Odinga amkingia kifua Rais Ruto

Kenya. Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga amewajibu wakosoaji wa Serikali ya Rais William Ruto wanaotaka aondoke madarakani huku akisema wanataka atoke aende wapi.

Kauli ya Odinga inakuja zikiwa zimepita  siku chache tangu asaini makubaliano ya kufanya kazi na Rais Ruto nchini Kenya.

Makubaliano hayo kati ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Ruto na Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Odinga, yana lenga kukabiliana na changamoto zinazotishia kuleta mpasuko ndani ya taifa hilo.

Mkataba huo utaongeza uwajibikaji, kupambana na ufisadi, changamoto ya ajira na kuzuia upotevu wa rasilimali za Serikali ili kukuza ufanisi katika uendeshaji wa sekta za umma.

Akizungumza jana Jumamosi, Machi 15, 2025 kwenye mazishi ya rubani mstaafu, Kanali James Gitahi huko Maanzoni, Kaunti ya Machakos, Odinga amepuuza wito wa kumuondoa Rais na Serikali yake pamoja na wale wanaopinga ushirikiano wake na Rais Ruto.

Hata hivyo, katika mitandao ya kijamii baadhi ya Wakenya wamekuwa na kauli inayosema #RutoMustGo yaani Ruto lazima aondoke, huku Odinga akisisitiza kwamba, kumuondoa Rais Ruto au Serikali ya sasa hakutatatua changamoto zinazowakumba Wakenya.

Kutokana na kauli ya kiongozi huyo wa upinzani, Wakenya wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha na kumwondoa Rais Ruto kutaitumbukiza nchi katika msukosuko wa kisiasa usioisha na kusababisha matatizo zaidi.

“Gharama ya maisha ziko juu mno; watu wanateseka kwa sababu bei ya chakula iko juu, kodi ni kubwa sana na ufisadi umeongezeka. Ajenda ya vipengele kumi si usaliti kwa Wakenya,” amesema Odinga.

“Mnasema Ruto aende, aende halafu nini ifanyike? Gachagua alienda, sasa mnataka Ruto aende, Kindiki abaki pale, halafu naye pia aende aje mwingine…”amenukuliwa na Citizen Digital ya nchini humo.

Rigathi Gachagua alikuwa Naibu Rais wa Kenya aliyeng’olewa madarakani huku Profesa Kithure Kindiki alichaguliwa kuchukua nafasi yake. 

Kiongozi huyo wa ODM amewataka viongozi na wananchi kuepuka siasa zisizo na mwisho na kusubiri hadi 2027,

watakuwa na fursa ya kuchagua viongozi wa matakwa yao.

Amesisitizza kuwa, siasa za kila mara zinazoshuhudiwa kote nchini zinakwamisha maendeleo ya Serikali.

“…Hakuna haja, 2027 itafika, lakini shida za Wakenya lazima zitatuliwe sasa, si siku nyingine. Hatuwezi kuwa kwenye kampeni kwa miaka yote mitano nchi haiwezi kusonga mbele kwa sababu kelele ni nyingi sana, tumeifanya nchi kuwa kwenye hali ya kampeni kila wakati,” amesema Odinga.

Related Posts