WACHEZAJI wakongwe wa Tanzania Prisons waliokuwa wamepangiwa majukumu mengine nje ya timu, Jumanne Elfadhili na Salum Kimenya wamerejeshwa na wameshajiunga na wenzao kambini ili kuongeza nguvu katika vita ya kuepuka kushuka Ligi Kuu.
Nyota hao sambamba na Jeremiah Juma walidaiwa kuondolewa dirisha dogo kabla ya mambo kwenda mrama na kocha kuwataka, lakini ni Jeremiah aliyekuwa amekubali kurudi huku wawili hao wakitaka waendelee na majukumu mapya.
Hata hivyo, inaelezwa baada ya majadiliano wamekubali kurudi katika kikosi hicho kinachoshika nafasi ya 15 katika msimamo kikiwa na pointi 18 baada ya mechi 23.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo iliyowahi kuwa bingwa wa Tanzania kupitia Ligi Kuu ya Muungano 1999 ni kwamba uongozi umeamua kuwarejesha kikosini ili kusaidiana na wenzao kuiokoa timu hiyo isishuke.
Katika mechi 23 ilizocheza Prisons imeshinda nne na kutoka sare sita huku ikipoteza 13 na kuwa katika hatarii ya kushuka kwani imepishana pointi mbili na KenGold iliyopo mkiani ilhali ligi ikisaliwa na mechi saba kabla ya kumalizika Mei 25.
Chanzo cha kuaminika kimelidokeza Mwanaspoti kuwa timu hiyo kwa sasa imeweka kambi ya wiki moja Kiwira, Mbeya, kipindi cha mapumziko ya Ligi Kuu kupisha timu ya Taifa kucheza mechi ya kufuzu Kombe la Dunia ugenini Machi 26 dhidi ya Morocco.
“Hali ni mbaya tunapambana timu iweze kusalia Ligi Kuu. Tayari Kimenya na Elfadhili wamesharejeshwa kambini,” kilisema chanzo.
“Wachezaji hao wakongwe wana mchango mkubwa na wameipambania timu kwa muda mrefu, hivyo tunaamini kurejea kwao kutaleta mabadiliko makubwa ndani ya kikosi,.”
Alipotafutwa kocha wa timu hiyo, Amani Josiah alisema hawezi kuzungumza kitu chochote, lakini katibu wa timu hiyo, John Matei alisema ni kweli wachezaji hao wamejiunga na kambi ya siku 10.
Prisons ambayo iliwahi kunusurika kushuka daraja 2021-2022 na kuishia kujiokoa kupitia mechi za play-off, imekuwa na msimu mbaya hali iliyoufanya uongozi uachane na kocha Mbwana Makata aliyechukua nafasi ya Ahmad Ally akiyekimbilia JKT Tanzania kisha kumlchukua Josiah, lakini upepo bado haujakaa sawa.
Mbali na Kimenya na Elfadhili walioondolewa kwa majukumu mengine kabla ya kurejeshwa, lakini kuna Yona Amos, Zabona Mayombya, Ibrahim Abraham na wengine waliondoka kwenda kujiunga na timu zingine msimu huu na kuifanya Prisons iyumbe.