WASIRA ATOA RAI KWA VIJANA KUGOMBEA UBUNGE,UDIWANI KATIKA UCHAGUZI MKUU 2025

Na Said Mwishehe,Ileje

VIJANA wenye sifa jitokezeni kugombea nafasi za ubunge na udiwani katika uchaguzi Mkuu mwaka huu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara Stephen Wasira alipokuwa akizungumza na wanachama wa Chama hicho Wilaya ya Ileje mkoani Songwe.

Wasira amesema kwa vijana ambao wanajiona wana uwezo na sifa za kugombea udiwani au ubunge wajipange katika uchaguzi Mkuu ujao kwani hakuna mwenye haki miliki ya kushikilia nafasi hizo kwa miaka mitano, isipokuwa leseni zinapatikana kupitia kinyang’anyiro cha kushawishi wananchi na mwenye nguvu ya kushawishi wanapata ridhaa.

Makamu Mwenyekiti Wasira alitoa Maelezo hayo alipokuwa akiunga hoja iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama hicho mkoa wa Songwe Radiweli Mwapashi akiyetaka kuona vijana wapewe nafasi katika uchaguzi huo.

Wasira amesema ili kada apate nafasi ndani ya chama hicho lazima apambane na kukubalika kwa wananchi na kuongeza hata wabunge na madiwani waliopo hawakugombea peke yao.

Amesema katika uchaguzi Mkuu mwaka huu hakuna mtu kupita bila kupingwa kwahiyo hata watakao gombea lazima walijue hilo maana wamekubaliana kijana kama anataka kugombea muda ukifika ajitokeze na kama anataka kuwa msindikizaji shauri yake.

Wasira amesema katika kuelekea uchaguzi huo kwa nafasi ya udiwani na ubunge vitakuwa wazi isipokuwa nafasi ya urais pekee ambayo tayari Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika Dodoma umeshapitisha jina la Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea Urais.

Amesisitiza mkutano mkuu maalum ulikubali nafasi ya Urais kugombewa na Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi nzuri aliyofanya ndani ya kipindi chake cha miaka minne ya uongozi wake.

“Tanzania inavijana wengi na kazi ya CCM ni kujenga viongozi bora kazi waliyoifanya tangu kupata uhuru hivyo wajitokeze wakanolewe ili wawe tayari kuwatumikia wananchi.”

Awali Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe Radiweli Mwapashi amesema vijana wengi hasa katika mkoa huo wanaingiwa na uoga kukabiliana na madiwani na wabunge watakaotetea nafasi hizo katika uchaguzi ujao.

Hata hivyo amesema kuhamasisha vijana wachukue fomu isitafsiriwe kuwa anawabagua au kuwatenga waliopo madarakani, bali anatamani kuona wanatengeneza viongozi vijana ili Chama hicho kiendelee kupika viongozi kizazi hadi kizazi.

Related Posts