Kanda ya Ziwa, Kilimanjaro wamkumbuka JPM kwa misimamo, nidhamu ya kazi

Nyanza/Kilimanjaro. Wakati leo Rais wa awamu ya tano, Dk John magufuli ametimiza miaka minne tangu afariki dunia Machi 17, 2021, baadhi ya wananchi wamesema bado wanakumbuka misimamo yake, nidhamu kazini na utendaji wake wa kuthubutu na hasa kwenye miradi mikubwa.

Dk Magufuli, ambaye aliongoza Tanzania kuanzia Novemba 5, 2015 hadi Machi 17, 2021 alipofariki dunia, alikalia kiti cha urais kwa miaka mitano na miezi minne.

Ikiwa leo ndio kumbukumbu yake, Mwananchi alifanya mahojiano na baadhi ya wananchi katika ya Kanda ya Ziwa hasa mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga na Kilimanjaro ambao wameelezea wanavyo mkumbuka kwa namna alivyoleta mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kiutawala.

Pia, walikiri kwamba misimamo yake, nidhamu ya kazi, na utendaji wake ni miongoni mwa mambo wanayokumbuka.

Michael John, mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu, amesema Hayati Magufuli alikuwa kiongozi aliyesimamia kwa ukali suala la nidhamu kazini, hasa kwa watumishi wa umma, na kupambana na uzembe na ubadhirifu katika utumishi wa umma.

“Hayati Magufuli alisisitiza sana suala la uwajibikaji. Aliweka msisitizo katika kupambana na watumishi hewa na kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika kwa manufaa ya wananchi.

“Alifanya hivyo kwa hatua za haraka na kali kwa wale waliokuwa wanashindwa kutekeleza majukumu yao,” amesema John.

Diwani wa kata ya Buchambi, Slivester Mipawa kutoka Maswa, Mkoa wa Simiyu, amesema kwamba alikumbuka mapambano ya Magufuli dhidi ya ufisadi na mikataba isiyokuwa na manufaa kwa taifa, hasa katika sekta ya madini.

Amesema Magufuli alifanya majadiliano ya kimkakati na makampuni ya madini ili taifa lipate mapato stahiki kutokana na rasilimali zake.

“Magufuli alifuta mikataba mingi isiyokuwa na faida kwa taifa, hasa kwenye sekta ya madini. Hii ilisaidia kuongeza mapato kwa Serikali na kufanikisha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo,” amesema Mipawa.

Miradi mikubwa ya kiuchumi

Wakazi wa Shinyanga walikumbuka jinsi utawala wa Hayati Magufuli ulivyochangia maendeleo makubwa, hususan katika sekta ya miundombinu. Everist Kabalo, fundi cherehani ambaye anaishi Shinyanga mjini, amesema Magufuli alikua akifanya ziara za mara kwa mara kwenye mikoa ya mbali, akikusanya maoni na kutoa maamuzi haraka kwa masilahi ya wananchi.

“Kama fundi cherehani, ni wazi kuwa miradi mikubwa ya miundombinu iliyoanzishwa na Hayati Magufuli, kama vile ujenzi wa hospitali na barabara, iliboresha huduma za kijamii na kiuchumi. Kila wakati alifanya maamuzi kwa haraka na kutatua kero za wananchi,” amesema Kabalo.

Joram Isack, mkazi wa Nyakato jijini Mwanza, amesisitiza kwamba chini ya utawala wa Magufuli, taifa lilijivunia miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi, na ujenzi wa meli ya MV Mwanza.

Isack aliongeza kuwa miradi hiyo imesaidia sana katika kukuza uchumi na kuboresha usafiri nchini.

“Miradi ya Magufuli kama vile SGR na daraja la Kigongo-Busisi ni baadhi ya mambo ambayo tunaweza kujivunia leo hii. Vitu hivi vimegusa maisha ya Watanzania wengi,” amesema Isack.

Kwa upande mwingine, Sikitu Marwa, mkazi wa Kirumba wilayani Ilemela, amesema utawala wa Hayati Magufuli ulionyesha dhahiri umuhimu wa kuwahudumia wananchi kwa haraka na bila ubaguzi.

Alikumbuka jinsi alivyokuwa akifanya ziara za kushtukiza katika hospitali, vituo vya afya, na ofisi za serikali, kuhakikisha kuwa huduma zinatolewa kwa wakati na bila ucheleweshaji.

“Huduma za afya ziliboreshwa sana kipindi cha utawala wa Magufuli. Watumishi wa umma walijua kuwa walikuwa chini ya uangalizi mkali, hivyo walifanya kazi kwa bidii,” alisema Marwa.

Ester Masue, mkazi wa Moshi, Kilimanjaro, alikumbuka jinsi watumishi wa umma walivyokuwa wakifanya kazi kwa nidhamu na ufanisi, wakijali masilahi ya wananchi.

Amesema kwamba Magufuli alisisitiza viongozi wa umma, lazima wahudumie wananchi bila kujali cheo wala hadhi zao.

“Magufuli alikaza sana suala la nidhamu kazini. Watumishi walijua kuwa watapambana na utendaji usioridhisha, hivyo walijitahidi kufanya kazi kwa bidii,” amesema Masue.

Uongozi wa Magufuli ulivyovuma

Wakati utawala wa Magufuli ulivyovuma Kanda ya Ziwa, mikoa kama Mwanza na Shinyanga ilionekana kuwa na mafanikio makubwa kutokana na miradi mikubwa aliyoanzisha.

Tatu John, mkazi wa Mbuyuni mjini Shinyanga, amesema Magufuli alijenga miundombinu muhimu, kama vile Hospitali ya Rufaa ya Shinyanga, uwanja wa ndege wa kisasa wa Ibadakuri, na barabara zilizoboresha usafiri mkoani.

“Magufuli alijenga miundombinu muhimu, na hivyo kuleta mabadiliko makubwa. Tunaona matokeo ya kazi yake hadi leo,” alisema John.

Kwa upande wa Kilimanjaro, Happyness Mrungu, mfanyabiashara mjini Moshi, amesema kwamba alikumbuka jinsi Magufuli alivyokuwa miongoni mwa viongozi waliojizatiti kutatua matatizo ya wanyonge.

Amesema kwamba alijali masilahi ya wananchi wote bila kujali hadhi zao, na kwa kufanya hivyo, alibadilisha picha ya uongozi nchini.

“Namkumbuka Magufuli kwa namna alivyokuwa akifanya kazi kwa bidii kwa masilahi ya watu wa kawaida, wanyonge. Alikuwa mtetezi wa wananchi na alifanya kazi kwa ufanisi mkubwa,” amesema Mrungu.

Mabadiliko ya huduma za Serikali

Saidi Athumani, mkazi wa Sanya Juu Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro amesema wakati wa utawala wa Magufuli, huduma za Serikali zilikuwa bora na za haraka.

Amesema kila ofisi ya Serikali ilikuwa ikifanya kazi kwa kasi na wananchi walihudumiwa bila vikwazo.

Hata hivyo, amesema kuwa hali sasa imebadilika na wananchi wanapata huduma kwa shida, kinyume na wakati wa Rais Magufuli.

“Wakati wa Magufuli, tulikuwa tunapata huduma kwa haraka katika hospitali, vituo vya polisi, na halmashauri. Lakini, sasa, huduma ni za polepole na hakuna mtu anayeuliza kama umehudumiwa,” alisema Athumani.

Habari hii imeandikwa na Samwel Mwanga (Simiyu), Hellen Mdinda (Shinyanga), Damian Masyenene (Mwanza) Yese Tunuka na Bahati Chume

Related Posts