Kenya yajitosa sakata la raia wake kunyongwa Vietnam leo

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki saa chache ili adhabu ya kunyongwa hadi kufa inayomkabili Mkenya, Margaret Nduta Macharia (37) aliyekamatwa mwaka 2023 nchini Vietnam na dawa za kulevya kilogramu mbili za Cocaine, Serikali ya Kenya imesema inafanya juu chini asinyongwe.

Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Nation, Margaret aliyehukumiwa Machi 6, 2025, alisema alipewa mzigo huo wa dawa za kulevya aina ya Cocain kilogram mbili na anatarajiwa kunyongwa leo saa 2.30 usiku.

Hata hivyo, tovuti ya Daily Nation ya nchini humo, imeripoti kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Korir Sing’Oei amesema kuwa: “Kesi ya Nduta ni ngumu lakini tunafanya kila linalowezekana ili kupata ahueni kwa taifa letu,” aliandika Dk Sing’oei.

Waziri huyo pia alifichua kuwa wameanza mawasiliano na Vietnam na kwamba alikuwa amezungumza na Naibu Waziri wa Vietnam, Nguyen Minh Hang kuhusu suala la Nduta.

Pia, taarifa hiyo inaeleza kuwa alifanikiwa kupita katika viwanja vitatu vya ndege bila kukamatwa, kabla ya kugundulika Vietnam. Viwanja hivyo ni; Jomo Kenyatta (Kenya), Bole (Ethiopia) na Hamad (Qatar).

Hata hivyo, Margaret akijitetea mahakamani nchini Vietnam alidai hakufahamu kama mzigo ule ulikuwa ni dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Vietnam, Margaret anatarajiwa kunyongwa leo baada chakula chake cha mwisho saa 1:30 usiku na kisha kunyongwa saa 2:30 za usiku.

Related Posts