Mke adaiwa kuuawa kisa Sh50,000

Dar es Salaam. Mkazi wa Kibonde Maji B, wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam Paulina Mathias (40) anadaiwa kuuawa na aliyekuwa mumewe kwa kuchomwa kisu tumboni baada ya kumnyima Sh50,000 kulipia kodi ya pango.

Tukio hilo limetokea Machi 10, 2025 eneo la Kibonde Maji alikokuwa amepanga mwanamke huyo.

Leo Jumapili, Machi 16, 2025 Mwananchi limemtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro kuhusu tukio hilo, ameelekeza taarifa hiyo ijibiwe na Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Temeke kwa kuwa yeye yupo safarini.

“Mtafute Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke atazungumzia, mimi nipo safarini,” amesema Muliro kwa simu.

Alipotafutwa Kamanda Kipolisi Temeke, Kungu Malulu amesema taarifa hiyo itazungumziwa na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Happy Athuman, mdogo wa marehemu (Paulina) akizungumza na Mwananchi leo kuhusu mgogoro ulioanza Februari mwaka huu, amedai kuwa, kabla ya mauaji kutokea, mwanamume alimuomba mkewe fedha zake za kikoba alipie kodi na alimpatiwa kwa sharti la kurejesha.

“Dada alipokea Sh50,000 ya kikoba, mwanamume akamfuata akamwambia ampe fedha hiyo alipe kodi ya nyumba kwasababu anadaiwa Sh50,000, dada akamwambia kama unataka basi nakukopesha kwasababu nimeandaa fedha hii kwa ajili ya mwezi Ramadhani (wakati huo ilikuwa Februari),” amedai Happy.

Baada ya muda, Happy amedai kuwa dada yake alimpatia Sh50,000 mwanamume huyo kwa ajili ya kulipa kodi lakini, alitoweka na fedha hizo na baada ya muda baba mwenye nyumba alifuata kodi yake.

Amesema kwa kuwa shemeji yake tayari alishapatiwa fedha hizo, Happy alisema Paulina alimpigia simu kumwambia tayari mwenye nyumba amefika akihitaji kulipwa deni lake.

Amedai kuwa, mwanamume huyo alirudi na Sh48,000 na kumrejeshea Paulina akimwambia aongeze ifike Sh50,000 ili itoshe kulipa kodi, lakini Paulina alihoji kwa nini fedha hiyo ni pungufu (wakati awali alimpa Sh50,000).

“Baada ya dada kuhoji upungufu wa hizo fedha, mwanamume alimwambia aongezee, dada akamwambia hatompatia tena hizo fedha, mwanamume akamwambia kama hutotoa narudi kwetu mikoroshini utajuana na mwenye nyumba,” amedai.

Happy amedai kuwa, shemeji yake alianza kukusanya kila kitu kilicho chake pamoja na nguo na viatu alivyowahi kumnunulia dada yake na kuondoka nazo.

Amedai kuwa, baada ya shemeji anaondoka, alimwita kusuluhisha ugomvi huo lakini alisema siku zote amekuwa akimpatia Paulina fedha za kikoba lakini hataki kulipa kodi.

Baada ya wawili hao kutengana, Happy alidai dada yake alipata kibarua eneo la Feri Kivukoni Machi mwaka huu na baada ya mwanamume kusikia Paulina waliyetengena amepata kazi, alianza kumfuatilia.

“Mwanamume alimfata usiku mkewe ampe mtoto wake ambaye sasa anasoma darasa la tatu ampeleke kwa ndugu zake Dodoma, wakati dada anajiandaa kwenda kazini mumewe aliingia bafuni na kuanza kumpiga ngumi hadi kumpasua uso,” amedai.

Kufuatia tukio lile alidai walimchukua dada yao na kuondoka naye hadi nyumbani kwenda kumuuguza na alipopona aliendelea na shughuli zake.

“Siku ya tatu ndio alikwenda kushitaki polisi Kituo cha Maturubali Mbagala, kule aliambiwa amechelewa alipaswa kufika kituoni tu baada ya kutendewa tukio lile akaulizwa kwanini alikaa hadi majeraha yamekauka,” amedai mdogo wa marehemu.

Happy amedai kuwa, siku mbili tu zikiwa zimepita tangu dada yake kwenda kulalamika polisi, aliyekuwa mumewe Machi 10 saa mbili usiku alifika alikokuwa akiishi Paulina na kuanza kumshambulia.

“Usiku mtoto wake ndiye alikuwepo wakati mwanamume akimshambulia, mtoto tulimpeleka polisi; baba yake aliingia ndani na kutoka nje na kumuita aliyekuwa mkewe waingie ndani, basi mwanamke alijua mwanamume anataka wasuluhishe baada ya muda mwanamume alianza kufoka.

“Dada alimuuliza ulichokifata ni nini hapa, baada ya swali hilo mwanamume alitoa kisu mfukoni na kuanza kumchoma choma tumboni na kisu kingine alitoa kabatini na kumshindilia hadi kumtoa utumbo,”amedai.

Happy amedai kuwa, pamoja na mtuhumiwa kutumia kisu kumchoma dada yake tumboni walikuta majeraha ya viwembe mwilini kwa ndugu yake huyo wakati wasiusafisha mwili kwa maziko.

Alichokisema mwenyekiti wa mtaa

Mwenyekiti wa Kibonde Maji, Chawata Luhoga akizungumza na Mwananchi amedai kuwa, haikuwa mara ya kwanza kwa wanandoa hao kupigana kwani mwanamume aliwahi kumpiga mwanamke hadi kumuumiza jicho.

Amedai kuwa, siku yalipotokea mauaji ya mwanamke huyo, kulianza ugomvi na mjumbe alikwenda kusuluhisha na kumuonya mwanamume huyo.

“Baada ya muda baba wa mwanamke alinipigia simu mwanawe anapigwa na mumewe sana, niliwapigia simu sungusungu tuwahi eneo la tukio na tulipofika mwanamume tayari ameshaondoka na tulipofungua mlango kutoa msaada kwa mwanamke, tayari alishafariki,”alidai.

Mwenyekiti amedai kuwa, baada ya hali ile walianza kumsaka mwanamume huyo kwa kushirikiana na jeshi la polisi bila mafanikio yeyote na hadi sasa bado anatafutwa.

Related Posts