Dar es Salaam. Baada ya kukamilika mchakato wa kupangiwa vituo vya kazi, waombaji wote wa kazi za mkataba katika Mpango wa Uwekezaji katika Afya ya Mama na Mtoto nchini Tanzania (TMCHIP), wametakiwa kuripoti kazini.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), waajiriwa hao 435 wanatakiwa kuripoti kazini ndani ya siku 14 kuanzia jana, Machi 15, 2025.
Waajiriwa hao ni wale walioomba nafasi mbalimbali za ajira za TMCHIP katika kada ya afya zilizotangazwa Desemba mwaka jana.
Taarifa hiyo, ilitolewa na Tamisemi jana Machi 15, 2025 kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Adolf Ndunguru.
Taarifa hiyo imeeleza kwa waombaji ambao hawataripoti ndani ya siku 14, nafasi zao zitajazwa haraka kutoka kwa wengine walioomba.
Mbali na kuripoti ndani ya siku 14, waajiriwa hao wanapaswa kuwasilisha vyeti halisi vya kidato cha nne, sita, chuo kikuu, Nacte na vyeti halisi vya usajili wa mabaraza ya kitaaluma
kwa ajili ya uhakiki kabla ya kupewa barua ya ajira.
“Waombaji waliopata nafasi za ajira watakaoripoti bila ya kuwa na vyeti halisi hawatapokelewa,” imeeleza taarifa hiyo.
Pia, imeelezwa hakutakuwa na nafasi ya kubadilisha vituo vya kazi walivyopangiwa waajiriwa hao wapya.
Hata hivyo, taarifa hiyo imesisitiza waombaji wote ambao majina yao hayakuonekana watambue kuwa hawakupata nafasi, hivyo wasisite kuomba kwa mara nyingine zitakapotangazwa.
“Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wanaelekezwa kuwapokea, kuhakiki vyeti na kuwafanyia mafunzo elekeziĀ kabla ya kuwapangia vituo vya kazi,” imeeleza.