KESI YA BONI YAI NA MALISA: Shahidi athibitisha mwili wa marehemu ulikaa mochwari polisi siku 12

Dar es Salaam. Shahidi ya pili wa upande wa mashtaka katika kesi ya jinai inayowakabili meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob maarufu Boni Yai na mwanaharakati Godlisten Malisa, ameileza Mahakama kuwa mwili wa marehemu ulikaa mochwari ya Hospitali ya Polisi siku 12 kabla ya kufanyiwa uchunguzi.

Shahidi huyo, Dk Denis Basiagile ambaye ni daktari wa Hospitali ya Jeshi la Polisi ya Kilwa Road, amekiri mwili huo kukaa hospitalini hapo siku 12 kabla ya kufanyiwa uchunguzi huo, wakati akitoa ushahidi wa msingi na wakati wa maswali ya dodoso.

Katika kesi hiyo, Boni Yai, mkazi wa Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam na Malisa, mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kutoa taarifa za uwongo mitandaoni.

Wanadaiwa kuchapisha taarifa za uwongo katika mitandao yao ya kijamii ya X (zamani Twitter) na Instagram, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015, wakilihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia.

Katika taarifa hizo wanadaiwa kulihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia akiwemo mkazi wa Dar es Salaam, Robert Mushi maarufu Babu G na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, Omari Msemo.

Pamoja na mambo mengine Jacob aliandika licha ya ndugu kutoa taarifa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam lakini kila siku polisi walikuwa wakisema halijapata taarifa wala fununu zozote na kuwataka ndugu waendelee kuwa wavumilivu wakiendelea kumtafuta.

Hata hivyo, ndugu walidokezwa na msiri mmoja akiwataka waende Hospitali ya Polisi Kilwa Road mkachungulie vyumba vya kuhifadhi maiti ambako walikwenda wakamkuta ndugu yao akiwa ameua na wahusika wa hospitali walidai kuwa mailiti ilipelekwa tangu Aprili 10, 2024 na askari wa Jeshi la Polisi.

Hivyo Boni Yai katika andiko lake alihoji:“Maiti ina siku 12 Hospitali ya Polisi Kilwa Road  haijui bila Jeshi la Polisi kujua ipo hapo? Polisi walioipeleka maiti ni wa nchi gani?

Kesi hiyo ya jinai namba 11805/2024, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu Ushindi Swallo, imeendelea leo, Jumatatu, Machi 17, 2025, ambapo shahidi huyo wa pili wa upande wa mashtaka, ametoa ushahidi wake jinsi alivyofanya uchunguzi wa mwili huo na kile alichokibaini.

Kwa mujibu wa ushahidi wake, alioutoa akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Asiath Mzamiru, Dk Basiagile ambaye ni mkazi wa  Kurasini Aprili 23, 2024, akiwa kazini aliitwa mochwari na mhudumu kufanya uchunguzi wa mwili.

Mochwari alimkuta askari Jamada akiwa na amiri ya Mahakama ya Kisutu ikielekeza kufanya uchunguzi wa mwili wa wa mtu mwenye jina la Robert Mushi, pamoja na ndugu wawili wa marehemu, John Mushi na Gunda Msele, ambao waliutambua mwili wa marehemu.

Kisha alifanya uchunguzi wa mwili mbele ya ndugu wa marehemu kwa kuuangalia kwa mwili kwa nje ambapo mwili ulionekana ulikuwa na majeraha mengi, kuanzia usoni, kifuani, mikononi na miguuni, huku sehemu nyingine zilikuwa zimebonyea.

Sehemu hizo ni pamoja na upande wa kulia wa kifua na tumbo na sehemu ya nyonga kulia.

Kisha alifungua baadhi ya sehemu za mwili kama kifua ambapo aliona mbavu ya kwanza mpaka ya tatu za kulia zilikuwa zimevunjika na ini pia lilikuwa limepasuka na kusababisha damu nyingi kumwagika kifuano na tumboni.

Nyonga pia ilikuwa imevunjika sehemu ya kichwa cha mfupa wa paja la kulia.

“Kutokana na uchunguzi huo nilibaini kuwa kilichomuu marehemu ni kupoteza damu nyingi kutokana na majeraha sehemu mbalimbali za mwili,” amesema Dk Basiagile na kuongeza:

“Kwa namna yake majeraha yalivyokuwa inaonekana yalitokana na ajali ya barabarani.

Amesema baada ya kukamilisha uchunguzi huo aliandika ripoti ya uchunguzi na kumkabidhi yule askari.

Shahidi ameiomba mahakama na imekubali kupokea ripoti hiyo ya uchunguzi kuwa kielelezo cha pili cha upande wa mashtaka, baada ya wakili wa utetezi, Peter Kibatala kuieleza Mahakama hana pingamizi nayo.

Baada ya ripoti hiyo kupokewa na kuwa kielelezo cha mahakama, akiongozwa na wakili Mzamiru, shahidi huyo ameisoma ripoti hiyo na kuhitimisha kuwa mpaka siku aliyofanya uchunguzi kifo hicho kilikuwa na siku kama 12.

Hata hivyo wakati wa maswali ya dodoso, akiohojiwa na wakili na wakili wa utetezi, Peter Kibatala, shahidi huyo amekiri kuwa aina ya majeraha hayo pia yanawezoa kusababishwa na kupigwa na na pia kupigwa na kitu kizito chenye ubaba.

Wakili Kibatala: Mimekusikia ukisema baada ya kufanya uchunguzi yale majeraha yalikuwa ni ya ajali ya barababrani.

Wakili: Ulimwambia hakimu kuwa ulikuwa umeshachunguza miwili mingapi ya ajali za barabarani ili kujua uzoefu wako kutambua majereha ya ajali za barabarani?

Wakili: Tunapima dhidi ya taarifa gani kwamba mwili huo ulikuwa na majeraha ya ajali kama wewe hujatwambia kuwa ulishachunguza miwili mingi kwani unafahamu kesi hii imetokana na tuhuma dhidi ya Jeshi la Polisi ambalo ni mwajiri wako?

Wakili: Unafahamu kuwa mtu akiwa na mgongano wa maslahi (kwa kuwa ni mwajiriwa wa Polisi wanaotuhumiwa) inapunguza thamani ya kile anachokisema?

Shahidi: Hilo inaweza kuwa.

Wakili: Katika hii karatasi (ripoti ya uchunguzi wa mwili) kuna majina yako wapi?

Shahidi: Hapo haijaandikwa.

Wakili: Katika ushahidi wako wote ulimwambia hakimu kuwa uliwahi kumuuliza Jamadal au kina Mushi (ndugu wa marehemu) kujua sababu ya majereha hayo ni nini?

Wakili: Uliwahi kufahamu kuwa mwili wa huyo mtu ulikuwa wapi kwa siku zote hizo 12?

Shahidi: Nilijua baadaye kuwa ililetwa kama mwili usiojulikana.

Wakili: Ni sahihi kwamba mwili huo ulikuwa umekaa hapo hospitalini kwa siku 12 kabla ya kufanyiwa uchunguzi?

Wakili: Umetoa mahakamani hapa nyaraka halisi ikiwemo ya amri ya Mahakama hii inayoonesha hadidu rejea kufanya uchunguzi wa mwili huo?

Wakili: Kama hujaitoa tunajuaje kwamba Mahakama hii ilitoa amri hii kuchunguza mwili ambao umekaa hospitalini siku 12?

Shahidi: Mahakama yenyewe itajua maana ndio iliyotoa amri.

Wakili: Kama hujaitoa hivyo nyaraka (amri ya mahakama kufanya uchunguzi huo) tutaaminije kuwa karatasi hii (ripoti ya uchunguzi) hamkuitunga ili kuendana na kesi hii?

Shahidi: Hapana hatukuitunga ni ya kweli.

Kesi hiyo itaendelea kesho Jumanne Machi 18, 2025 kwa shahidi mwingine wa upande wa mashtaka.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani hapo kwa mara ya kwanza Mei 6, 2024 na kusomewa jumla ya mashtaka matatu, mawili kati ya hayo yanamkabili Jacob pekee yake, huku Malisa akikabiliwa na shtaka moja.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 19 na Aprili 22, 2024 jijini Dar es Salaam.

Related Posts