Chikola, Makambo wanyatia rekodi Tabora United

NYOTA wa Tabora United, Offen Chikola amebakiza bao moja ili kuandika rekodi ya mfungaji bora tangu ilipopanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2022-2023 kutokana na kiwango bora anachoonyesha.

Chikola aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Geita Gold iliyoshuka daraja amefunga mabao saba katika Ligi Kuu Bara, ikiwa ni idadi sawa na aliyekuwa mfungaji bora wa kikosi hicho msimu uliopita raia wa Ghana, Eric Okutu.

Okutu aliyejiunga na Pamba Jiji msimu huu baada ya kuachana na Tabora aliyojiunga nayo 2023-2024 akitoka Hearts of Lions ya Ghana akiwa na Tabora United aliifungia pia mabao saba katika ligi.

Rekodi hiyo tayari imefikiwa na Chikola na huenda akaivunja kutokana na kiwango bora anachokionyesha, huku kikosi hicho kilichopo nafasi ya tano na pointi 37 kikiwa kimesaliwa na michezo saba kumaliza msimu.

Mbali na Chikola, nyota mwingine anayeweza kuvunja rekodi hiyo ni mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Heritier Makambo kutokana na kiwango kizuri anachoonyesha tangu ajiunge msimu huu.

Makambo aliyejiunga na timu hiyo akitokea Al Murooj ya Libya tayari amefunga mabao matano ya Ligi Kuu Bara na kuasisti manne, jambo linalomuweka kwenye nafasi nzuri pia ya kuifikia au kuivunja rekodi hiyo.

Mwingine aliyekuwa na nafasi nzuri ya kuifikia au kuivunja japo ni majeruhi ni mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Yacouba Songne aliyehusika katika mabao saba akifunga manne na kuasisti matatu.

Yacouba aliyejiunga na Tabora akitokea AS Arta/Solar7 ya Djibouti alikuwa katika kiwango bora ingawa majeraha ya goti aliyoyapata katika mchezo dhidi ya KMC walioshinda mabao 2-0, Novemba 29, mwaka jana yalitibua ndoto zake.

Kwa sasa nyota huyo amefanyiwa upasuaji wa goti huko Morocco na anaendelea na matibabu vizuri, ilhali taarifa za awali huenda akakosekana kwa msimu mzima ingawa kama atarejea kwa wakati anaweza kuifikia au kuivunja rekodi.

Akizungumzia suala la kukaribia kuvunja rekodi hiyo, Chikola alisema litakuwa jambo jema japo kitu kikubwa anachozingatia ni timu kwanza kufanya vizuri kwa kushirikiana na wenzake, ili wamalize nafasi nne za juu kwa msimu huu.

“Hakuna mchezaji asiyependa kuandika rekodi yake binafsi maishani… ingawa kama ambavyo nimesema mwanzoni malengo yangu ni kuona tunafanya vizuri mwenyewe,” alisema.

Related Posts