Dar es Salaam. Kesi ya utekaji nyara inayowakabili washtakiwa sita imeshindwa kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni iliyoko Kinondoni kwa sababu mawakili wa upande wa utetezi kushindwa kufika mahakamani.
Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga amesema hayo leo Jumatatu Machi 17, 2025 kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji, hata hivyo wakili wa upande wa utetezi hawajafika mahakamani hapo.
“Leo tuna mashahidi wawili na wapo tayari kuendelea na ushahidi lakini mawakili wa upande wa utetezi hawajafika hivyo tunaiomba Mahakama hii iahirishe shauri hili hadi tarehe nyingine,” amesema Katuga.
Washtakiwa hao wanawakilishwa na Wakili Joseph Salira na Jeremiah Mtobesya hawakuwepo mahakamani hapo kutokana na kuwa nje ya mahakama kwa dharura.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Ramadhan Rugemalira amewaonya mashahidi waliofika mahakamani hapo kufika tarehe ijayo ili shauri liende mbele.
“Washtakiwa mhakikishe tarehe ijayo itakayopangwa mawakili wenu wafike mahakamani ili shauri liende mbele, nafahamu washtakiwa mna haki ya kuwakilishwa ila tusiwanyime haki wasio wakilishwa,” amesema Rugemalira.
Shauri limeahirishwa hadi Aprili 23, 2025 na washtakiwa wataendelea kuwa nje kwa dhamana.
Washtakiwa ni Fredrick Juma Said mjasiriamali, Isack Mwaifani, Benki Mwakalebela ambaye ni wakala Stendi ya Magufuli, Bato Bahati Tweve, Nelson Elimusa ambaye dereva wa teksi na Anita Temba.
Wote kwa pamoja wanaokabiliwa na shtaka moja la kujaribu kuteka mtu na kumuweka kizuizini isivyo halali kinyume na vifungu vya 380(1) na 381(1) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Wanadaiwa katika eneo la Kiluvya Madukani Lingwenye, jijini Dar es Salaam walijaribu kumteka mfanyabiashara Deogratius Tarimo kwa nia ya kumuweka kizuizini isivyo halali.