Ndoa ina pandashuka nyingi, kikiwemo kipindi cha wenza kukosa kuchangamkiana kama siku za mwanzo za uhusiano wao.
Hii inafanyika kwa wanaochukulia ndoa kama kitu cha kawaida.Wapo wanaohisi kwamba baada ya kufunga pingu za maisha, wana haki ya kumiliki wenza wao.
Hisia hizi ziko mbali sana na ukweli wa mambo kwa kuwa zinachozaa ni watu kuchoshwa na uhusiano wao.
Ndoa ni kama mti, unapopandwa, unafaa kupapaliwa, kuwekwa mbolea na kunyunyuziwa maji kila wakati ili uweze kunawiri na kuchanua maua yenye harufu ya kuvutia.
“Usipotunzwa vyema, mti hauwezi kuchanua maua yenye afya na hauwezi kuzaa matunda mema ya kufurahia. Ndivyo ilivyo kwa ndoa, lazima itunzwe kila wakati ili iweze kunawiri,” anasema mtaalamu wa masuala ya ndoa Jane Muthoni.
Anasema, ndoa ikikosa kupaliliwa na wahusika huwa inachokesha. Hivyo inahitaji wenza kuwa wabunifu sana kwa kila hali.
Mume asiwe mtu katili na dhalimu kwa mkewe. Wake ni viumbe maalumu,wanachoshwa na tabia ya kugombezwa na kulaumiwa kila wakati na wenza wao.
“Watu wanaojua kupalilia ndoa huwa hawagombezi wenza wao, huwa wanawapa mwelekeo. Hakuna asiyechoshwa na mwenza anayemtusi na kumlaumu kwa kila kitu kibaya kinachotendeka katika uhusiano wao,” anaeleza Muthoni.
Lakini mtu hawezi kuchoshwa na mwenza anayemnyenyekea, kumjali na kumkosoa kwa hekima akidumisha heshima kwake. Kuepuka kuchokana kunahitaji mke anayejua kumtunza na kumhudumia mumewe.
Wanaume hupagawishwa na mambo madogo sana kama vile kumvua koti na kumkumbatia akitoka kazini.
Mwanamume hawezi kuchoshwa na mke anayemuomba ushauri na ruhusa ya kutoka nyumbani kwenda kokote hata kama ni kazini au mkutanoni.
Ajabu ni kuwa wanawake wengi huwa wanaacha mambo kama hayo wakidai wamemea mizizi katika ndoa na wao wana hisa sawa na waume wao katika ndoa.
Wenza wanaoheshimiana hawawezi kutuhumiana na kuchokana. Wanajua kuwa tuhuma ni sumu kwa mapenzi na huzaa vurugu.
Kuna kinadada ambao wakiingia katika ndoa huwa wanageuka kuwa simba dume, kiasi cha kuwapokonya waume zao nafasi yao katika ndoa.
Vile vile, kuna wanaume wanaogeuka kuwa katili katika ndoa zao ilhali walikuwa wenye mioyo safi na maneno matamu walipokuwa wakitafuta wachumba wa kuoa.
Watu wanaofanya hivi, wanajiweka katika hatari ya kuchokwa na wenza wao.
Wanaume wengi, na kuna ushahidi wa kutosha, wamegeukia ulevi wa kupindukia kutokana na mfadhaiko wanaosababishiwa na wake wao.
Ili kuepuka kuchokana, wenza wanafaa kuomba pamoja, kuepuka kurushiana lawama au kulazimisha mambo.
“Lawama zinachosha, hazijengi na mara nyingi chanzo chake huwa ni mambo yanayoweza kutatuliwa kila mmoja akitambua nafasi yake katika uhusiano wa kimapenzi na kujitahidi kuuboresha zaidi,” anafafanua Muthoni.
Ni vyema kwa mume, kutambua kuwa mkeo ni mpenzi; si mke tu, na hivyo ni muhimu kuonyesha upendo wako kwake. Mpende kwa moyo wako wote. Mwanamume yeyote anayemjali mkewe anafaa kufahamu hili na kulikumbatia.
Vile vile, mkeo ni rafiki yako, mpe tumaini, mlee, mfurahie, omboleza naye, msherehekee na zaidi cheka naye. Mtendee kama mtoto mchanga, mlishe na umthamini. Mruhusu alale kifuani mwako, mbembeleze na umruhusu ajisikie vizuri na wewe.
Utakuwa unakosea kwa kumtenga kwa visingizio vingi vya hapa na pale. Kaa na mkeo uliko ikiwezekana, mlale kwenye kitanda kimoja, mfanye ahisi raha ya kuwa mwenza wako.
Kumbuka kuwa mkeo ni mwenza wako wa roho, mpe akili yako na moyo wako, usimfiche chochote. Mtambue kama malkia wako.
Mke wako ni mshirika wako wa ngono; usione aibu kufanya naye mapenzi. Mvue nguo, jifurahishe, hakikisha naye anaifurahia. Usiwe mchoyo, mtazame usoni, na uangalie ikiwa anaifurahia.
Usilale na mwanamke mwingine yeyote, ni dhambi.Mume anapaswa kumheshimu mkewe kama malkia jinsi alivyo; ukifanya hivyo, atakutendea kama mfalme. Ikiwa wewe ni mfalme, zungumza naye kwa heshima.
Ndoa iliyojikita kenye msingi wa heshima haiyumbi.Kufanya hivi, mkeo anapaswa kuwa mwanamke wa pekee kwako, mwanamke nambari moja maishani mwako.
Kamwe usiruhusu mwanamke mwingine yeyote, mama yako, dada zako au wafanyakazi wenzako kuchukua nafasi yake katika maisha yako.Mfundishe mkeo kile unachotaka afanye.
Usimkasirikie; mwache aendelee kujifunza kwako, wewe ni mwalimu wake namba moja.Vilevile, wanawake wanastahili kufahamu kuwa hakuna mwanamume mgumu, ujinga ndio huleta ugumu.
Ukitaka mwanaume akupende, lazima uelewe ni nini kinamfanya awe mwanaume.Wanawake wengine wanatarajia wanaume wao kukubali ushauri wao wote na kufuata maagizo yao yote, hiyo haiwezekani!
Hawezi kukubali kila kitu. Yeye ndiye kichwa. Hauwezi kulazimisha mawazo yako kwake, unaweza kushauri tu, uamuzi wa mwisho upo mkononi mwake.Wanaume hutaka amani.
Ugomvi, kupiga kelele, matusi na kumlaani kunaweza kumkosesha utulivu.Wanaume wengine huchukia kurudi nyumbani mapema kwa sababu ya usumbufu wa wake wao.
Wanaume hukimbilia wanawake wanaowapa amani si kuwavunja vipande vipande kwa kelele na ubishi.Wanaume pia hupenda mlo bora.
Akikupa pesa za chakula, anataka mlo unaoakisi pesa hizo! Ongeza kile ulicho nacho, mpikie kama mfalme na atakwama kwako.Na usisahau kumsifu mume wako. Wanaume wanapenda kumiminiwa sifa na wake zao.
Makala haya yaliyoboreshwa awali yalichapishwa katika gazeti dada la Taifa Leo.