MSHAMBULIAJI wa Al Mina’a inayoshiriki Ligi Kuu nchini Iraq, Wazir Jr Shentembo ugumu wa ligi hiyo unampa changamoto ya kuipambania timu hiyo.
Mina’a iko nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi hiyo maarufu ‘Iraq Stars League’ ikiwa na pointi 25 kwenye mechi 24 ilizocheza, ushindi mechi sita, sare saba na kupoteza 11.
Akizungumza na Mwanaspoti, Wazir Jr alikiri ugumu wa ligi hiyo huku akiahidi kuipambania timu hiyo kila anapopata nafasi ya kufunga ili itoke nafasi iliyopo.
“Ligi ina ushindani mkubwa kila timu inapambana kupata matokeo mazuri, natamani kila ninapopata nafasi ya kucheza niweze kuisaidia timu kupata ushindi kwa kufunga mabao kazi yangu ni kufunga,” alisema Wazir Jr.
Wazir Jr ambaye aliwahi kukipiga Yanga 2020/21, alisaini mkataba wa miezi sita hivi karibuni kujiunga na timu hiyo iliyopo nafasi ya 16 kati ya 20 zinazoshiriki ligi hiyo.
Nyota huyo anakipiga timu moja na Mkongomani, Tuisila Kisinda ambaye pia aliwahi kuwika na Yanga kwa misimu tofauti 2020/21 na 2022/23 alikotokea AS Vita ya nchini kwao.
Hata hivyo, usajili wa Wazir Jr unafanya kuwa na Watanzania wawili wanaokipiga ligi hiyo baada ya Simon Msuva kusajiliwa na Al Talaba na tayari amefunga mabao saba.