Kamati yaishauri Serikali iwafidie waliotoa ardhi kuwekeza miradi ya umeme Njombe

Njombe. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kuwalipa fidia wananchi waliotoa  maeneo yao  kwa ajili ya uwekezaji wa miradi mikubwa  miwili ya umeme ya Ruhudji na Rumakali, iliyopo Mkoa wa  Njombe.

Ushari huo umetolewa leo Machi 17, 2025 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dk Mathayo David  wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.

Amesema maeneo ambayo wananchi wametoa endapo watawekeza kwa kuweka mitambo ya umeme itaweza kuzalisha zaidi ya megawati 500 za umeme.

“Tunaiomba na kuishauri Serikali iweze kutafuta fedha ili iweze kulipa fidia kwa wananchi ambao wanaathiriwa na maeneo hayo kusudi wananchi hao waendelee na shughuli zingine lakini na Serikali iweze kutekeleza miradi hiyo vizuri,” amesema Mathayo.

Ameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuweza kupeleka umeme katika vijiji na vitongoji na maeneo mengine ambayo umeme umefikiwa kwa asilimia 100.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema wizara hiyo ina miradi mingi ambayo inaitekeleza hivyo miradi ambayo inahitaji fidia Serikali imekuwa ikilipa fidia kwa wananchi.

Amesema kwa miradi ya Ruhudji na Rumakali, Serikali imejidhatiti kuhakikisha  inawalipa wananchi fidia ili utekelezaji wa miradi hiyo iweze kwenda vizuri.

“Kwa ujumla Serikali ya awamu ya sita imejipanga kuhakikisha wananchi wetu wanaendelea kupata umeme wa uhakika ambapo kwa Mkoa wa Njombe karibu vijiji vyote vimefikiwa na nishati ya umeme bado vijiji tisa ambavyo changamoto zake zitatatuliwa,” amesema Kapinga.

Mkuu wa Wilaya  ya Njombe, Juma Sweda ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema matumizi ya nishati mkoani hapa yamekuwa makubwa kutokana na kuwepo kwa zao la parachichi ambalo linahitaji maji ya kutosha.

“Umwagiliaji unahitaji umeme ndiyo maana sasa tunataka kupeleka umeme kwenye maeneo ya uzalishaji zaidi ili tuweze kuzalisha parachichi kwa wingi na kuuza nje ya nchi,” amesema  Sweda.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Uwekezaji, Mipango na Utafiti wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Renata Ndege amesema miradi ya kufua umeme ya Ruhudji na Rumakali kwa ujumla inahitaji uwekezaji wa Sh4 trilioni.

“Waathirika wa miradi hiyo jumla wanatakiwa kulipwa Sh63 bilioni kwa hiyo utaona ni fedha ambayo inahitajika ili kuhakikisha miradi hii inaanza,” amesema Ndege.

Mhandisi Jones Olotu ambaye ni Mkurugenzi wa Umeme Vijijini wa REA, amesema Mkoa wa Njombe una jumla ya vitongoji 1,833 ambapo mpaka kufikia sasa jumla ya vitongoji 1,154 tayari vimefikiwa na umeme.

“Vitongoji 679 havijafikiwa na umeme, lakini vipo katika mpango wa REA katika kufikishiwa umeme,” amesema Olotu.

Related Posts