Mwanafunzi wa darasa la kwanza auawa kwa kuchinjwa

Rombo. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia mwanamume (26), mkazi wa kijiji cha Kirwa, kata ya Katangara Mrere, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kumuua na kumtenganisha kichwa na kiwiliwili mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mahaheni.

Mwanafunzi huyo Rosemary Mathius (6), mkazi wa Kijiji cha Mrere anadaiwa kuuliwa na mwanamume (jina limehifadhiwa, wakati alipokuwa akicheza na wenzake nyumbani kwa wazazi wa mtuhumiwa baada ya mama yake kumuombea hifadhi ya muda kwa jirani ili aende kwenye mazishi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema tukio hilo limetokea jana Jumamosi Machi 15, 2025 wakati mtoto huyo akiwa anacheza na wenzake.

Kamanda Maigwa amesema wanamshikilia mtuhumiwa huyo katika kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi.

” Machi 15, 2025, majira ya saa 9:00 alasiri huko Kijiji cha Mrere, Kata ya Katangara Mrere, Rosemary Mathius (Careen), mwanafunzi wa Mahaheni aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya shingoni,” amesema Kamanda Maigwa.

“Mwili wa marehemu umekutwa nyumbani kwa mtuhumiwa kwa nje, kichwa kikiwa pembezoni mwa mwili huo,” ameeleza Kamanda Maigwa.

Kamanda Maigwa amesema chanzo cha tukio hilo bado hakijafahamika na mtuhumiwa anashikiliwa kwa mahojiano na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Huruma, wilayani Rombo.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mrere, Salvatory Urassa amedai kuwa, mama mzazi wa Careen aliwaombea mtoto huyo aliyeuawa na dada yake kwa jirani ili akazike, ndipo mama wa mtuhumiwa alipomkubalia.

Amesema wakati watoto hao wakiwa nyumbani kwa wazazi wa mtuhumiwa wakicheza, mtuhumiwa huyo alifika na kumuuliza mama yake kwamba, baba yake yuko wapi na mama alimjibu kaenda kwenye mazishi.

“Wakati huo, mdogo wa mtuhumiwa alikuwa anawachomea mahindi ya kula hawa watoto na mama mzazi …, wakati (mama) anamjibu ameenda kwenye mazishi, ndipo papo hapo akamshambulia huyo mtoto,” amesema Urassa.

Amesema baada ya kuanza kumshambulia, dada yake akakimbia na kuanza kupiga ukunga ndio watu walipoenda eneo la tukio na walipofika tayari walikuta mtuhumiwa ameshatekeleza mauaji hayo.

“Wakati watu wanafika eneo la tukio mtuhumiwa alikimbia na ndipo walipomkimbiza na kwenda kumkamatia eneo linaitwa Mrao ambalo lipo nje ya kijiji hicho,”amesema mwenyekiti huyo.

Amesema tukio hilo limeleta simanzi kubwa kijijini hapo.

Msaidizi wa masuala ya kisheria katika kijiji hicho, Mathius Kavishe amesema matukio kama hayo yamekuwa yakishamiri vijijini, huku akalaani tukio hilo akisema mtoto huyo hakupaswa kuuawa kikatili namna hiyo.

Related Posts