Changamoto sekta ya maji zatajwa

Dar es Salaam. Mabadiliko ya tabianchi, upotevu, wizi kwa baadhi ya watu na gharama za utekelezaji wa miradi ya maji zimetajwa kuwa changamoto zinazoikabili sekta ya maji huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji.

Changamoto hizo zinaelezwa wakati Tanzania ikitajwa kuwa na maji ya kutosha yaliyopo juu na chini ya ardhi.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amesema hayo leo Jumatatu Machi 17, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kikao maalumu cha wadau wa maji.

“Changamoto nyingine ni gharama ya usambazaji wa maji kutoka kwenye vyanzo kwenda maeneo mbalimbali yasiyo na maji ili kuyatibu, mchakato ambao unahitaji fedha nyingi,” amesema Mwajuma.

Amesema kutokana na hali hiyo, wizara inaendelea kukabiliana na changamoto huku ikisisitiza kutunza vyanzo vya maji kwa kuwa kuna athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.   

Mwajuma amesema ndio maana Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa Bwawa la Kidunda lililopo mkoani Morogoro kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya athari hizo.

“Huduma ya maji inaendelea kuimarika ila changamoto inayotukabili ni mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri vyanzo vya maji ambayo si Tanzania tu hata mataifa mengine. Hata hivyo, bado hatujafikia kwenye ukosefu wa maji,” amesema Mwajuma.

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa huduma hiyo, Mwajuma amesema  maeneo ya vijijini imefikia asilimia 83 kutoka 79 mwaka 2020 huku mijini ikifikia asilimia 91.6 kutoka asilimia 84 mwaka 2020.

“Lengo letu ni kufikia asilimia 85 vijijini na 95 mijini. Maendeleo haya yanatokana na mradi wa maendeleo ya maji unaoshirikiana na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi,”amesema Mwajuma.

Amesema maji yaliyopo juu na chini ya ardhi yapo ya kutosha kuhudumia mtu mmoja mmoja na juhudi zilizopo ni kuyatafuta ya chini na kuyasambaza ya juu ili yaweze kutumiwa.

Katika kukabiliana na hali hiyo, amesisitiza utunzwaji wa vyanzo vya maji ili yapatikane na yasambazwe.

Mwajuma amesema wadau wa maendeleo wanasisitiza kuangalia ubora wa maji unaopatikana na maabara zilizopo pamoja na kuangalia namna gani huduma hiyo inapatikana kwa wananchi.

Katibu Mkuu Kiongozi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi, Zena Said amesema sekta hiyo inapewa kipaumbele kwa kuwa inakuza uchumi wa nchi.

“Mradi wa maendeleo ya sekta ya maji ulioanza mwaka 2006 hadi 2026 unahakikisha maji yanamfikia kila mwananchi kama ilivyo kwenye dira yetu ya maendeleo,” amesema Zena.

Related Posts