KESHO saa 10:00 za jioni kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam itashuhudiwa Dabi ya Wanawake kati ya Simba Queens ambao ni wenyeji wa mchezo huo ikiikaribisha Yanga Princess.
Huo ni mchezo wa 12 tangu timu hizo zilipokutana kwa mara ya kwanza mwaka 2019, Simba Queens ikionekana mbabe kwa Yanga, kwani katika mechi hizo Mnyama ameshinda tisa, sare mbili na kufungwa mara moja huku mtani wake akishinda mara moja, sare mbili na kupoteza tisa.
Ile Karikaoo Dabi ya duru la kwanza ambayo Simba ilikuwa mgeni wa mchezo huo na kufanikiwa kuondoka na pointi tatu mbele ya mtani wake kwa bao la kujifunga na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo kuondoka kifua mbele.
Lakini hivi karibuni ni kama upepo umebadilika kutokana na muendelezo mzuri wa matokeo wanayopata Yanga na kuufanya mchezo huo kuwa tofauti na watu wanavyofikiria.
Kiuhalisia sasa Yanga ipo katika wakati mzuri na imekuwa ikifanya vizuri katika mechi zake licha ya kusalia nafasi ya tatu kwenye msimamo na pointi 27, lakini Simba ndiyo bora zaidi kwani inaongoza kileleni mwa msimamo kwa pointi 34.
Katika mechi 12 zilizocheza timu hizo, Yanga imepoteza mechi mbili dhidi ya JKT na Simba, sare tatu na ushindi mechi saba huku watani wao Simba wakiwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo ikishinda 11 na sare moja.
Kutokana na mwenendo huo hasa kwa matokeo ya hivi karibuni yanafanya mchezo huo kuonekana mgumu ukiachana na rekodi za nyuma.
Mwanaspoti imekuchambulia mambo matano yanayoweza kuamua mchezo huo muhimu kwa timu zote mbili.

Kwa siku za hivi karibuni Yanga imeanza kuimarika karibu kila eneo la timu hiyo chini ya kocha Edna Lema ‘Mourinho’ ambaye mwanzoni mwa ligi hakuanza vizuri.
Baada ya kuonekana upungufu hasa kwenye eneo la kiungo cha ushambuliaji, Yanga iliingia sokoni na kusajili namba 10 mwenye ubora na pia kuimarisha eneo la ulinzi wa pembeni.
Yanga ikampa kandarasi ya miaka miwili, Aregash Kalsa aliyetokea C.B.E ya Ethiopia na kuongeza wachezaji eneo la ulinzi Protasia Mbunda, Diana Mnally na Zubeda Mgunda kutoka Gets Program na baadaye kumleta Jeaninne Mukandasyenga kuwa mbadala wa mshambuliaji, Ariet Udong ambaye alipata majeraha mwishoni mwa mzunguko wa kwanza.
Unapozungumzia wachezaji wanaoweza kuamua mechi hii, huwezi kumuacha Mukandasyenga, ambaye ni mshambuliaji hatari, akifunga mabao manne katika mechi tatu zilizopita.
Hii ni mechi ya kwanza ya dabi kwa nyota huyo raia wa Rwanda na mabeki wa Simba wanapaswa kuwa makini naye hasa anapokuwa ndani ya boksi kwani ni straika mwenye nguvu na anatumia akili kuwafanya walinzi wa timu pinzani kumfanyia makosa.
Mchezaji mwingine ambaye Simba inapaswa kuwa naye makini ni Neema Paul ambaye ndio kinara wa mabao kwa Yanga akiwa nayo 12 nyuma ya wakali wakali wawili tu, Jentrix Shikangwa aliyeweka kambani mabao 17 na kinara Stumai Abdallah wa JKT mwenye 21.
Ni winga ambaye hana kasi lakini ni mkali kwenye mipira ya kona kama hatazuiwa vilivyo huenda akaleta madhara kwa Wanamsimbazi.
Wachezaji kama Mnally, Mgunda ni miongoni mwa wachezaji waliowahi kuichezea Simba kwa muda mrefu hivyo wanaifahamu vizuri kuanzia ubora wa mnyama hadi udhaifu wake.
Ubora ambao Yanga imeuonyesha tangu mzunguko wa pili uanze unaweza kuufanya mchezo huo kuwa mgumu kutokana na ongezeko la baadhi ya nyota kikosini.

Kwa misimu takribani saba sasa tangu Simba ianze kushiriki Ligi msimu 2017 imekuwa na ubora kuanzia kwa wachezaji na benchi la ufundi chini ya msaidizi, Mussa Hassan ‘Mgosi’.
Simba ambao ni watetezi wa ligi wana wachezaji wakali kama Violeth Nickolaus, Fatuma Issa ‘Fetty Densa’, Asha Djafar na Vivian Corazone ambao ni wazoefu katika Ligi.
Nyota hao wamechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Simba iliyobeba ubingwa mara nne wa WPL ikiwafanya mashabiki wa Msimbazi waendelee kutamba na timu hiyo.
Uzoefu wa baadhi ya nyota hao unaweza kuamua mchezo huo ambao ni muhimu kwa Simba inayopigania kutetea ubingwa ili iweze kushiriki mashindano ya CECAFA kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake ambapo msimu uliopita iliishia hatua ya nusu fainali ikiondoshwa na Kenya Police kwa jumla ya mabao 3-2.
Mchezo uliopita ambapo Yanga ilikuwa mwenyeji, Simba iliondoka na ushindi wa bao 1-0 la kujifunga baada ya Corazone kutia presha katika lango la Wananchi na kumfanya beki wa Yanga, Angela Chineneri kujifunga.
Simba ina wakali wengi wa kuamua mechi. Urejeo wa Aisha Mnunka ambaye alikuwa na sakata na klabu yake ya Simba unaifanya Yanga kuingia ubaridi na nyota huyo machachari.
Msimu uliopita Simba Queens aliifunga Yanga Princess mabao manne, mawili kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza na mengine mzunguko wa pili.
Mkenya Shikangwa tangu ajiunge na Simba msimu 2022/23 ameifunga Yanga mara mbili tu lakini ni miongoni mwa nyota wa kuchungwa kwani ana uwezo wa kufunga kwa mashuti ya mbali.

Kama timu mojawapo itaondoka na ushindi kwenye mchezo huo basi itakuwa inaendelea kujiweka pazuri katika mbio za ubingwa ambazo zinaonekana kuwaniwa na timu tatu, JKT, Simba na Yanga.
Simba imeendelea kusalia kileleni na pointi 34, JKT iliyopo nafasi ya pili na pointi 32 huku Yanga ikiwa na alama 27 kwenye michezo 12 ya ligi iliyocheza timu hizo.
Endapo Simba itapoteza mchezo huo basi itampa mwanya wa kusogea kileleni JKT ambayo imetofautiana pointi mbili na mnyama ambae tangu ligi ianze haijashuka nafasi hiyo.
Vivyo hivyo, kwa Yanga kama itapoteza mchezo huo ikiwa ugenini itapoteza matumaini ya kuwania ubingwa ambao wamekuwa wakiuota tangu msimu 2018 ambao wananchi hao walianza kushiriki ligi hiyo.

Mchezo huo utaamuliwa na mbinu za makocha wawili, Yussif Basigi kwa upande wa Simba Queens na Edna Lema ‘Mourinho’ wa Yanga.
Makocha hao wote ni kama mbinu zao zinashabihiana kwani wamekuwa wakijilinda zaidi wanapokutana kwani msimu huu wamekutana mara mbili moja ya Ligi na ile ya Ngao ya Jamii.
Mourinho anapenda kutumia mfumo wa kujilinda zaidi kuliko kushambulia, lakini hivi karibuni amekuwa akibadilika kwani anafanya vyote kwa wakati mmoja anashambulia na kuzuia.
Kwa Basigi katika michezo mingine kutokana na ubora wa washambuliaji wake unamfanya ashambulie zaidi.

Rekodi zinaonyesha tangu wadada hao wakutane msimu wa 2019/20 zimekutana mara 12 katika Ligi na Simba ikishinda michezo mara tisa, kupoteza mara moja na sare mbili.
Kwa Yanga imeshinda mara moja tu msimu wa 2022/23 bao 1-0 likifungwa na Clara Luvanga ambaye kwa sasa anaitumikia Al Nassr ya Saudia, mechi tisa ikipoteza na kupata sare mbili katika michezo hiyo.
Aidha, mshambuliaji mkongwe, Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ ndiye mchezaji aliyewafunga zaidi Yanga akitupia kambani mara 10 akishikilia rekodi ya kufunga hat-trick kwenye dabi msimu 2019/20.

Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Yanga Edna Lema ‘Mourinho’ alisema; “Ni mchezo wa dabi ambao hautabiriki na mashabiki wasije na matokeo, wayapokee kwa lolote tukishinda watupongeze, tukipoteza watupe moyo, tunawaahidi waje kuona burudani lakini kama timu tumejiandaa kushinda na sitamani kama kocha kupoteza mchezo wa pili mfululizo kwenye dabi.”
Kocha wa Simba Queens, Yussif Basigi alisema; “Dabi siku zote ni mchezo unaokuwa na ugumu kwa kiasi chake, tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunaondoka na ushindi kwenye mchezo huo, hautakuwa rahisi hata kidogo.”