Kisa hiki kinamhusu rafiki yetu. Siku moja, alisimulia kuwa kulikuwa na mabishano juu ya suala la kifamilia baina ya mkewe na kaka zake wawili ambao ni mashemeji zake.
Katika ubishi huu, mke wa jamaa aliwapinga kaka zake juu ya jambo fulani kiasi cha kuwaudhi. Mmojawapo wa wale kinakaka ambaye ni mkubwa kwa kufuatana na mke wa jamaa, alimtishia dada yake kuwa angeweza kumpiga.
Kwanza, alisahau kuwa, pamoja na kuwa dada yake, alikuwa mke wa mtu. Pili, alisahau kuwa jukumu walilomkabidhi shemeji mtu alipomuoa dada yao ilikuwa ni kumlinda na kumtunza dhidi ya hatari au tishio lolote.
Tatu, hakujua au alijua lakini akasahau kuwa shemeji yake alimpenda na kumheshimu sana mkewe kiasi cha kutoweza kuvumilia kuwa shahidi wa udhalilishaji au utesaji wake.
Kaka mtu alipomtishia dada yake kuwa angempiga, shemeji mtu aliamka kwenye kiti pembeni ya mkutano wa ndugu na kumwambia shemeji yake “huwezi kumpiga mke wangu nami nikuache. Tutapigana liwalo na liwe.”
Kwa vile wale kaka hawakutegemea kitu hiki, walishangaa na kuogopa kiasi cha kuwataka radhi dada yao na mumewe na ugomvi kuishia hapo.
Baada ya tukio hili, kaka mtu walimheshimu dada yao kiasi cha kuwa wakisimulia kisa kile mara kwa mara kwa kuangua vicheko.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa, kaka mtu walizoea kusema kuwa mumewe alikuwa amemfundisha kuwa na roho ngumu, yaani ugaidi. Kwani, hawakutegemea kuwa shemeji yao angeonyesha hasira na kuamua kuingilia ugomvi wa kifamilia.
Badala ya kukuta ndugu wakigombana na kuchukua jembe akalime kama wahenga wanavyotuusia, mume mtu aliamua kuingilia kati akimkingia kifua mkewe. Jambo hili liliwapa somo kubwa wahusika.
Kadhalika, jambo hili linatoa funzo kwa wengine kuwa, kama utamlinda mwenzio, hakuna atakayehatarisha maisha yake kwa kuwa tayari kumdhuru.
Isitoshe, kama mke au mume ni mwili mmoja, kama mmoja atadhalilishwa au kupigwa, na mwingine, kadhalika atakuwa amedhalilishwa na kupigwa.
Jamaa alitueleza kuwa baada ya mkasa kusuluhishwa hivyo, mashemeji zake walizoea kumuuliza ni kwanini aliamua kuingilia ugomvi wa ndugu badala ya kuchukua jembe akalime?
Aliwajibu kuwa, kama angelaza damu na mkewe akadhalilishwa au kupigwa, angeenda kulipia nyumbani mbali na kushindwa kumlinda na kumheshimisha mkewe.
Hivyo, alizoea kuwajibu kuwa walipompa dada yao amuoe, walikoma kuwa na mamlaka juu yake. Kwa maana nyingine, wahusika siyo walitaka kuwadhalilisha na kuwaumiza hawa wawili tu bali kupora madaraka ya shemeji yao.
Je, ni wangapi wanaliona hili hivi kiasi cha kuwahami wenza wao kama alivyofanya jamaa huyu? Ni wangapi wangechukua majembe na kwenda kulima wakati wakiacha mambo ya familia kama yalivyo japo aliyekuwa akiumizwa ni mke mtu?
Je, wewe ungefanya nini katika hali hii? Je hili limewatokea wangapi na walichukua hatua gani? Si vibaya kumlinda na kumhami umpendaye hasa anapokuwa mke au mumeo. Tuna wajibu kwa wenzetu kama walivyo nao kwetu pia.
Hivyo, unapokutana na changamoto au tishio kama hili, wala usisite wala kuona aibu kumhami mwenzio. Kwani, kumhami ni wajibu wako na kutomhami ni kushindwa kutekeleza wajibu wako kwake na kwako. Hisani, siku zote, huanzia nyumbani. Kupenda siyo kuambizana nakupenda bali kuonyesha upendo kwa matendo.
Hata sheria nyingi ziko wazi kiasi cha kuzuia mke kuwa shahidi dhidi ya mumewe. Chini ya kile kinachoitwa ‘spousal testimonial privilege ‘au haki ya ushahidi wa mwanandoa dhidi ya mwenzake, mwanandoa ana haki ya kukataa kutoa ushahidi dhidi ya mwenzie.
Hata hivyo, sheria hii humpa haki haki hii mwanandoa kwa makosa yaliyodaiwa kutendeka wakati wakiwa katika ndoa si kabla au baada ya kuachana.
Sheria, mara nyingi, ni kipofu na haina huruma. Ila katika kuleta amani katika ndoa, inatoa haki hii kwa wanandoa.
Hivyo, wanandoa wasiojua sheria wasilazimishwe kutoa ushahidi dhidi ya wenza wao kwa vile jukumu lao ni kulindana na kuhamiana katika kila hali. Pia, kumhami au kumlinda mwenza wako si hisani kwake bali wajibu wako kwake.