Dodoma. Serikali ya Tanzania kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imetenga Sh6.3 bilioni kwa ajili ya miradi ya utafiti wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku Sh600 milioni zikiwa zimetumika katika miradi ya usalama wa chakula.
Miradi hiyo inahusisha udhibiti wa magonjwa ya mazao, uboreshaji wa uhifadhi wa chakula, na ubunifu wa vyakula vyenye virutubishi vya hali ya juu.
Aidha, Serikali kupitia Costech imedhamini zaidi ya tafiti 50 katika sekta mbalimbali za elimu, kilimo, afya, na mazingira, huku vituo zaidi ya 111 vya ubunifu vikiboreshwa.
Tafiti hizo zimezaa suluhisho za kisayansi ambazo zimekuwa msaada kwa jamii na kuboresha maisha ya Watanzania.
Hayo yamesemwa leo, Jumatatu Machi 17, 2025, na Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya tume hiyo katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Serikali ya awamu ya sita Jijini Dodoma.
Dk Nungu amesema jumla ya kampuni 70 zimeanzishwa, na zaidi ya wabunifu wamewezeshwa na serikali ili kutekeleza miradi mbalimbali ya ubunifu.
Dira ya Serikali: Uwekezaji wa kisayansi
Katika kipindi cha miaka minne, Tanzania imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya sayansi, teknolojia, na ubunifu.
Serikali imewekeza Sh25.7 bilioni kupitia Costech, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha misingi ya maendeleo ya kisayansi na teknolojia.
Dk Nungu amesema uwekezaji huu ni ishara ya dhati ya dhamira ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya sayansi na teknolojia, na katika kutengeneza taifa lenye maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia tafiti na ubunifu.
“Hatua hii sio tu inaimarisha msingi wa maendeleo ya kisayansi, bali pia imethibitisha dhamira ya Serikali kujenga Taifa linalowekeza katika kuibua teknolojia, likiongozwa na tafiti na ubunifu,” amesema Dk Nungu.
Ushirikiano wa kimataifa katika utafiti
Costech pia imefanikiwa kupata Sh5.65 bilioni kutoka kwa washirika wa kimataifa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya utafiti wa pamoja kati ya watafiti wa Tanzania na wenzao kutoka nchi rafiki.
Uwekezaji huu umeiweka Tanzania katika nafasi ya ushindani wa kimataifa katika nyanja ya sayansi na teknolojia, na kuthibitisha kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameleta mapinduzi katika sekta hii.
“Uwekezaji huu ni wa kimkakati na unaonyesha uongozi wa Rais Samia una maono makubwa kwa Taifa,” amesema Dk Nungu.
Costech pia ina mpango wa kuwafikia wabunifu wadogo ili kuwasaidia kukuza na kuboresha bunifu zao.
Dk Nungu amesema kuwa Costech imekuwa ikifanya kazi ya kutoa maelekezo na ushauri kwa wabunifu wa ndani ili kuhakikisha ubunifu wao hauleti madhara kwa jamii.
Amesema Serikali inatambua na kuthamini ubunifu wa vijana na inajitahidi kuendeleza bunifu hizi kwa manufaa ya wananchi.
“Hakuna ubunifu unaozuiwa, bali tunahakikisha kuwa unaleta manufaa na hauleti madhara kwa watu. Kwa mfano, kama kijana amebuni helikopta, tunajiridhisha kuwa haileti hatari kabla ya kuruhusu matumizi yake,” amesema Dk Nungu.