Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu leo Jumatatu Machi 17, 2025 imefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara za Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Tatu (BRT 3) na kueleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huku ikitoa wito wa usimamizi wa karibu ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Selemani Kakoso, amesema serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika mradi huu ili kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam. Amesema baadhi ya barabara tayari zimekamilika, huku nyingine zikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi huku akisisitiza kuwa serikali inapaswa kuhakikisha mkandarasi anafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi kwa mujibu wa mkataba.
Pamoja na hilo, Kamati imependekeza maboresho kwenye miundombinu ya mradi, ikiwemo kupunguza baadhi ya kingo zisizo za lazima barabarani ili kutoa fursa kwa magari yanayopata dharura. Vilevile, Kamati imetoa wito kwa serikali kuwatafutia wafanyabiashara wanaovamia maeneo ya mradi sehemu mbadala za kufanyia shughuli zao ili kuepusha ajali na ucheleweshaji wa ujenzi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema mradi wa BRT 3 umefikia asilimia 81 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni mwaka huu.
Amesema tofauti na awamu zilizopita, BRT 3 imejengwa kwa kiwango cha juu zaidi na itakuwa mojawapo ya barabara bora jijini Dar es Salaam.
“Tuna hakika itakapokamilika, barabara hii itakuwa na njia sita – mbili za kwenda, mbili za kurudi na njia maalum za BRT katikati. Serikali imeshalipa takribani shilingi bilioni 136 kwa ajili ya mradi huu na hakuna changamoto ya malipo kwa mkandarasi, hivyo tunatarajia kukamilika kwa wakati,” alisema Mhandisi Kasekenya.
Aidha, ameonya juu ya uvamizi wa maeneo ya mradi kwa shughuli za biashara, hususan maeneo ya Buguruni na Gongolamboto, akisisitiza kuwa hali hiyo inachelewesha ujenzi na kuhatarisha usalama wa wananchi.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Mradi wa BRT, Mhandisi Frank Mbilinyi, amewataka madereva kuheshimu alama za barabarani na kufuata maelekezo ya mkandarasi ili kuepusha msongamano na kurahisisha kazi za ujenzi.