Shinyanga. Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Pauline Gekuru amekosoa ripoti ya ujenzi wa bwawa la umwagiliaji la Nyida baada ya kutoainishwa gharama za kifedha za ujenzi mbalimbali zinazokamilisha bwawa hilo.
Hayo yamebainishwa Machi 17, 2025 katika ziara ya ukaguzi wa bwawa hilo lililopo katika kijiji cha Nyida Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
“Katika taarifa yenu mmeonesha aina ya ujenzi uliofanyia na kutaja asilimia, lakini sioni kiwango cha fedha katika kila ujenzi husika ambayo hii itatusaidia kufanya majumuisho ya kifedha kutathimini kile kilichofanyika na gharama iliyotumika,” amesema Gekuru.
Akijibu swali hilo, Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa amesema kuwa gharama za ujenzi kwa ujumla ni bilioni 13.6 na ujenzi mdogomdogo unaokamilisha mradi gharama zake zipo ila hazikuainishwa katika ripoti hiyo.
“Gharama zinazotumika katika ujenzi mdogo mdogo unaokamilisha bwawa hili, zipo lakini ni kwamba hazikuainishwa katika nyaraka, hii tumelipokea na tutalifanyia kazi,” amesema Mndolwa.
Bwawa la Nyida litahudumia heka 800 za mashamba ili kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga kutoka gunia 10 kwa heka kwa sasa hadi gunia 40 kwa heka tena misimu miwili litakapomalizika na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kama ukame.
Mhandisi wa umwagiliaji Mkoa wa Shinyanga, Ebenezer Kombe amesema kuwa Kijiji cha Nyida kina wakazi 9,263 watakaonufaika na bwawa hilo ambalo litahudumia heka 800 za mashamba ili kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga kutoka gunia 10 kwa heka kwa sasa hadi gunia 40 kwa heka tena misimu miwili litakapomalizika na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kama ukame.
“Kijiji hiki kina wananchi 9,263 watakaonufaika pia bwawa hili litahudumia wakulima 1,500 ambao wanamashamba ya mpunga heka 800, kupitia bwawa hili litasaidia ongezeko la uzalishaji wa zao la mpunga na kutoka gunia 10 kwa heka hadi gunia 40 kwa heka tena kwa misimu miwili pia itasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kama ukame,” amesema Kombe.
Pia, Kombe ameongeza kwa kusema kuwa bwawa hadi kukamilika kwake litatumia bilioni 13.6 na lina mita za ujazo 7,800,000 ambazo zitamwagilia heka 800 za mashamba ya wakulima kwa Shinyanga na Tabora.
“Kwa asilimia 25 za ukamilishaji zilizobaki wa ujenzi huu ni sawa na bilioni 5.6 ambapo lina kita za ujazo 7,800,000 zitakazo mwagilia heka 800 za mashamba ya mpunga ya wakulima wa Shinyanga na Tabora hasa kwa Nzega” amesema Kombe.
Mndolwa ameongeza kuwa mbali na kilimo cha umwagiliaji ambalo ndio lengo kuu wananchi wa Nyida pia wanaweza kutumia bwawa hili katika ufugaji wa samaki na kujiongezea kipato na pato la kata na Halmashauri.
“Katika bwawa hili tutaweka uzio kwa ajili ya ulinzi pia kwa wananchi wa Nyida wanaweza kutumia fursa hii kujiongezea kipato kwa kupitia ufugaji wa samaki ambao watawauza na kujiongezea kipato,” amesema Mndolwa.
Aidha, mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Deodatus Mwanyika amesema kuwa anatoa shukrani zake kwa wananchi kutambua juhudi za Serikali kwa kuwajengea bwawa hilo.
“Napenda kutoa shukrani zangu kwa wananchi wa kata hii kwa kutambua juhudi za Serikali katika kuwajali na kuwaletea ujenzi wa bwawa hili la umwagiliaji ambalo litasaidia kuongeza kuzalishaji wa zao la mpunga na kukabiliana na mabadiliko ya tabia za nchi,” amesema Mwanyika.