Vijana 200 Tanzania, Burundi kulipiwa mahari kupitia Al-Hikma

Dar es Salaam. Taasisi ya dini ya Kiislamu ya Al-Hikma Foundation imetangaza kuwalipia mahari vijana 200 kutoka nchi za Tanzania na Burundi ambao wapo tayari kuoa.

Tangazo hilo limetolewa katika mashindano ya 25 ya kimataifa ya uhifadhi wa Qur’an, yaliyofanyika leo Jumapili Machi 16, 2023. Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Mshindi wa mashindano hayo, aliyekuwa akiwakilisha Urusi, Aiemiddin Farkhudinov, alishinda nafasi ya kwanza kati ya washiriki 17 na kujinyakulia zawadi ya fedha taslimu Sh30 milioni.

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Hassan Mwinyi akihutubia katika mashindano ya Quran yaliyoandaliwa na Al-Hikma Foundation

Mashindano hayo yalifanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, huku Uwanja wa Uhuru pia ukitumika kutokana na idadi kubwa ya wahudhuriaji, kiasi cha kujaza viwanja vyote viwili.

Akizungumza katika mashindano hayo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, Sheikh Nurdin Kishki, amesema kuwa mwaka huu, taasisi yake itawalipia mahari vijana 100 kutoka Tanzania na wengine 100 kutoka Burundi.

“Kutokana na idadi ya watu wasiokuwa kwenye ndoa kuwa kubwa, mwaka huu tutaozesha vijana 200; ndoa 100 zitafungwa Tanzania na 100 nyingine kwa ndugu zetu wa Burundi,” amesema.

Sheikh Kishki amesema kuwa mahari pamoja na gharama nyingine za ndoa, ikiwemo ukumbi, vyakula, vinywaji, na nguo za maharusi zitalipwa na taasisi hiyo.

Pia, alisema kwamba pamoja na kulipia mahari, vijana watafanya tohara kwa watoto wa kiume 1,000 hapa nchini bila malipo.

Mbali na tohara, taasisi hiyo ilitoa tiketi kwa watu wawili za kwenda kwenye ibada ya Hija na nne za Ummra ambao namba zao za kuingia uwanjani hapo zilitangazwa baada ya mashindano hayo. Kila aliyehudhuria alipewa namba wakati kuingia.

Hii si mara ya kwanza kwa taasisi hiyo kutangaza kuwalipia mahari vijana wasiokuwa na uwezo ili waweze kuoa.

Aprili 9, 2023, katika mashindano kama hayo ya 23, Sheikh Nurdin Kishki alitangaza kulipia vijana 50 mahari kwa ajili ya kufunga ndoa.

Alieleza kuwa vigezo ni kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za ndoa na isiwe kuongeza mke mwingine.

Hata hivyo, taasisi hiyo ilipokea maombi zaidi ya 1,000 kutoka mikoa mbalimbali nchini na kati ya hayo iliwachagua vijana 70, ambao walifanyiwa harusi ya pamoja iliyofanyika Agosti 6, 2023.

Sheikh Kishki alisema kuwa mambo haya yanafanyika kupitia programu maalumu iliyoanzishwa na taasisi hiyo ya kurejesha kwa jamii kupitia mashindano hayo kwa kushirikiana na Ubalozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo.

Ameongeza kuwa baada ya mashindano hayo kufanyika jijini Dar es Salaam, baada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, mashindano mengine yatafanyika jijini Arusha kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, aliyetaka mashindano hayo pia yafanyike katika mkoa wake.

“Baada ya Ramadhani, mashindano haya yatafanyika tena katika Jiji la Arusha kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa huyo, Paul Makonda. Natumaini kama tulivyoujaza uwanja wa Benjamin Mkapa na Uhuru, ndivyo tutakavyofanya huko,” amesema.

Mwinyi ahimiza watoto kufundishwa dini

Akizungumza katika mashindano hayo, Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, aliyekuwa mgeni rasmi, amewasihi wazazi kuhimiza watoto wao kusoma na kuhifadhi Qur’an, kwani ni njia mojawapo ya kukienzi kitabu hicho kitakatifu.

Pia, amesema kuwa kufanya hivyo kutasaidia kutengeneza masheikh na maulamaa wa baadaye.

Vilevile, ametumia fursa hiyo kuwasihi Waislamu kumuomba Mwenyezi Mungu msamaha kwa makosa yote waliyoyafanya kwa kujua au kutokujua.

Katika kipindi hiki cha Ramadhani, amesisitiza kuendeleza desturi ya kufanya mema, kushirikiana, na kusaidiana ili kuwafariji wale wanaopitia hali ngumu.

Ameongeza kuwa uwepo wa mashindano kama hayo ni muhimu katika kuleta umoja na ushirikiano miongoni mwa waumini, na ni ushahidi kwamba nchi inazingatia uhuru wa kuabudu na kutoa ushirikiano wa kutosha katika masuala ya dini bila kujali dhehebu la mtu.

Kwa upande wake Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amewahimiza Watanzania kuilinda amani, utulivu kwa mwaka huu ambapo nchi inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, Oktoba 2025.

Katika fainali za mashindano hayo, mshindi Aiemiddin Farkhudinov akiwakilisha Urusi ameshinda nafasi ya kwanza kati ya washiriki 17 na kujinyakulia zawadi ya fedha taslimu Sh30 milioni.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Abdulmuhaimin Mohamed Jumah kutoka Libya, mshindi wa tatu alikuwa Eslam Ahmed kutoka Misri, mshindi wa nne ni Saalihi Rahim kutoka Guyana, na nafasi ya tano ikaenda kwa Kassim Ayoub Salim aliyewakilisha Tanzania Bara.

Pia, mshiriki mwenye miaka 11 kutoka Uganda, Abdallah Minshawi, alishinda katika kategoria mbili: kuwa mshiriki mdogo kuliko wote na msomaji mwenye sauti nzuri kuliko washiriki wote 17.      

Nafasi ya pili imechukuliwa na Abdulmuhaimin Mohamed Jumah kutoka Libya, mshindi wa tatu akawa Eslam  Ahmed kutoka Misri, mshindi wa nne ni Saalihi Rahim kutoka Guyana na nafasi ya tano ikaenda kwa Kassim Ayoub Salim aliyeiwakilisha Tanzania Bara.

Pia, mshiriki mwenye miaka 11 kutoka nchini Uganda Abdallah Minshawi ameshinda katika kategoria mbili ambazo ni kuwa mshiriki mdogo kuliko wote na msomaji mwenye sauti nzuri kuliko washiriki wote 17.

Related Posts