Ahoua bado rekodi mbili | Mwanaspoti

MABAO mawili aliyoyafunga kiungo nyota mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua, juzi katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Dodoma Jiji, unamfanya kunyatia rekodi mbili kwenye michezo minane iliyobaki ya Ligi Kuu Bara.

Nyota huyo aliyejiunga na Simba Julai 3, 2024 akitokea Stella Club d’Adjame ya kwao Ivory Coast, amebakisha bao moja tu na asisti nne, ili kuivunja rekodi yake ya msimu uliopita iliyomfanya kuibuka kidedea wa mchezaji bora (MVP) Ligi Kuu ya Ivory Coast.

Msimu huu pekee tayari nyota huyo amefunga mabao 12 akiwa ndiye kinara na kuchangia sita ‘Assist’, huku msimu uliopita wakati akiwa na kikosi cha Stella Club d’Adjame alifunga mabao 12 na kusaidia upatikanaji wa mengine tisa.

Ujio wa Ahoua ulimfanya kufikisha idadi ya nyota watatu waliotoka Ivory Coast na kuibuka wachezaji bora wa msimu (MVP), baada ya Stephane Aziz KI msimu wa 2022-2023 na Pacome Zouzoua msimu wa 2023-2024, walioko Yanga wakitokea ASEC Mimosas.

Licha ya wengi kutokuwa na imani mwanzoni na Ahoua wakati alipotua nchini, hasa baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kipenzi cha timu hiyo, Clatous Chota Chama ‘Triple C’ aliyejiunga na Yanga, ila taratibu amekuwa msaada mkubwa kikosini humo.

Ahoua aliletwa Simba ili kuwa mbadala wa Chama aliyefanya makubwa na kikosi hicho cha Msimbazi na kujizoelea umaarufu mkubwa, huku mashabiki wa kikosi hicho wakiendelea kufurahia matunda yake ikiwa ndio msimu wake wa kwanza hapa nchini.

Msimu huu Ahoua amechangia mabao 18 ya Ligi Kuu Bara ndani ya kikosi cha Simba kati ya 52 yaliyofungwa na timu nzima ambayo kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi 57, nyuma ya wapinzani wao Yanga wenye 58.

Nyota huyo aliyezitumikia timu za LYS Sassandra na Sewe Sports kisha kutua Stella zote za kwao Ivory Coast, ana uwezo wa kufunga na kutengeneza mabao, huku akicheza nyuma ya mshambuliaji na wakati mwingine akitokea winga ya kulia au kushoto.

Tangu atue kikosi cha Msimbazi, tayari ameivunja rekodi ya mabao ya Chama aliyoiweka msimu wa kwanza wa 2018-2019, akitokea Lusaka Dynamos FC ya kwao Zambia, alipofunga mabao saba na kuchangia mengine tisa katika ligi.

Kwa maana hiyo Ahoua amebakisha asisti tatu tu kuifikia rekodi ya Chama ya msimu wake wa kwanza japo ikiwa atafikisha nne ataivuka, ingawa anatakiwa kuendelea kuonyesha kiwango bora kama alivyofanya ‘Mwamba wa Lusaka’ akiichezea Msimbazi.

Ahoua amechangia Simba kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu ikiwa ni kwa mara ya sita kwenye misimu yake saba iliyopita ya michuano ya CAF tangu msimu wa 2018-2019, amefunga mabao mawili na kuchangia pia mengine mawili.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids baada ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji alisema wachezaji wote walitimiza vyema majukumu yao hivyo, anatoa pongezi kwao kutokana na ushirikiano waliouonyesha uwanjani, kwani hiyo ndio silaha ya kuishinda vita.

“Kila mmoja alicheza vizuri ndiyo maana tumepata ushindi mzuri ambao sasa unatupa nafasi ya kujipanga vyema na mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ugenini dhidi ya Al Masry, niwape pongezi kwa kiwango bora walichokionyesha uwanjani,” alisema Fadlu.

Related Posts