Askofu Shoo ataka mambo mawili uchaguzi mkuu

Moshi. Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya  Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo ameitaka Serikali kusimamia haki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kuhakikisha kunakuwepo na uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa ili kuepusha  yaliyojitokeza katika chaguzi zilizopita kujirudia.

Mbali na hilo amewataka pia wananchi, kutumia nafasi yao vizuri ya kushiriki katika uchaguzi na kuepuka kuingia kwenye vurugu, mapigano na tabia ya kutukana.

Askofu Shoo ambaye ni Mkuu wa KKKT mstaafu, ametoa rai hiyo jana Jumapili, Machi 16, 2025, wakati akitoa salamu za Dayosisi kwenye ibada ya uzindunzi wa jengo la Kanisa katika Usharika wa Kirua, Jimbo la Kilimanjaro Mashariki mkoani Kilimanjaro.

Amesema viongozi wa dini wameendelea kusimama imara na wanahitaji kuona kila mtu akipewa haki ya kushiriki uchaguzi mkuu kwa uhuru, amani na haki ikitendeka kwa kila atakayeshiriki kuchagua na kuchaguliwa.

“Huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu, tutakwenda kuchagua madiwani, wabunge na tutakwenda kumchagua Rais, sisi kama viongozi wenu wa dini tunatoa wito tena na tena hatutaki kuona yale yaliyotokea katika chaguzi zilizopita yakijirudia,” amesema Askofu Shoo.

“Kila mtu apewe haki yake ya kushiriki kwa uhuru , kwa amani katika uchaguzi mkuu, uhuru wa kuchagua, lakini pia uhuru na haki katika kuchaguliwa.

“Wananchi waweze kuwachagua wale wanaowapenda, wale ambao wanafahamu watakuwa wawakilishi wa kweli na watawawakilisha vyema, ili haki na amani ambavyo ndivyo msingi wa maendeeleo viweze kuwepo katika nchi yetu,” amesema.

Amesema “Kwa Watanzania wote natoa wito tutumie nafasi yetu hiyo vizuri na tusiingie katika vurugu, mapigano na matukakano. Mambo yote yatendeke kwa amani na kwa utaratibu.”

Askofu Shoo ametumia pia nafasi hiyo, kuwataka Wakristo kutumia kipindi  cha Kwaresma katika kutafakari na kuacha matendo maovu yakiwemo ya ukatili, wizi wa rasilimali za Taifa na kujilimbikizia mali kwa masilahi yao binafsi.

Amesema Tanzania kuna vilio vingi ambavyo vinasababishwa na Watanzania wenyewe kutendeana ukatili, kukosa uaminifu na kuliibia Taifa rasilimali zake huku wengine wakiiba kile kinachopangwa kwa ajili ya kusaidia wananchi wanyonge na maskini vijijini.

“Kila mahali tunapewa taarifa za ubadhirifu, wizi wa kutisha, watu wenye mamlaka na wasio na mamlaka kuhusu hii roho ya kuliibia Taifa, kujilimbikizia mali utafikiri utaenda nazo. Mali ambazo Serikali inawekeza ili kwenda kujenga miundombinu ya maji, shule, zahanati na vitu kama hivi alafu wachache,  waroho, wanaona kwamba ni nafasi ya kujitajirisha binafsi,” amesema Askofu Shoo na kuongeza kuwa

“Biblia inasema na neno la Mungu linatuambia inatosha na Kwaresma hii usikie sauti hiyo inatosha. Usijilimbikizie mali kwa ajili yako binafsi kwa njia zisizo halali eti kwa ajili yako na kwa ajili ya familia yako tu kwani mali zile badala ya kugeuka kuwa furaha unavyo tarajia wewe zitageuka kuwa pilipili, kuwa kitanzi kwako wewe maana itakuondolea furaha, amani na itakuondolea baraka za Mungu kwa kizazi chako”.

Amesema “Unawaibia watoto wa masikini, unawaibia watanzania maskini ambao ndio walipa kodi alafu unafanya unaona unafanya jambo sahihi bila dhamiri  yako kukuuma. Dhamiri ziamke, tuache kuwaibia Watanzania, tuache kuiba rasilimali za Nchi hii, kwa gharama ya wale walio wonyonge , Mungu anaona na Mungu anajibu, tuache ukatili tutendeane mema”.

Akizungumza Mchungaji  kiongozi wa usharika wa Kirua, Mchungaji James  Sambo amesema  ujenzi wa jengo hilo la ibada ulichukuwa muda wa miaka 22 hadi kukamilika na umegharimu  Sh100 milioni.

“Tunamshukuru Mungu kutuwezesha kukamilisha ujenzi huu wa nyumba ya Ibada, ambayo imetuchukua miaka 22, hadi kuikamilisha na kwa kanisa hili sasa kutasaidia   Wakristo wa Kilutheri kukutana na kuabudu kwa pamoja,” amesema Mchungaji Sambo.

Pia, baadhi ya waumini wa Kanisa hilo, wamesema kuzinduliwa kwa jengo hilo la ibada kunawapa uhuru wa kuabudu na kuondokana na changamoto waliyokuwa wakikumbana nayo hapo nyuma ya kushindwa kufanya huduma kutokana na kukosekana kwa nyumba ya ibada.

Related Posts