuteua na kuondoa katibu mkuu wa CAF, kupanga tarehe na mahali pa mashindano yake.
Pia ni kuthibitisha chati ya utawala ya shirikisho hilo na kuthibitisha kanuni zinazoongoza CAF isipokuwa zile zilizo chini ya mamlaka ya mkutano mkuu.

Kwa Karia kuwepo ndani ya kamati ya utendaji ya CAF, maana yake Tanzania sasa ina fursa ya kufikisha ajenda zake katika mkutano mkuu wa shirikisho hilo, ambayo mwanzoni ilikuwa ngumu kufanyika hilo kwa vile haikuwa na mtu ndani ya Kamati ya Utendaji ya CAF ambayo kwa mujibu wa katiba ya shirikisho hilo, ni mjumbe wake tu mwenye mamlaka ya kufanya hivyo.
Tanzania sasa ina fursa kubwa ya kunufaika na fursa za kuandaa mashindano makubwa ya soka Afrika, mikutano na matukio ya CAF na pia marefa au maofisa wa shughuli tofauti za kisoka kunufaika kwa kuteuliwa kusimamia mechi na matukio mbalimbali ya CAF kwa vile Karia sasa ni miongoni mwa wateuzi.
Mfano wa hilo unaweza kuthibitishwa na miaka ya hivi karibuni ambapo nchi nyingi zilizoandaa mashindano ya CAF ni zile ambazo zimekuwa na wajumbe wa kamati ya utendaji ya shirikisho hilo.
Fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) zilizopita zilifanyika Ivory Coast ambayo ndio anatoka mjumbe wa kamati ya utendaji ya CAF, Idriss Diallo wakati za wanawake (Wafcon) zilifanyika Morocco anakotoka mjumbe wa kamati ya utendaji, Faouz Lekjaa.

Kujiuzulu kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa CAF, Augustin Senghor kunatoa uwezekano kwa Karia kuteuliwa na Rais wa CAF, Patrice Motsepe kushika nafasi hiyo.
Lakini kama asiposhika hiyo, Karia anaweza kushika nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais au ya tatu kwa vile wanaoshika nafasi hizo kwa sasa, Ahmed Yahya wa Mauritania na Souleimane Waberi wa Djibouti watajiuzulu kwa vile wameshinda nafasi za ujumbe wa baraza la Fifa.
Karia pia ana uhakika wa kuvuna kiasi cha Dola 60,000 (Sh160 milioni) kwa mwaka kutoka CAF, kiasi ambacho kila mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo anapata kwa mujibu wa mwongozo wa malipo ambao limeuweka.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Karia alisema: “Namshukuru Mwenyezi Mungu, lakini niseme hongera sote, hongera pia kwa Watanzania, hongera watu wa Cecafa lakini na wale wenzangu wote walionisapoti kule upande wa CAF. Kwa hapa nyumbani niwashukuru Watanzania, nimshukuru waziri wetu na wasaidizi wake kwa niaba ya serikali kwa sapoti ambayo wamenipa.
“Lakini nishukuru kwamba tumepata nafasi hii, jambo kubwa nazungumza kwamba basi tusisherehekee sana twende tukafanye kazi tuhakikishe kwamba mpira wetu ulipofika tuhakikishe unaenda mbele zaidi.
“Nitakuwepo mimi katika vikao vya juu vya mpira. Nilikuwa naingia kama rais wa Cecafa, lakini nilikuwa ni mwalikwa lakini sasa naingia kama sio mwalika ila kama mjumbe kamili. “Ni jambo la faraja kwamba nimekuwa Mtanzania wa tatu kutumikia nafasi hii mmojawapo akiwa mzee wetu Said El Maamry (marehemu) ambaye alitumikia miaka mingi sana hadi akawa mjumbe wa heshima wa kamati ya utendaji lakini pia alikuwepo mzee wetu Tenga naye alifanya kwa miaka nane.”
Karia aliongeza kwa kusema: “Kwa hiyo ni nafasi hadhimu sana kwamba nimeipata nashukuru. Kitu kikubwa ni kuhakikisha kwamba kwa kukwa kwenye nafasi ile nastahili kuwepo pale kwamba tufanye vizuri kwa nchi yetu ili tuweze kuonyesha kwamba hatukupata nafasi hii kwa bahati lakini tumestahili kuipata.”