Kituo cha sayansi kwa vitendo kujengwa Dodoma, kuzalisha wanasayansi

Dar es Salaam. Katika kuwazalisha wataalamu wa sayansi, teknolojia na ubunifu kupitia mafunzo kwa vitendo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeitaka Taasisi ya Projekt Inspire kujenga kituo kikubwa cha ubunifu (Stem Park) jijini Dodoma.

Kituo hicho cha kisasa cha Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati kitatumika kufundishia wanafunzi kwa vitendo ili wapate ujuzi pamoja na maarifa watakayotumia katika bunifu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumamosi Machi 15, 2025 katika miaka kumi ya taasisi hiyo, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kituo hicho kitatumika kama shamba darasa kwa viongozi wa kiserikali na wadau kabla ya kujengwa maeneo mengine nchini.

“Kwa sababu Dodoma ni katikati ya nchi Bunge linakutana pale, wakuu wa wilaya wakuu wa mikoa na wabunge mara nyingi wanakutana jijini hapo, hivyo nimewaambia hii taasisi wajenge kubwa zaidi waone inavyofanya kazi, iwahimize waweze kujenga maeneo mengine nchini,” amesema.

 Profesa Mkenda ameiagiza Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kushirikiana na taasisi hiyo kwa makubaliano ili nayo ichangie na katika bajeti ya mwaka ujao zitengwe hela kuwasaidia waendelee.

“Mataifa yote makubwa duniani msingi wake unatokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, mfano sasa hivi watu wanapigana vita kwa kutumia drones, hata vijana wetu hawa wanaweza kutengeneza drones, bado tunataka wanasayansi wengi,” amesema. 

Amesema kituo hicho kitakuwa kikubwa Afrika Mashariki kutokana na ukubwa wa eneo lake la eka kumi  na baadaye halmashauri zitatenga maeneo na kununua vifaa kwa ajili ya wanafunzi kujifunzia.

Waziri Mkenda amesema lengo ni kuongeza kujiamini kwa vijana na kujifunza kwa vitendo yale wanayojifunza darasani.

“Tumeunda kamati mbalimbali sasa hivi za kuunganisha vyuo na maeneo ya kazi. Kila chuo kikuu sasa hivi kinatakiwa kuwa na muunganiko na taasisi za benki, viwanda na wazalishaji ili anayesoma ajifunze kwa vitendo,” amebainisha. 

Mwanzilishi wa Projekt Inspire,  Dk Lwidiko Mhamilawa amesema kwa dunia ilipo sasa watoto wanapaswa kujifunza kwa vitendo tangu awali ili wapate maarifa kama taasisi hiyo inavyofanya kwa miaka kumi sasa.

“Kwa sasa kuna vituo Tanga na hapa Dar es Salaam tunawafundisha kwa vitendo kwa kutumia vifaa, mfano kuchanganya kemikali na vifaa vya kimaabara ili watoto waone tija ya elimu kulingana na yale wanayojifunza darasani,” amesema Dk Mhamilawa.

Innocent Richard, mmoja ya aliyejifunza kwa vitendo kwenye taasisi hiyo ambaye kwa sasa anaiwakilisha nchi kimataifa ameshauri vijana kusoma ya sayansi kwasababu sasa kuna mafunzo kwa vitendo.

 “Nilipata nafasi ya kushiriki katika programu ya kimataifa huko London, kutoka hapo nilipata udhamini wa Uhandisi wa Umeme.  Kwa hiyo natoa wito kwa vijana wengine kujihusisha na masomo ya STEM kwa sababu ya fursa nyingi zilizopo,” amesema.

Related Posts