Geita. Wanafunzi 1,969 kutoka shule mbili za Igwamanoni na Kakoyoyo zilizopo Kata ya Bulega wilayani Bukombe, Mkoa wa Geita, wanalazimika kusoma kwa kupokezana katika Shule ya Msingi Igwamanoni kutokana na hali mbaya ya madarasa ya shule ya Kakoyoyo.
Vyumba vya madarasa vya Kakoyoyo vimeonekana kutitia na kupata nyufa, hali inayotishia usalama wa wanafunzi.
Shule ya Msingi Kakoyoyo yenye wanafunzi 934 wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 13 kila siku kwenda shule ya Igwamanoni kutokana na madarasa kutitia na kupata nyufa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha mapema mwaka 2024.
Kutokana na changamoto hiyo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Zainab Katimba ametembelea shule hiyo, kuona uhalisia, na kuahidi Serikali itaanza ukarabati baada ya tathmini ya wataalamu itakapokamilika.
“Tumeona uhitaji mkubwa wa kurejesha shule hii, na kupitia mapato ya ndani, Serikali Kuu, pamoja na wadau wa maendeleo tutahakikisha ukarabati unafanyika ili wanafunzi waendelee kusoma katika mazingira bora,” amesema.
Diwani wa Bulega, Erick Kagoma, amesema kwa sasa wanafunzi 1,035 wa shule ya Igwamanoni wanasoma asubuhi hadi mchana na kuwapisha wale wa Kakoyoyo wanaosoma mchana hadi jioni.
“Zile mvua za mwaka jana mwanzoni zilisababisha baadhi ya madarasa kuonyesha dalili za kutitia, lakini lipofika Juni 2024, chumba kimoja cha darasa kilidondoka. Hii hali ilihatarisha usalama wa watoto, nikaenda Halmashauri, nilimueleza Mkurugenzi aliyetuma wataalamu kukagua na waliona sio salama kwa watoto kuendelea kuwa pale,” amesema.

Kwa mujibu wa diwani, baada ya wataalamu kuthibitisha madarasa hayo sio salama kwa wanafunzi, Mkurugenzi aliandika barua ya kuifunga shule kwa muda ili wajipange kwa ajili ya ukarabati.
“Hata mtihani wa darasa la saba mwaka jana, wanafunzi wa Kakoyoyo walifanyia shule ya Igwamanoni. Huu umbali mrefu unasababisha utoro wa wanafunzi, lakini Serikali yetu sikivu imeahidi kujenga upya ili wanafunzi waweze kusoma karibu,” amesema Kagoma.
Ziara hiyo imefanyika kutokana na ombi la mbunge wa Bukombe, Dk Doto Biteko, ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ili kuwapa wananchi taarifa kuhusu hatua za Serikali katika kuboresha shule hiyo.