WAKATI Kombe la Shirikisho likiwa hatua ya robo fainali, ni mastaa watatu tu wa timu za Ligi ya Championship walioweka heshima kwa kufunga hat trick katika michuano hiyo wakiwapiga bao hadi nyota wa Ligi Kuu Bara, iliyoingiza timu nyingi hatua ya 16 Bora.
Nyota wa kwanza kufunga ‘Hat-Trick’ ni Kassim Shaibu ‘Mayele’ wa TMA FC, wakati timu hiyo iliposhinda mabao 5-1, dhidi ya Mabingwa wa Mkoa wa Tanga Leopards FC hatua ya 64 bora, mechi iliyopigwa Sheikh Amri Abeid Arusha Desemba 5, 2024.
Mwingine ni Elias Maguri anayeichezea kwa sasa Geita Gold aliyeifungia Biashara United katika ushindi wa kikosi hicho wa 5-0, dhidi ya TRA FC ya Kilimanjaro hatua ya 64 bora, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Karume Musoma, Desemba 7, 2024.
Nyota mwingine ni Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar aliyefunga pia wakati timu hiyo ikishinda mabao 5-3, dhidi ya Mabingwa wa Mkoa wa Singida, Town Stars katika hatua ya 32 bora, mechi ikipigwa Uwanja wa Manungu Complex Morogoro Machi 3, 2025.
Rekodi hiyo imeivuka ile ya msimu uliopita kwani ni nyota wawili tu wa Ligi ya Championship waliofunga ‘hat-trick’ kati ya saba zilizofungwa, ambao ni Pascas Wagana anayeichezea Biashara United ya Mara na Shaban Seif wa Mbuni FC ya Arusha.