Dar/Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka watendaji wa ardhi nchini kubadilika kwa sababu wananchi wanawalalamikia kwa rushwa, kujilimbikizia viwanja na kugawa kiwanja kimoja kwa watu wawili.
Mbali na hilo, amewataka watumishi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), kubadilika kwa kutokuwa mvinyo uleule kwenye chupa mpya.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatatu Machi 17,2025 na wakati akizindua Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 toleo la Mwaka 2023 jijini Dodoma.
Amesema mafanikio ya sera hiyo yatategemea sana utekelezaji wake na mabadiliko ya kifikra huku akieleza kuwa watumishi waliopo katika sekta hiyo hawazungumzwi vizuri na wananchi.
Amesema watumishi wa ardhi wamekuwa hamsemwi vizuri na jamii na kuwa wanasemwa kuwa wanatoa kiwanja kimoja kwa watu zaidi ya mmoja, jambo ambalo wakati mwingine ni mazingira yanawafanya kufanya hivyo lakini wakati mwingine ni makusudi.
“Kuna kamdudu kale kanatembea tembea, kenye ari ndogo , rushwa inawafanya mfanye vitendo vya hovyo sana, niwaombe sana watumishi kwenye sekta hii kila mmoja sasa aseme na moyo wake, aseme nakwenda kubadilika na kuhudumia nchi yangu,”amesema.
Amesema kuwa mambo yanayotokea ni kubatilisha haki kuwa halali na halali kuwa batili huku akieleza kuwa Mungu hapendi suala hilo.
“Mwenye haki unambatilisha lakini asiye haki unamhalalisha, hili Mungu halipendi hata kidogo, kwahiyo niwaombe sana watumishi sekta ya ardhi badilikeni. Mnasemwa kwa ucheleweshaji hati makusudi leo (jana) nimezindua mfumo wa utoaji hati ambao unaenda kuharakisha utoaji hati, kwahiyo hii linakwenda kuondoshwa,”amesema.
Amesema watumishi hao wamekuwa wakisemwa kwa kujilimbikizia viwanja kwenye miradi mbalimbali na kwamba kama wanapima viwanja 3,000, vyao vinakuwa 300 hadi 400.
“Vinawekwa pembeni huko na wenye haki ya kupata maeneo yale hata kama ni mashamba mmechukua ni ya watu mnasema hapa ardhi yote ni mali ya serikali shamba lako hili utapata viwanja viwili hivi hapa vilivyobaki huku vyote wanapewa wengine. Kumbe mmejiwekea wenyewe akiba yenu,”amesema.
Rais Samia amesema hilo halikubaliki na kueleza kuwa wahusika wataumbuka kupitia mfumo wa Tehama wa E-Ardhi kwa sababu viwanja hivyo vitakuwa havina majina au vina majina bandia hayana utambulisho wa taifa hivyo vitabainika kuwa ni tupu na watapewa wananchi.
Amesema utekelezaji wa sera hiyo unapoenza ni vyema kila mmoja katika sekta ya ardhi na Tamisemi kuhakikisha wanabadilika badala ya kuwa mvinyo ule ule kwenye chupa mpya kwa sababu sera ni mpya lakini watu ni wale wale na tabia ni zile zile.
“Hatutasogea, hatutakwenda, lazima mbadilike, sera mpya na watu tuwe wapya, siyo wapya phyisically, hatuwezi kuwatoa wote tukaweka wengine lakini nyoyo zenu ziwe mpya zibadilike na mkusudie kuifanyia kazi nchi hii, hivyo kafanyeni kazi tusisubiri kubadilishwa badilikeni wenyewe,”amesema.
Kuhusu ugawaji magari 70 kwa ajili ya maafisa Ardhi, Rais Samia amewataka kutumia vizuri magari hayo waliyokabidhiwa leo (jana), kwa kwenda maeneo yenye migogoro na kutoa suluhisho.
“Gari zile zikatimike kwa matumizi kusudiwa, zikafanye kazi ya kuhudumia wananchi, zitunzwe isiwe tena bwana mkubwa ushakadhiwa wewe kazi yako kushusha sketi , kupanisha kilemba, au bibi ardhi tena umeshapewa lile gari linakuwa si lako ni la mwenza, hapana yale magari ni ya kazi hatukatai kupandisha wenza lakini ni nje ya kazi,”amesema.
Amesema kuwa ardhi ni suala linalogusa kila mtu na amani ya nchi hivyo kupungua kwa migogoro ni kuendeleza amai hiyo na kuwataka watumishi wa ardhi kufanya kazi kwa kutanguliza utu mbele ili kuwezesha utekelezaji wa sera.
“Tukapunguze migogoro ya ardhi na uhamiaji kutoka vijijini kwenda mijini, wale wenzetu nje mtu yupo kijijini nyumba yake ina kila kitu, maeneo ya biashara yamejengwa hivyo na sisi tukifanya hivyo kwa kiasi kikubwa tutapunguza mambo hayo hivyo kuchochea uchumi wa nchi,”amesema.
Mambo sita yaliyoko katika sera
Rais Samia amesema miaka 30 ya Sera hiyo imeonyesha ulazima wa kuifanyia maboresho ili kuendana na uhalisia wa sasa na lengo la jumla la sera hiyo iliyoboreshwa ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na mfumo madhubuti na usawa wa umiliki, upatikanaji na usimamizi wa matumizi ya ardhi kwa maendeleo endelevu.
Ametaja mambo yaliyomo katika sera hiyo ni kuimarisha udhamini na ulipaji wa fidia, kuimarisha uwekezaji katika uendelezaji wa ardhi, kuongeza kasi ya usajili wa ardhi, uimarishaji wa mipaka ya Tanzania na nchi jirani, usimamizi kwenye soko la ardhi nchini na kuimarisha utatuzi wa migogoro.
Akizungumzia kuhusu uimarishaji wa mipaka ya kimataifa ya Tanzania na nchi jirani, Rais Samia amesema maboresho hayo yatatoa nguvu ya kurekebisha sheria za mipaka ya Tanzania.
Amesema vilevile maboresho hayo yatawezesha kutambua fursa zinazopatikana katika uchumi wa bluu na kuwa sera hiyo imebainisha juu ya kuweka utaratibu wa kisera wa kusimamia raslimali za uchumi zilizoko katika maji kwa kupima na kumilikisha ardhi kwenye maji ili itumike kwa ufanisi na tija.
“Tumejumuisha na kuweka utaratibu wa kupima ardhi kwenye maji, kwenye hili nafikiri mnakuwa mnasikia tunabishana na huyu ziwa limesogea huku ziwa limerudi huku, mara tunabishana na huyu mto umezid huku,”amesema.
“Tunakwenda sasa kupima tunajua ni changamoto kuna diplomasia ya kutosha lazima itumike ili kuelewana na majirani na tuweze kupima na tujue Tanzania inakwenda hadi wapi na kuviepusha vizazi vyetu vijavyo ya ardhi na mipaka huko baadaye,”amesema.
Kuhusu kuimarisha usimamizi kwenye soko la ardhi hapa nchini, Rais Samia amesema kuna watu wangependa kuja Tanzania kuja kusaidia katika mradi wa makazi ambao uko chini ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lakini sekta hiyo haikuwa na sawa.
Amesema wakishaweka sera watabadilisha sheria ili waje wajenge nyumba lakini si kwa kuwamilikisha ardhi bali kwa kuwakodisha na hivyo watapunguza changamoto ya makazi.
Amesema pia kwa kufanya hivyo kutaongeza kasi ya usajili wa ardhi na kwamba licha ya hatua walizopiga katika upimaji lakini bado asilimia 75 ya ardhi nchini haijasajiliwa na kuwa hiyo imechangia upotevu wa mapato na kutokuwa na usawa kwa kuwa baadhi watu ndio wanalipa umiliki wa ardhi.
“Sasa tunataka kila kipande cha ardhi kipangwe, kipimwe na kusajiliwa kwa wale mliokuwa na vijumba vyenu ambako mabwana ardhi hawafiki mara kwa mara sasa watakwenda kupima na kusajiliwa na kila mwaka ailipie kama sheria inavyotaka,”amesema.
Kwa upande wa kuimarisha uwezo wa utatuzi wa ardhi, Rais Samia amesema wanakwenda kupitia upya mfumo wa mabaraza hayo na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa vyanzo vya migogoro ya ardhi kwa kutumia Tehama
Kuhusu kuimarisha udhamini na ulipaji wa fidia. Rais Samia amesema wamebaini upungufu katika malipo ya fidia ya ardhi na mali hali ambayo imeleta malalamiko makubwa miongoni mwa wananchi ikiwemo tathimini, ucheleweshaji wa fidia na mapunjo.
“Kupitia sera hii tutaimarisha mfuko wa fidia ya ardhi ili kurahisisha ulipaji wa fidia kwa haki kwa wakati na thamani halisi, tunapoimarisha mfuko huu ni vizuri watumishi wanaoratibu masuala ya fidia wakabadilika mmefanya vyakutosha sasa basi,”amesema.
Kwa upande wa kuimarisha uwekezaji kwenye uendelezaji wa ardhi, Rais Samia amesema sera iliyopita haikuruhusu wawekezaji kwenye miliki ardhi (Real estate) kutoka nje ya nchi kuuza nyumba zinazojengwa lakini maboresho hayo yameruhusiwa na hivyo kusaidia kuboresha sekta hiyo.
Awali, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi amesema mchakato wa kufanya marekebisho Sera hiyo ulifanyika kwa zaidi ya mara mbili mwaka 2010 na 2015 lakini hakuweza kukamilika.
Amesema Rais Samia alivyoingia madarakani alitoa maelekezo ya kupitiwa kwa sera hiyo ili kuendana na nyakati za sasa ambapo utekelezaji wake ulianza.
Amesema utekelezaji wake ulianza kwa kuwashirikisha watu mbalimbali wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wawekezaji, viongozi wa dini na kisha kwa wabunge na hatimaye kukamilika.
Kuhusu kupima na kuipanga ardhi ya Tanzania, Ndejembi amesema hadi kufika mwaka 2030, ardhi ya Tanzania itakuwa imepimwa na hivyo kuwezesha kila kipande kueleweka mmliki wake.
Aidha, Ndejembi amemkabidhi tuzo Rais Samia kwa kutambua mchango wake katika kusimamia mifumo ya usimamizi wa sekta ya ardhi Tanzania.