Kuvunjika kwa uhusiano, kujichukia kwa kukosa mwonekano mzuri ni baadhi ya mambo wanayokumbana nayo wanawake wenye vitambi, huku takwimu zikionesha kuwapo kwa idadi kubwa ya wanawake wenye hali hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Ufuatiliaji wa Kaya (NPS) wa mwaka 2020/21, asilimia 47 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wasio na mimba, wana uzito uliopitiliza likiwa ni ongezeko la asilimia 8.2 kutoka mwaka 2014/15.
Ripoti hiyo iliyotumia kipimo cha ulingano wa uzito na urefu (BMI), inaonyesha vigezo vya mtu kuwa na uzito uliopitiliza ni kuwa na BMI kuanzia 25 na zaidi ya 30.
Takwimu hizo zinaonyesha katika kila wanawake wawili nchini, mmoja ana uzito uliopitiliza kutokana na kutumia vyakula vyenye mafuta mengi.
Judith Sanga mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam amesema kitambi anachoishi nacho kwa zaidi ya miaka mitatu, kimekuwa kikwazo kwenye maisha yake
“Kitambi kwangu ni tatizo nimezunguka sana kukitoa nimeshindwa. Kilinifanya nikose mume. Nakumbuka nilikutana na mchumba mtandaoni tukawa tunawasiliana kama unavyosikia sauti yangu ni nzuri na sura ni nzuri. Yule mchumba alinitumia nauli tukaonane nilifunga safari kutoka Dar es Salaam hadi Manyara.
“Nilipofika alivyoniona akaniuliza kwani nina ujauzito. Nikamwambia hapana ni tumbo la kawaida(kitambi). Yule baba aliniambia mimi ni mzuri sana lakini kwa tumbo langu hatoweza kuwa na mimi. Alinipatia nauli ya kurudi Dar na pesa ya kunipotezea muda, niliumia sana kukosa mume kisa tumbo,”amesema.
Amesema kutokana na kitambi chake kuwa kikubwa kupita kiasi kinafanya watu wengi wadhani ana ujauzito, hivyo anakitaja kama sababu ya kutoolewa hadi sasa.
“Nimetafuta mchumba mwingine mtandaoni hajawahi kuniona mwili mzima anaona picha nusu, sasa mwezi wa sita tumepanga kuonana sijui itakuwaje. Lakini nimenunua dawa za kukitoa sasa sijui kama itasaidia,”amesema Judith.
Kwa upande wake, Catherine John amesema anashindwa kwenda na fasheni kutokana na tumbo lake kuwa kubwa
“Yani kuna mitindo mingi ya mavazi nashindwa kuvaa kabisa kitambi kinanitia aibu. Nikivaa nguo ya kubana kinaonekana. Sasa inabidi nivae nguo za kumwaga tu yaani sipo huru kabisa na mwili wangu. Hiki nilikipata baada ya kujifungua mtoto wangu wa kwanza nimehangaika lakini tumbo halijarudi,”amesema Catherine.
Oliva Atma mkazi wa Moshi, Kilimanjaro, amesema alianza kupata kitambi mara baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza.
“Baada ya kujifungua nikajikuta tumbo limekuwa tofauti na nilivyokuwa msichana. Mimi ukweli kitambi kinanitesa siwezi kuvaa nguo nikapendeza ni tofauti na zamani. Sasa hivi nikivaa sipendezi tumbo linakuja mbele. Linaninyima uhuru yaani najiona sipo sawa,”anasema
Juma Said mkazi wa Kijichi mkoani Dar es Salaam, amesema mara nyingi havutiwi na wanawake wenye kitambi.
“Kwanza mimi kinachofanya nisipende wanawake wenye kitambi nawaona hawana nidhamu kuanzia ya chakula kujua wale vipi na kutunza miili yao. Pia mara nyingi hukosa mwonekano mzuri, kama kwenye upande wa mavazi mengi wanashindwa kuvaa. Mimi napendelea zaidi wanawake wasio na kitambi na wenye mwili mdogo,”anasema.
Kwa upande wake, Frank Simon, anasema hapendelei wanawake mwenye kitambi kwani humfanya akose uhuru wa kuongozana nao.
“Kawaida mimi mwanamke mwenye kitambi sipendelei kwa sababu kitambi kinafanya apoteze mvuto, lakini hata katika tendo la ndoa ni changamoto,” amesema
Mbali na hao Rashidi Massoud anasema chaguo lake mara zote ni mwanamke mnene na mwenye kitambi.
“Mimi ukweli kabisa chaguo langu ni mwanamke mwenye kitambi kwa sababu wanajali sana na wanathamini. Upendo wao ni mkubwa tofauti na hawa wengine. Ni kweli kwenye mavazi kwao ni changamoto lakini nawapenda sana wanawake wa aina hiyo,”amesema.
Usiyoyajua kuhusu kitambi
Ofisa Lishe Manispaa ya Kinondoni, Janeth Mnzava amesema kitambi ni mkusanyiko wa mafuta mengi kwenye sehemu ya tumbo, unaosababisha kuonekana kwa tumbo kubwa na linalojitokeza.
Amesema hali hii mara nyingi hutokea kutokana na ulaji wa chakula kupita kiasi, mtindo wa maisha usiofaa au matatizo ya kimetaboliki.
“Kitambi mara nyingi husababishwa na ulaji wa vyakula vyenye kalori nyingi na virutubishi vichache, kama vile, vyakula vya wanga vilivyosindikwa kama mikate myeupe, ugali, na wali uliokobolewa,’’ amesema na kuongeza vyakula vingine kuwa ni pamoja na vyakula vyenye mafuta mengi, vyakula vya kukaanga na vyakula vya haraka (fast foods), vyakula vyenye sukari nyingi kama soda, juisi zilizosindikwa, keki, pipi, na biskuti na pombe, hasa bia, ambayo huongeza mafuta ya tumbo kwa kasi.
Amesema kawaida kitambi kinaweza kugawanyika katika aina kuu mbili ambazo ni kitambi cha mafuta ya juu ya misuli ya tumbo. Mafuta haya hukaa chini ya ngozi na ni rahisi kuyapunguza kwa mazoezi na mlo bora.
Anataja aina ya pili ni kitambi cha mafuta ya ndani karibu na viungo. Mafuta haya huzunguka viungo vya ndani kama ini, figo na kongosho.
‘’Ni hatari zaidi kwa afya kwani yanaweza kusababisha magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu, na magonjwa ya moyo,” amesema.
Amesema kuwa ili kuepuka kitambi, mtu anapaswa kula vyakula vyenye virutubishi bora na vilivyopunguzwa mafuta na sukari, kama vile mboga za majani na matunda yenye sukari chache na yenye nyuzi nyuzi nyingi kama spinachi, brokoli, tufaa, nyanya na tango.
“Nafaka zisizokobolewa kama mchele wa brown, uwele, na dona. Protini zenye mafuta kidogo kama samaki, kuku wa kienyeji, na maharagwe. Vyakula vyenye mafuta mazuri kama karanga, mbegu za maboga, na parachichi lakini pia na maji ya kutosha badala ya vinywaji vyenye sukari hii itasaidia sana,” amesema na kuongezea:
“Kitambi si suala la muonekano tu, bali lina athari kubwa kwa afya. Mafuta ya tumboni yanaweza kuathiri utendaji wa mwili na kuongeza hatari ya magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.
Kwa wanaodai kupata kitambi cha uzazi, Daktari bingwa wa uzazi na magonjwa ya wanawake, Benny Kimaro kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, amesema hicho pia kinatokana na kutopangilia mlo
“Kikubwa ni kula kiwango kidogo cha wanga… wanawake hasa wa Kiafrika wakiwa wajawazito huwa hawali vizuri na hawapangilii. Pamoja na kuwa kuna mabadiliko ambayo hutokea kwa mzazi bado mlo ni muhimu. Hata ukifunga tumbo baada ya uzazi ukawa unakula vibaya chakula, utapata kitambi,”amesema.