Tunduma. Wananchi wa Mji wa Tunduma wamewasilisha kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), kero tatu zinazowakabili zikiwamo za uhaba wa maji na bodaboda kunyanyaswa na Polisi.
Changamoto nyingine ni msongamano wa malori kwenye barabara kutoka Mbeya hadi Tunduma.
Wananchi wamesema ili CCM kijihakikishie ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 lazima zitatuliwe.
Kero hizo zimebainishwa mjini humo, mkoani Songwe leo Machi 15, 2025 kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM- Bara, Stephen Wasira. Umefanyika Kata ya Majengo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
“Katika mji wetu changamoto ya maji ni kubwa, kwa muda mrefu tumekuwa tukilalamika lakini hatupati majibu, viongozi wamekaa kimya. Hatuna maji tunaweza kupata magonjwa ya mlipuko, tunaomba kiongozi tusaidie kulibeba hili,” amesema Lilian Mwakareli.
Hoja ya ukosefu wa maji pia ilizungumzwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo kwenye mkutano wa ndani uliofanyika Mbozi jana Machi 14, akisema Serikali ipo kwenye mchakato wa kusogeza huduma hiyo.
“Upatikanaji wa maji katika mkoa wetu kwa vijijini ni asilimia 74 lakini katika miji yetu ukiwemo Tunduma ni asilimia 50. Ni changamoto kubwa ambayo tunaishughulikia tuweze kuitatua,” alisema Chongolo.
Wasira akizungumzia changamoto hiyo amesema kuanzia Machi 20, 2025 Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso watakwenda mkoani humo kusaini mradi wa maji zikiwa ni juhudi za kutatua kero hiyo.
“Ni kweli changamoto hii ni ya muda mrefu hata mwenyewe nilipokuwa Waziri wa Maji mwaka 2006 nilikuja hapa nilipata kilio hiki, katika kipindi cha miezi 10 niliyokaa katika nafasi hii tulichimba visima viwili sasa kulingana na wingi wa watu kwa kweli kutegemea maji kutoka visima viwili havitoshi,” amesema.
Amesema mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji ukisainiwa, CCM kitasimamia kuhakikisha changamoto hiyo inapatiwa majibu.
Waendesha bodaboda mjini humo wamesema wamekuwa wakinyanyaswa na Polisi kwa kukamatwa mara kwa mara wanapofanya shughuli zao na wakati mwingine hubambikiwa makosa.
“Tunashukuru kiongozi umekuja vurugu za Polisi na bodaboda ni kama paka na panya, hatufanyi kazi zetu kwa uhuru muda wote tunakamatwa hatujui tatizo nini na wanashindwa kujua tunatafuta riziki,” amesema Yasin Mwakasasa.
Akijibu changamoto hiyo, Wasira alianza kwa kuwataka waendesha bodaboda kuheshimu sheria za usalama barabarani kulinda afya zao, na kuwataka Polisi kuacha kuwanyanyasa.
“Polisi punguzeni makosa msiwakamate mara kwa mara na wenzetu wanatafuta riziki lakini na ninyi bodaboda zingatieni sheria ili kazi zenu zifanyike kwa amani,” amesema.
Amesema chama hicho kinatokana na watu lazima kisikilize kero zinazowasumbua na kuzipatia majibu.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Songwe, Aden Mwakiondo amesema msongamano wa magari katika barabara inayotoka Mbeya hadi Tunduma ni pasua kichwa.
Licha ya barabara hiyo kuanza kujengwa kuanzia Mbeya kwa njia nne, ametoa ombi kwa kiongozi huyo kuishinikiza Serikali kutafuta mkandarasi mwingine aanzie mji huo ili wakutane katikati.
“Kama huku Tunduma wataanza kujenga tutakutana katikati tunaweza kukabili hii changamoto kwa haraka tofauti na ilivyo sasa hali ni ngumu kutoka hapa kwenda Mbeya,” amesema.
Wasira akizungumzia upanuzi wa barabara hiyo amesema atakwenda kumshauri Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ili kuliangalia hilo.
Awali, Wasira alikagua ujenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa huo inayojengwa kwa gharama ya Sh16.1 bilioni, pia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Kanda ya Juu Kusini iliyoanza kujengwa. Ujenzi utakaogharimu Sh4 bilioni.