DC ataka uwanja wa ndege Sumbawanga ujengwe usiku na mchana

Rukwa. Mkandarasi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga ameongezewa muda wa miezi mitatu kukamilisha ujenzi kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi huo.Awali, ujenzi wa uwanja huu ulitarajiwa kukamilika na kukabidhiwa kwa Serikali ifikapo Machi 13, 2025. Hata hivyo, kutokana na kucheleweshwa kwa malipo, ufinyu wa rasilimali, na baadhi ya vikwazo vya kiufundi, ujenzi umefikia asilimia 60 hadi sasa.Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Ally Chirukile, alieleza kuwa baada ya kutembelea eneo la mradi na kufanya ukaguzi, ilibainika kuwa kazi ya ujenzi ilikosa kasi ya kutosha, na hivyo, ni muhimu kuhakikisha kwamba mkandarasi anafanya kazi kwa bidii ili mradi huu ukamilike kwa wakati.

Mkuu wa Wilaya wakati akiingia kwenye jengo la abiria nakujionea hatua iliyofikiwa.

Aliagiza mkandarasi kufanya kazi mchana na usiku ili kuhakikisha kuwa uwanja unakamilika kwa wakati na kupunguza ucheleweshaji zaidi.Nyakia amesema hayo leo March 17, 2025 alipokwenda kukagua uwanja huo akiwa na Kamati ya Usalama ya Wilaya na amesisitiza kuwa kazi za ukarabati zinapaswa kuendelea usiku na mchana ili kuhakikisha uwanja huo unakamilika ndani ya muda.Amesema mkandarasi ameongezwa muda hadi Juni 13, 2025 na kuongeza kuwa kukamilika kwa uwanja huo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa malengo ya Serikali ya kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga nchini. “Namtaka mkandarasi afanye kazi mchana na usiku ili kuhakikisha anakwenda sambamba na makubaliano ya mkataba aliousaini na hakikisha unamaliza kwa wakati,“ amefafanu Nyakia.

Kwa upande mwingine, mbunge wa Jimbo la Sumbawanga, Aesh Hirary, amesema  kuwa uwanja wa ndege ukikamilika utachochea maendeleo ya kiuchumi mkoani Rukwa, kuongeza fursa za ajira, na kuvutia wawekezaji, na hivyo kuwa nyenzo muhimu kwa ukuaji wa biashara na uchumi wa mkoa.Amesema uwanja utarahisisha usafiri wa anga, kuongeza idadi ya abiria na kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara, hivyo kupanua wigo wa biashara na masoko ya ndani na kimataifa.“Kukamilika kwa uwanja kutafungua milango ya uwekezaji na kusaidia wafanyabiashara kufanya biashara ndani na nje ya nchi,” amesema Aesh.Amesisitiza kuwa uwanja huo utakuwa nyenzo muhimu katika maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Rukwa, Galasiano Tobagoze, amesema kuwa mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Sumbawanga unagharimu zaidi ya Sh60 bilioni.Amefafanua kuwa ujenzi wa uwanja umefikia asilimia 60, huku ujenzi wa jengo la abiria na tabaka la juu (BBB) ukiwa umefikia asilimia 46.Wakazi wa Mtaa wa Katusa, Kata ya Sumbawanga, wakiwemo Maria Chambala, wamesema kuwa kukamilika kwa uwanja kutaleta mabadiliko makubwa kiuchumi.

Chambala amesema kuwa mikoa mingi nchini imefaidika kibiashara kutokana na uwepo wa viwanja vya ndege, na Rukwa pia itafaidika kwa ufunguzi wa fursa za ajira na biashara.“Mikoa mingi hapa nchini imefunguka kibiashara kutokana na kuwa na viwanja vya ndege, na sisi Rukwa tukiwa na uwanja wetu, tunatarajia mabadiliko makubwa ya kiuchumi,” amesema Chambala.

Related Posts