Kamati ya Bunge yaingilia kati matengenezo MV Magogoni

Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeielekeza Serikali kutoa fedha zilizoidhinishwa na bunge katika bajeti ya mwaka uliopita, ili kukamilisha malipo ya matengenezo ya kivuko cha MV Magogoni kilichopo nchini Kenya.

Kivuko hicho, kilipelekwa kwenye matengenezo makubwa Mombasa nchini Kenya, Februari 2023 na iliahidiwa kingekamilika Agosti mwaka huo, lakini ni mwaka wa pili sasa bado hakijakamilika.

Hata hivyo, katika ripoti yake maalumu baada ya uchunguzi wa miezi mitatu, gazeti hili liliwahi kuripoti, licha ya kivuko hicho kupelekwa kwenye matengenezo, Serikali ililipa asilimia 10 pekee ya Sh7.5 bilioni ilizopaswa kumlipa mkandarasi, African Marine and General Engineering Company Ltd.

Hali hiyo, ilisababisha mkandarasi huyo asiendelee na matengenezo ya kivuko hicho, ndio sababu kimeendelea kubaki nchini humo hadi sasa.

Agizo hilo, limetolewa leo Jumatatu Machi 17, 2025 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Suleiman Kakoso, alipokua katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya miundombinu, yakiwemo maegesho ya kivuko cha magogoni, Kigamboni.

Sio kivuko hicho pekee, amesema katika miradi yote ya Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) waliyotembelea hakuna fedha iliyolipwa.

“Tumeielekeza Serikali na kuiambia Wizara ya Miundombinu ihakikishe inatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha vile vivuko ikiwemo kile kilichopelekwa nchini Kenya. Kinahitajika kikamilike  kuwasidia wananchi kwa ajili ya kupata huduma,” amesema.

Akizungumzia hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amekiri kuwepo kwa changamoto ya fedha, akifafanua utaratibu wa mawasiliano na Wizara ya Fedha unafanyika kufanikisha.

Hata hivyo, amesema tayari ujenzi wa kivuko hicho, umefikia asilimia 60 hadi sasa na kufikia Julai mwaka huu kutarudishwa nchini kuendelea kutoa huduma.

“Sisi tunaamini vivuko ni daraja linalotembea, tuatendelea kusukuma tuone fedha hizo zinapelekwa ili kivuko hicho kitengemae na kufanya kazi tena,” amesema Kasekenya.

Akiwa katika mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka awamu ya tatu (BRT3), Kakoso ameonyesha wasiwasi iwapo utakamilika ndani ya muda uliopangwa (Juni mwaka huu), akisisitiza mkandarasi aisimamiwe afanye kazi usiku na mchana.

“Kwa namna tulivyoona utekelezaji wa ujenzi katika mradi huo awamu ya tatu, imebaki miezi michache kukamilika lakini huenda isiwe hivyo. Tunaomba serikali imsimamie mkandarasi kuweza kumaliza kwa wakati,” amesema.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya (wa pili kushoto) akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, kuhusu maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara ya mwendokasi kutoka Kariakoo kwenda Gongo la Mboto walipofanya ziara katika ujenzi wa mindombinu ya mabasi yaendayo haraka awamu ya tatu (BRT3) Jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Ametaka kingo zilizowekwa kwenye barabara hizo maeneo yasiyo ya lazima ziondolewe au kupunguzwa ili kuwapa fursa wananchi kupita inapotokea dharura.

Kwa upande wa maeneo ya barabara hiyo yaliyovamiwa na wananchi wanaofanya biashara, amesema ni vema Serikali iwajengee masoko ili wasiendelee kufanya hivyo mradi utakapokamilika.

Akifafanua hayo, Kasekenya amesema watasimamia kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati, huku akisema uhamishaji na ubadilishaji wa miundombinu ya maji, umeme na Cyber ndiyo iliyochelewesha kazi.

“Mradi mpaka sasa umeshafika asilimia 80 na tunaamini hadi Juni tutakuwa asilimia 96 na vitu vitakavyokuwa vimebaki vitakuwa vichache vidogo tu,” amesema

Kuhusu wafanyabiashara kuvamia miundombini ya barabara hizo, amesema wanawasiliana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuwapangia maeneo.

Meneja wa mradi wa BRT kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Frank Mbilinyi amesema kuongezeka kwa msongamano katika maeneo ujenzi kunasababishwa na madereva kutofuata utaratibu wanaoelekezwa.

Amesema watazingatia suala la kupunguza kingo za barabara, ili kuruhusu wananchi kupita wakati wa dharura.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imefanya ziara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kubaini changamoto ya malazi kwa wanafunzi.

Kwa mujibu wa taarifa ya chuo hicho, kwa sasa kina uwezo wa kulaza wanafunzi 11,115, huku wahitaji wa huduma hiyo ni 22,000.

Kutokana na changamoto hiyo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga amesema Serikali inatarajia kuongeza ghorofa mbili kwenye jengo A na E katika hosteli za Magufuli.

Amesema mradi huo, unatarajiwa kugharimu Sh3.8 bilioni na utawezesha wanafunzi takribani 576 kupata huduma ya malazi, kati yao wasichana ni 192 na wavulana 386.

Sambamba na hosteli hizo, Kipanga amegusia ujenzi wa kituo cha wanafunzi kilichofikia asilimia tano na kinatarajiwa kukamilika Mei 12, 2026.

Jengo hilo la ghorofa nne, amesema linagharimu zaidi ya Sh9 bilioni, litasaidia wanafunzi kupata huduma muhimu ndani ya eneo moja.

“Wanafunzi takribani 1,000 watapata eneo maalumu kwa ajili ya kujisomea,” ameongeza.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko amesema ujenzi na ukamilikaji wa miradi hiyo utasaidia kuboresha maisha ya wanafunzi wa chuo hicho.

“Vyuo vingi hasa katika Mkoa wa Dar es Salaam vinakabiliwa na changamoto ya hosteli na kuwafanya wanafunzi kwenda kupanga nje,“ ameeleza.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi chuoni hapo, Tyson Kwigendaho amesema upanuzi wa hosteli hizo ni neema kwao kwani utasaidia kupunguza changamoto ya malazi katika chuo hicho.

“Mwanafunzi anapopanga nje ya chuo pamoja na kulipa gharama kubwa katika malazi vilevile hutakiwa kulipa gharama za nauli ya kwenda na kurudi ili kufika chuoni kuhudhuria vipindi,” amesema.

Katika Mkoa Njombe, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kuwalipa fidia wananchi waliotoa maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa miradi ya Ruhuji na Rumakali.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk David Mathayo amesema; “tunaiomba na kuishauri Serikali iweze kutafuta fedha ili iweze kulipa fidia kwa wananchi ambao wanaathiriwa na maeneo hayo kusudi wananchi hao waendelee na shughuli zingine lakini na Serikali iweze kutekeleza miradi hiyo vizuri.”

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema wizara hiyo ina miradi mingi inayoitekeleza na inayohitaji fidia Serikali imekuwa ikilipa.

“Kwa ujumla Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wetu wanaendelea kupata umeme wa uhakika. Kwa Mkoa wa Njombe karibu vijiji vyote vimefikiwa na nishati ya umeme bado vijiji tisa ambavyo changamoto zake zitatatuliwa,” amesema.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania, Renata Ndege amesema miradi ya umeme ya Rumakali na Ruhuji inahitaji uwekezaji wa Sh4 trilioni.

“Waathirika wa miradi hiyo jumla wanatakiwa kulipwa Sh63 bilioni kwa hiyo utaona ni fedha ambayo inahitajika ili kuhakikisha miradi hii inaanza,” amesema Ndege.

Related Posts