Polisi Geita yachunguza kifo cha mchimbaji mdogo

Geita. Jeshi la Polisi mkoani Geita linachunguza kifo cha mchimbaji mdogo wa madini, Emmanuel Sitta (25), mkazi wa Nyakabale, anayedaiwa kuingia kinyemela kwenye mgodi wa dhahabu wa Geita na kupatikana akiwa na jeraha kichwani, kisha kupoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Manispaa ya Geita.

Taarifa ya maandishi iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, kwa waandishi wa habari leo Jumapili, Machi 16, 2025, imeeleza kuwa marehemu akiwa na wenzake watano, Machi 13, 2025, walikutwa ndani ya mgodi wakati eneo hilo lilipovamiwa na kundi la wahalifu waliovamia leseni ya mgodi kinyume na sheria.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kamanda ameeleza kuwa uchunguzi wa kifo hicho umeanza kwa kuwashirikisha wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi ili kubaini sababu na chanzo cha kifo hicho, ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa yeyote atakayebainika kuhusika.

 Ameeleza pia kuwa, kutokana na tukio hilo, watu wanne waliokuwa na marehemu kabla ya kifo hicho wanashikiliwa kwa mahojiano, huku majina yao yakihifadhiwa kwa sababu za uchunguzi.

Kamanda Jongo ameeleza kwenye taarifa yake kuwa Machi 13, saa 11 jioni, mgodi ulibaini uingiaji wa watu visivyo halali katika eneo la LIG10, na watu hao wanaodaiwa kuwa wahalifu walionekana wakiwa wameiba na kubeba mawe yenye dhahabu kwenye mifuko zaidi ya 20. Taarifa hiyo imeeleza kuwa ufuatiliaji ulianza na watu hao walipogundua wanafuatiliwa na walinzi ili wakamatwe, walitawanyika na kusambaa ili kukwepa kukamatwa.

Amedai miongoni mwa watu hao watano, watatu walipita eneo lenye ulinzi na walipotakiwa kujisalimisha, akiwemo marehemu, walikaidi agizo hilo huku wakiwa wameshika sululu na nyundo walizotumia kuvunja mawe.

“Walinzi waliokuwa eneo hilo walichukua tahadhari zote za kiusalama ili kusitokee madhara kwao na kwa watu wengine na kuhakikisha wanafanya ukamataji salama.

“Lakini watu hao waliendelea kukimbia kuelekea kwenye maeneo ambayo si salama kwao, ikizingatiwa kuwa licha ya watuhumiwa hao kuingia visivyo halali pia hawakuwa na vifaa maalum vya kujikinga na hatari,” amesema Jongo.

Kamanda Jongo amesema siku hiyo hiyo, saa 11.30 jioni, Emmanuel Sitta alipatikana akiwa na jeraha kichwani upande wa kushoto na alikimbizwa hospitali ya wilaya ya Geita, na ilipofika saa 3.45 usiku alifariki dunia.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi wa tukio hilo ukifanyika.

Watuhumiwa wengine waliokamatwa

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia watu 11 kwa tuhuma za kukutwa na laini 9,389 za mitandao mbalimbali ya simu walizokuwa wakitumia kufanyia uhalifu kwa njia ya mtandao na unyang’anyi.

Kamanda Jongo amethibitisha kuwakamata watu hao na kusema walikamatwa Machi 13, 2025, katika kata ya Ludete Wilaya ya Geita, baada ya polisi kupata taarifa ya uwepo wa wahalifu na kuweka mtego uliofanikisha kuwakamata wakiwa na vifaa vyao vya kufanyia uhalifu.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Ilege Charles (42), Shabani Abdallah (25), Daudi Omary (25), Alex Rashid (32), Jumanne Mageso (27), Meshack Bahebe (31), Alex Edward (29), Nkwabi Ipilinga (21), Dennis Ndihunze (33), Vicent Vedastus (25) na Hamduni Issa (30).

Aidha, watuhumiwa hao pia wamekutwa na vifaa mbalimbali vya kufanyia uhalifu, ikiwemo kompyuta mpakato (Laptop) moja aina ya HP, mashine mbili za kusajili line kwa kutumia alama za vidole, simu janja “Smartphone” 15, pamoja na simu ndogo za kawaida 18.

Vifaa vingine ni pamoja na Sim card mpya za mitandao mbalimbali 1,600, mabaki ya Sim card za mitandao mbalimbali jumla 6,189, line za Yass (Tigo) zilizosajiliwa 2,600 na begi tatu za mgongoni.

Kamanda Jongo amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na taasisi nyingine ili kubaini mtandao mzima wa wahalifu hao na kuwachukulia hatua za kisheria.

Related Posts