Simiyu. Chama cha African Democratic Alliance Party (Ada-Tadea) kitatoa fomu bure kwa wagombea wanawake na wenye ulemavu watakaojitokeza kuwania nafas za urais, ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu ujao.
Katibu mkuu wa chama hicho, Salehe Msumari amesema hayo leo Jumapili Machi 16,2025 mjini Maswa wakati akiwapokea wanachama wapya 100 waliojiunga na chama hicho kutoka vyama mbalimbali vya siasa hapa nchini.
Katibu Mkuu ADA TADEA,Salehe Msumari akizungumza na viongozi na wanachama wa chama hizo mkoa wa Simiyu wilayani Maswa,(hawapo pichani)Picha na Samwel Mwanga
Akizungumza na viongozi na wanachama wa chama hicho wa Mkoa wa Simiyu, amesema chama hicho kimefikia uamuzi huo ili kuyawezesha makundi hayo kushiriki uchaguzi huo, unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
Amesema makundi hayo katika jamii wengi wao hawana uwezo wa kugharamia shughuli za uchaguzi ikiwamo kulipia ada za fomu kwa ajili ya kugombea uongozi.
“Mimi katibu mkuu nimekuja na tamko la chama chetu, kuna wengine wanaweza kusema kwa nini sijalitolea makao makuu na ikawa ni Maswa mkoani Simiyu, hii ni kwa sababu huku ndipo kuna mizizi ya Chama cha Ada-Tadea.
“Ada-Tadea tunatamka kuwa tutashiriki uchaguzi mkuu ujao na chama kimeamua na tumekubaliana wagombea wote wa nafasi ya urais, ubunge na udiwani ambao ni wanawake na walemavu kitawapa fomu bure na nitoe maagizo kwa viongozi wa wilaya na mikoa kuzingatia maelekezo hayo,” amesema.

Katibu Mkuu ADA TADEA,Salehe Msumari(kushoto)akimkabidhi kadi ya chama hicho,Samwel Kidima (kulia)mara ya kujiunga na chama hicho wilayani Maswa.Picha na Samwel Mwanga
Amesema chama hicho kinaingia kwenye uchaguzi huo kwa kauli mbiu ya E4C (Election for Change) kwa kuwa, ni lazima mabadiliko ya uchaguzi yafanyike ukiwa ndani ili uone upungufu na siyo kujitoa kwenye uchaguzi.
“Kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu ambao sisi tumetangaza tutashiriki tutatoa elimu ya kauli mbiu yetu kwa wanachama wetu wote ili waifahamu maana huwezi kutaka mabadiliko bila kushiriki uchaguzi,”amesema.
Mwenyekiti wa Ada-Tadea Mkoa wa Simiyu, Luhende Mipawa amesema uamuzi huo utawezesha wanawake na wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao.
“Kutokana fursa hii iliyotolewa na chama chetu ni matarajio yangu makubwa kuwa tutapata wagombea wengi katika uchaguzi mkuu,” amesema.
Mmoja wa wanachama wa Ada-Tadea wilayani Maswa, Mariam John amesema uamuzi huo utaongeza chachu kwa wanawake na watu wenye ulemavu, hivyo kuwataka kujitokeza kwa wingi wakati ukifika.
“Uamuzi huu ni chachu kwetu sisi wanawake na wenye ulemavu maana chama chetu kimeona umuhimu wa sisi kugombea, hivyo niwaombe hasa wanawake tujitokeze muda ukifika ili tuweze kugombea nafasi mbalimbali tuingie kwenye vyombo vya maamuzi,’ amesema.
Naye Jane Titus ambaye ni mwanachama wa chama hicho amesema chama hicho ndicho pekee chenye kuthamini makundi mbalimbali.
“Ni busara imetumika kufikia uamuzi huo, niwapongeze viongozi wangu kwa kutupatia fursa sisi wanawake na mimi nitajitokeza kuchukua fomu ili niweze kugombea udiwani katika Kata ya Malampaka Wilaya ya Maswa, muda kipenga kitakapopulizwa,” amesema.