KATIBU TAWALA UBUNGO: MALALAMIKO YA KODI KWA SASA YAMEPUNGUA

Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, Bw. Hassan Mkwawa amesema kuwa, kwa sasa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya juhudi kubwa za kutatua changamoto nyingi za Walipakodi jambo ambalo limepelekea kupungua kwa malalamiko ya kodi.

Bw. Mkwawa ameyasema hayo leo 17 Machi, 2025 katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo ambapo alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo wakati maafisa wa TRA walipomtembelea ofisi kwake kwa lengo la utambulisho kabla ya kuanza Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi ya mlango kwa mlango wilayani hapo.

Amesema kuwa, zoezi la elimu kwa mlipakodi linalofanywa na TRA linasaidia kuondoa kero na malalamiko kwa wafanyabiashara jambo ambalo linatasaidia kuongezeka kwa makusanyo ya mapato kwa ajili ya maendeleo mbalimbali nchini.

“Wakati mwingine tunaweza tukajikuta tunakaa ofisini huku wafanyabiashara hawajui namna ya kutatua kero zao za kikodi, hivyo zoezi hili la kuwatembelea katika maeneo yao ya biashara linawasaidia walipakodi kutatua kero zao na kuwafanya walipe kodi zao kwa hiari”, alisema Bw. Mkwawa.

Aidha, amewataka wafanyabiashara wilayani hapo kuhakikisha kwamba wanazingatia sheria za kodi ikiwemo kulipa kodi zao stahiki kwa wakati pia kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanatoa risiti halali za kodi za kielektroniki (EFD) na wanunuzi wanadai risiti hizo kila wanapofanya manunuzi ama kupata huduma mbalimbali.

Kwa upande wake Meneja wa TRA Mkoa wa Kodi Kinondoni, Bw. Azizi Rajab amesema kuwa, lengo la zoezi la elimu kwa mlipakodi la mlango kwa mlango wilayani hapo ni kuwakumbusha walipakodi wote kwenda kufanya makadirio ya kodi kabla au mnamo tarehe 31 Machi, 2025 pia kusikiliza kero na kupokea maoni mbalimbali yanayohusu kodi kwa lengo ya kuboresha huduma ili serikali iweze kukusanya kodi kwa urahisi pasipo kumuonea mlipakodi.

“Leo tupo wilayani hapo kwa dhumuni kubwa la kuwakumbusha walipakodi wote kwenda kufanya makadirio kwa mwaka huu wa 2025 lakini tumekuja kusikiliza kero na changamoto za walipakodi wetu ili tuzitatue nao waweze kulipakodi zao stahiki na kwa wakati”, alisema Bw. Rajab.

Kwa upande wao wafanyabiashara wa eneo la Mbezi Luis hususan katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Magufuli wamepongeza zoezi la utoaji elimu kwa mlipakodi na kuomba TRA iendelee kuwatembelea mara kwa mara kwa sababu lina umuhimu kwao na wako tayari kutoa ushirikiano kwa TRA wakati wowote kutokana na ushirikiano mzuri uliopo sasa baina ya TRA na Wafanyabiashara.

Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi inalenga kuwapa elimu, kusikiliza kero na kupokea maoni mbalimbali yanayohusu kodi kutoka kwa walipakodi nchini ili waweze kulipakodi zao stahiki na kwa wakati ambapo kwa sasa TRA inafanya zoezi hilo katika Mikoa ya Kikodi ya Kinondoni na Pwani kuanzia tarehe 17 hadi 30 Machi, 2025. 

Katibu
Tawala wa Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, Bw. Hassan Mkwawa akiongea na
Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) leo 17 Machi, 2025 katika ofisi ya
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo wakati walipofika ofisini hapo kwa ajili ya
utambulisho na kuanza kampeni ya utoaji elimu ya kodi ya mlango kwa mlango kwa
walipakodi wa eneo la Mbezi Luis jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Maafisa wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) wakipita katika maduka mbalimbali katika Stendi Kuu ya
Mabasi ya Magufuli iliyopo Mbezi Luis jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwapa
elimu ya kodi, kusikiliza kero na kupokea maoni ya Walipakodi wa Wilaya ya
Ubungo leo 17 Machi, 2025
wakati wa
kampeni ya utoaji elimu ya kodi ya mlango kwa mlango
wilayani hapo.

Meneja
wa Elimu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), CPA Paul Walalaze akiwapa elimu
ya kodi Maafisa Usafirishaji maarufu kama Madereva Bajaji wa Stendi Kuu ya
Mabasi ya Magufuli leo 17 Machi, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kampeni ya
utoaji elimu ya kodi ya mlango kwa mlango kwa walipakodi wa eneo la Mbezi Luis
jijini Dar es Salaam.

Related Posts