Hai. Wanawake wawili wanaodhaniwa kuwa ni washirikina wamekutwa wakiwa watupu (bila nguo) alfajiri ya leo Machi 15, 2025, katika madhabahu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Jimbo la Hai, Usharika wa Nkwarungo, Machame Kaskazini, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
Tukio hilo limezua taharuki kubwa wilayani hapa, ambapo wanawake hao walikamatwa na kuzungukwa na wananchi, baada ya kuhojiwa walidai kuwa walitumwa kwenda kuchukua ulimi wa mwanamke mmoja aliyezikwa hivi karibuni katika makaburi ya usharika huo.
Watuhumiwa wa ushirikina waliokamatwa madhabahuni katika Kanisa la KKKT Usharika wa Nkwarungo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wakiwa chini ya ulinzi.
Akizungumza eneo la tukio, Msaidizi wa Mkuu wa Kituo cha Polisi Bomang’ombe, (ASP) Daudi Kimashi, amethibitisha kuwakamata wanawake hao na kusema kuwa wanashikiliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
“Tukishindwa kwa njia za kibinadamu tutawapeleka hata kwenye maombi, uwepo wao hapa ni kosa kisheria, kwa hiyo tutawauliza wametokeaje hapa,” amesema Kimashi.
Akizungumza Mwinjilisti wa Usharika wa Nkwarungo, Jeremiah Nkya, amesema wanawake hao walinaswa na walinzi wa usharika huo wakiwa na mabunda ya vitu visivyoeleweka, ambavyo walinzi waliamua kuvichoma.

“Tulipofika, tulimwona bibi mmoja akiwa na mwingine wa makamu asiyeongea. Walikuwa wamevaa mahirizi kuanzia shingoni hadi kiunoni. Walinzi waliamua kuvichoma,” amesema Nkya.
Ameeleza kuwa baada ya taarifa za tukio kusambaa, waumini na wakazi wa eneo hilo walianza kukusanyika kwa hasira wakitaka kuwachoma moto, lakini hatua za haraka zilichukuliwa kwa kuwaita polisi ili kuwaokoa.
Naye, mzee wa Usharika wa Nkwarungo, Nelson Muro, amesema mmoja wa watuhumiwa hao alidai kuwa walitumwa kuchukua ulimi wa mwanamke mwenye umri wa takriban miaka 40, aliyefariki hivi karibuni na kuzikwa katika makaburi ya usharika huo.

Gari la Polisi likiwachukuwa watuhumiwa wa uchawi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Nkwarungo wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.
“Walivyokamatwa, walisema waliletwa na mtu fulani wanayemuita ‘Warindoo’ ili watekeleze kazi hiyo. Hata hivyo, walinzi waliwahisi mapema na kuwakamata kabla ya kufanikisha madhumuni yao,” amesema Muro.
Ameongeza kuwa mtuhumiwa mmoja alikuwa haongei kabisa, huku mwingine akizungumza kwa kilugha kiasi cha kutofahamika vizuri.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Foo, Trael Mboya, amesema kuwa alipofika eneo la tukio alikuta wanawake hao wakiwa wamewekwa chini na walikuwa tayari wamepewa mavazi ya kufunika miili yao kwa kuwa walikuwa utupu kabisa.
“Tulielezwa kuwa walikuwa hawajavaa nguo za ndani, isipokuwa mahirizi na mavazi yaliyochafuka. Kwa mujibu wa taratibu, tulihakikisha wanahifadhiwa kwa heshima kabla ya polisi kuwachukua,” amesema Mboya.
Hata hivyo polisi wamesema wataendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli wa madai hayo na hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa sheria.
Endelea kufuatilia Mwananchi digital kwa taarifa zaidi.