Dodoma. Wakati Umoja wa Walimu Wasio na Ajira (Neto) ukipendekeza serikalini umri wa kustaafu uwe miaka 50, wadau wamesema hoja hiyo ni ‘mfu’ kwani haiwezekani kuwaondoa mapema wenye uwezo wa kuzalisha kazini.
Hoja ya kustaafu kwa umri wa miaka 50 badala ya 60 ni moja ya hoja sita zilizotolewa na Neto katika mapendekezo yao kwa Serikali.
Mambo mengine yaliyowasilishwa katika andiko lao lenye kurasa 22 ni masuala ya mtalaa mpya, usaili wa ajira za walimu, uzalishaji wa walimu, hali ya maisha ya walimu wasio na ajira mitaani, na uhaba wa walimu.
Katibu wa Neto, Daniel Mkinga, amesema katika andiko hilo walitoa pia mapendekezo ya nini kifanyike, na kwamba mawaziri waliwasikiliza na kuyapokea.
Amesema viongozi wengi wamekuwa wakisisitiza vijana wajiajiri, hivyo wanaomba umri wa kustaafu upunguzwe hadi miaka 50 ili vijana wapate haki yao ya kulitumikia Taifa.
“Ndugu viongozi wetu, kwa kuzingatia haki sawa kwa wote, tunaomba umri wa kustaafu upunguzwe hadi miaka 50. Tunakumbuka kwamba viongozi wengi wamekuwa wakisisitiza vijana tujiajiri, hivyo basi tunaomba umri wa kustaafu uwe miaka 50 ili vijana nao wapate haki yao ya kulitumikia taifa.
“Kuruhusu watu kufanya kazi mpaka umri wa miaka 60 ndio wastaafu kunawanyima vijana haki ya kulitumikia taifa lao,” amesema Mkinga.
Mkinga pia amependekeza kwamba kwa wale ambao umri umeenda, wapewe ajira ya mkataba wa miaka 20 wafanye kazi serikalini.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Hery Mkunda, akizungumza leo Jumapili, Machi 16, 2025. amesema changamoto ya ajira si ya walimu pekee, na ndiyo maana Serikali ilibadili mitaala ya elimu ili kuwawezesha watu kujifunza ujuzi.
“Ni kweli ajira hazitoshelezi na si walimu pekee yao. Hata nyie waandishi habari, wapo kibao mtaani hawana kazi. Hivi wao wanafikiria kupunguza umri wa kustaafu kwa kuwa inaweza kupunguza demand (mahitaji) sokoni. Inaonekana hii hoja ni mfu kwa mtazamo wangu wa haraka haraka,” amesema Mkunda.
Amesema mtazamo wa kupunguza umri hauwezi kumaliza changamoto, bali kunahitajika kutafuta suluhisho kubwa, ikiwemo mabadiliko ya mtalaa utakaowezesha watu kujiajiri na kuongeza ubunifu.
Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na mchumi, Dk Lutengano Mwinuka, amesema changamoto ya ajira ipo pia katika kada nyingine, na kutaka isitafsiriwe kwamba ni kundi dogo la walimu tu ndilo linakabiliwa na changamoto hiyo.
Amesema kuwa watumishi wakistaafu wakiwa na umri wa miaka 50, mifuko ya pensheni itaanza kulipa mafao wakati watu wangali na nguvu za kufanya kazi, kulingana na tafiti zilizofanyika.
“Suluhu nzuri ya changamoto hii ni kutengeneza ajira nyingi kwenye sekta rasmi na isiyo rasmi na sio kuondoa ajira kwa wale ambao wako kwenye ajira,” amesema Dk Mwinuka.
Amesema suala la kuwaondoa kazini watu wenye uwezo wa kuzalisha ni suala ambalo halitekelezeki na halina mantiki kama walivyoshauri.
Dk Mwinuka amesema mwaka huu Serikali imeanzisha somo la biashara kuwa ni lazima kwa wanafunzi wa shule za sekondari, na ni vyuo vichache vinavyotoa walimu wenye uwezo wa kulifundisha.
“Hivyo, kungeweza kuwa na mpango kabambe wa kuweza kupata walimu wa eneo hilo ambao watakwenda kufundisha somo lenye mahitaji makubwa ya kitaifa. Ingekuwa ni chanzo cha ajira kwa wasio na ajira, ikawepo programu maalumu kwa walimu (wasio na ajira) wakaongezewa ujuzi kidogo katika masomo ya biashara ili waingie katika mfumo rasmi,” amesema.
Mkinga amesema Serikali ina nia njema katika kuanzisha mchakato wa kuwafanyia usaili walimu, lakini umekuwa na mapungufu mbalimbali katika utaratibu huo mpya kupitia mfumo wa ajira portal.
Amesema usaili hauna vigezo na sio wa haki kutokana na kuwahusisha walimu wote kuanzia waliohitimu mwaka 2015 hadi 2023 na kwamba sio haki kuwapima kwa pamoja bila kuzingatia miaka waliohitimu mafunzo yao.
“Tunashauri mchakato wa kuajiri urudishwe Ofisi ya Rais Tamisemi kama zamani na uanze kuajiri wahitimu wa miaka ya nyuma kwa sababu kuna watu wana miaka 10 bila ajira na wanaelekea kufikisha miaka 45, hivyo watakosa sifa ya kuajiriwa serikalini kwa mujibu wa sheria,” amesema Mkinga.
Mkinga amesema katika andiko lao wameshauri uzalishwaji wa walimu uzingatie uhitaji wa walimu shuleni, pia kada ya elimu iwekewe masharti yatakayopandisha hadhi kwa kada ya ualimu na walimu kwa ujumla.
“Kwani kwa sasa ualimu umeshushwa hadhi mpaka walio wengi wanaona aibu kutoka hadharani na kusema mimi ni mwalimu. Tunaiomba Serikali itazame upya namna ya kumuandaa mwalimu na kada hii isimamiwe na watu waliosomea ualimu tu bila kuwahusisha siasa kwa namna yoyote ile,” amesema.
Katika andiko hilo lenye kurasa 22, walimu hao wamesema vijana wengi ambao hawajaajiriwa kwa kada ya ualimu ni wale waliotoka katika familia maskini na wamesomeshwa na wazazi na kupewa mikopo na Serikali kwa matumaini ya kuwa watapata ajira kwa haraka.
Mkinga amesema, “Walimu tusio na ajira tuna majonzi makubwa, kwani kuwepo kwetu mtaani miaka mingi siyo kwa mapenzi yetu bali ni kwa sababu ya Serikali iliamua kusitisha zoezi la kuajiri kwa mkupuo mwaka 2015 kwa kigezo cha kuondoa watumishi hewa, wastaafu na waliofariki ndipo wataajiri.”