Dodoma. Serikali imelalamikiwa kutowashirikisha wakulima kwenye maandalizi ya bajeti zake kuanzia ngazi ya chini na badala yake wanapeleka maendeleo kwa maagizo.
Wawakilishi wa wakulima kutoka Wilaya za Chamwino (Dodoma) na Halmashauri ya Singida wametoa kauli hiyo leo Jumamosi Machi 15, 2025 wakati wa mafunzo ya ushirikishwaji wa maandalizi ya bajeti na hasa zinazogusa sekta ya kilimo.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Shirika la Action Aid kwenye mradi wa Trasnformative Impact Fund (TIF), unaolenga kuwajengea uwezo wa kuhoji mpango mzima wa bajeti kuanzia ngazi ya chini na usimamizi wa miradi kwa fedha zinazotolewa na Serikali.
Mkulima Sendeu Mjelwa wa kijiji cha Msanga Wilaya ya Chamwino, amesema hakuna bajeti shiriki bali zinazopelekwa ni maagizo kutoka ngazi ya juu na ndiyo maana utekelezaji wake umekuwa na changamoto hasa miradi mikubwa inayojengwa.
Sendeu amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wa vijijini hasa wakulima wakihoji namna gani wanashushiwa bajeti kutoka mamlaka za juu, bila ya kujua nani aliamua kujenga mradi au kutoa kiasi cha fedha kwa ajili ya kitu chochote kwenye kijiji ikiwa hakuna ushirikishwaji.
“Hasa sisi vijana tumekuwa waathirika kwenye mambo hatujui wa kumuuliza, huko vijiji viongozi hawana majibu ni lini na namna gani mchakato wa bajeti huwa unafanyika badala yake tunaona miradi mikubwa inajengwa wakati mwingine hata ile ambayo si kipaumbele chetu,” amesema Sendeu.
Agripina Ndahani amesema tatizo kubwa linalowaumiza wananchi ni uelewa hasi kuhusu masuala ya bajeti, kwani wengi wanaamini chombo pekee kinachopanga bajeti ni Serikali na ndiyo msimamizi.
Agripina amependekeza Serikali kutumia muda mwingi kutoa elimu kuhusu bajeti i na jinsi inavyoanza mchakato wake akisisitiza wenyeviti wa vijiji na vitongoji wawe wa kwanza kuipokea elimu hiyo.
Ofisa Kilimo na Mifugo kutoka Halmashauri ya Singida, Adam Sungita amesema ushiriki wa wananchi katika bajeti ni mkubwa na mara nyingi huanzia ngazi ya chini kwa wananchi wenyewe.
Sungita amesema ushiriki wa kuandaa bajeti siyo lazima ujikite kwenye pesa bali wananchi wanaweza kukaa na kuibua mradi au shughuli nyingine.