Tanga. Wananchi wa Pangani wameanza kupiga hesabu za kibiashara baada ya kukamilika kwa Daraja la Pangani linaloiunganisha Barabara ya Tanga- Pangani-Bagamoyo yenye urefu wa kilomita 256.
Mwishoni mwa wiki, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imekagua mradi huo na mingine ya kimkakati mkoani Tanga huku ikitaka kasi ya ujenzi wa daraja iendane na ujenzi wa Barabara ya Tanga-Pangani- Bagamoyo.
Ujenzi huo pia unatajwa kubadili madhari ya Pangani, eneo linalosifika kwa uvuvi wa samaki na kilimo cha minazi.

Ujenzi wa daraja umeanza kuonyesha fursa, baadhi ya maeneo inakopita barabara hiyo yakitengwa kwa ajili ya hoteli, vituo vya mafuta na uwekezaji mwingine, huku wananchi wa eneo hilo wakipiga hesabu ya kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja kwa kutumia fursa zinazotazamiwa baada ya ujenzi.
Daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 linalojengwa kwa kutumia teknolojia iliyotumika kujenga madaraja ya Tanzanite, Dar es Salaam na Wami linatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
Mbali na daraja, kipande cha Barabara ya Tanga-Pangani cha urefu wa kilomita 15.8 tayari kimekamilika, huku eneo lililosalia la ujenzi wa barabara katika awamu ya kwanza (lot one) likitarajiwa kukamilika Juni 16, 2025.
Mhandisi wa mradi huo, Gladson Yohana amesema ujenzi wa daraja hilo umefika asilimia 38 na hadi kukamilika litagharimu Sh 88.2 bilioni.

Yohana amesema, ujenzi wa daraja hilo utakuwa na barabara ya chini ya ushiroba ya ushongo na kuna barabara nyingine ya juu.
“Pia, katikati ya daraja tumeacha eneo pana, ambalo linaruhusu meli yenye upana wa futi 60 na boti kupita chini,” amesema.
Licha ya biashara ya samaki na nazi kutajwa kuwa kubwa zaidi Pangani, wakazi wa eneo hilo wanapiga hesabu ya kufanya biashara nyingine baada ya ujenzi huo kukamilika.
Ibrahim Kidiwa amesema biashara kubwa ya Pangani ni samaki na nazi, pia kuna maeneo ya mashamba ya mkonge.
“Huku kuna minazi, samaki ukienda nga’mbo eneo la Bweni kuna njia ya kwenda Mwera ambako ndipo kuna mashamba ya mkonge, hizi ndiyo kazi zetu kubwa huku,”amesema.
Amesema uwepo wa daraja na barabara hiyo kumeanza kumuonyesha njia ya kupanua wigo kwenye biashara yake ya samaki.
Mwazoa Hussein ambaye ni mkulima wa mkonge amesema daraja litakapokamilika wanatarajia eneo hilo litakuwa ‘busy’ kwa saa 24.
“Tumesikia kwenye barabara hii kutajengwa vituo vya mafuta, hoteli na vitega uchumi vingine, hii itaufungua mji wetu wa Pangani, ambacho nakifikiria ni kufanya biashara ya vinywaji baridi, kwa kuwa naiona fursa hiyo,” amesema.
Mfanyabiashara ndogo ndogo, Mwaija Athuman amesema uwepo wa daraja hilo utaiweka Pangani kwenye neema, akipiga hesabu ya kuboresha biashara yake ya chakula.
“Tulikuwa kama tumesahaulika, tujikiona tuko pembezoni, mabasi ya abiria yataanza kupita Pangani daraja na barabara hii vitakapokamilika, tushindwe sisi tu kutafuta riziki,” amesema Mwaija.
Pia, amesema ameanza kudunduliza pesa kidogo kidogo ili fursa ikianza awe tayari na mtaji wa kutosha.
Majala Mathayo amesema mbali na kulitazama daraja na barabara hiyo kufungua uchumi wa Tanga, wanatarajia kipato cha mtu mmoja mmoja kitaimarika.
“Hapa ni kuanza kujiandaa kufanya kazi, tusitegemee kushinda vibarazani halafu tuseme maisha magumu, tujiongeze, tumeletewa fursa mlangoni, sehemu inapokuwa na miundombinu kama hivi maana yake kuna fursa,” amesema,
Mbali na biashara, madhari ya Pangani na maeneo jirani yanatarajiwa kubadilika na kuongeza fursa kwa wakazi wa maeneo hayo na mkoa huku daraja na barabara hiyo vikitajwa kuwa njia ya mkato kutoka Tanga, Bagamoyo mpaka Dar es Salaam kwa wasafiri.
Ujenzi kukamilika Desemba
Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya alisema kipande cha Barabara ya Tanga-Pangani kitakamilika Juni mwaka huu huku daraja likitarajiwa kukamilika Desemba.
“Tumejipanga kuhakikisha sehemu hii ya kwanza ya Tanga-Pangani inakamilika ifikapo mwezi Juni wakati daraja likitarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu,” amesema Kasekenya.
Kamati ya Bunge yasisitiza
Jana Jumamosi, Machi 15, 2025, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Moshi Kakoso amesema kazi iliyokwishafanywa kwenye daraja hilo ni kubwa hivyo Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), wahakikishe linakamilika kwa wakati ili kukuza fursa za uwekezaji katika ushoroba wa fukwe za mikoa ya Tanga na Pwani.
Mwananchi imeshuhudia ujenzi wa barabara hiyo ukiendelea ukiwa umegawanywa katika sehemu nne.
Akifafanua mgawanyo huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Mohamed Besta amesema sehemu ya kwanza ni kipande cha Tanga-Pangani cha kilomita 50 ambacho tayari kipande cha kilomita 15.8 kimekamilika.
Sehemu nyingine ni Daraja la Pangani la mita 525 na barabara unganishi ya kilomita 25.6.
Sehemu ya tatu ni Barabara ya Mkange-Mkwaja-Tungamaa ya kilomita 95.2 na sehemu ya nne ni kutoka Mkange-Bagamoyo Makurunge kilomita 73.25 ambayo usanifu wake umekamilika.
“Kukamilika kwa barabara hii kutachochea ukuaji wa uchumi, kupunguza gharama na muda wa safari, kuwezesha kufikika kwa urahisi kwenye vivutio vya utalii na kuunganisha kwa njia fupi bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mombasa.
Kamati ya Bunge ya Miundombinu pia imekagua Kivuko cha Pangani ambacho kipo mita chache kutoka linapojengwa daraja.
Mwananchi ilishuhudia kivuko hicho kikiwa kimechaaa huku kamati ikikiri kinahitaji kuboreshwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Msonde amesema wanahitaji Sh2 bilioni ili kikarabatiwe kiendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Dk Msonde amesema daraja litakapokamilika litakuwa ni mbadala kwa wananchi wa Pangani na kivuko hicho kitahamishiwa eneo jingine lenye uhitaji.
Mbali na ukaguzi wa kivuko na daraja, kamati pia ilikagua miradi ya bandari, uwanja wa ndege na reli huku ikishauri kuwe na mfumo wa kuiunganisha bandari, barabara na reli kwa ajili ya kuwa na miradi endelevu itakayoleta tija jijini Tanga.
Katika ukarabati wa reli ya Ruvu-Tanga inayokwenda hadi Kilimanjaro mpaka Arusha, kamati imesema kiasi cha pesa kinachotolewa ni kidogo ikishauri kiongezwe ikisisitiza reli hiyo ni muhimu na itafungua uchumi mkubwa wa mikoa hiyo.
Upande wa bandari kamati ilishauri kuunganisha mifumo yake na reli na barabara ikibainisha kwenye mkoa huo kuna bomba la mafuta, hivyo barabara ya Afrika Mashariki ikifunguka nchi za Rwanda, Burundi na Uganda wataitumia zaidi bandari ya Tanga.
Kamati ilitaka upanuzi wa uwanja wa ndege uanze na jengo la abiria liwe na uwezo wa kubeba watu 250 hadi 300 na isiwe 150 kama ambavyo ramani inaonyesha.
Awali, Wizara ya Ujenzi ilisema upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tanga uliojengwa mwaka 1942 ukikamilika utaupandisha hadhi kutoka daraja 2C kwenda 3C na kuwa na uwezo wa kupokea ndege za aina ya Bombandier Dash 8 – Q400.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amesema miradi hiyo inakwenda kurejesha hadhi ya Mkoa wa Tanga, akibainisha ukuaji wake wa bandari ni wa pili nchini katika masuala ya kiforodha na mapato baada ya Bandari ya Dar es Salaam.
“Shehena imeongezeka kutoka tani laki nne na sabini hadi tani zaidi ya 1.1 milioni baada ya bandari kufanyiwa ukarabati,” amesema.
Hadi sasa idadi ya meli zinatotumia bandari hiyo ni 307 kutoka 118 za mwaka 2019 huku mapato yakiongezeka kutoka Sh17.2 bilioni hadi Sh45.6 bilioni.