Geita. Viongozi mbalimbali wa Serikali, siasa, na kiroho wamezungumzia maisha ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati John Joseph Magufuli, akiwemo Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi, aliyesema Magufuli amefanya mengi, ukiwa mtu hayaoni ni muongo.
Magufuli (61) alifikwa na mauti jioni ya Jumatano, Machi 17, 2021, katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo. Mwili wake ulizikwa makaburi ya familia nyumbani kwao, Chato, Mkoa wa Geita.
Leo Jumatatu, Machi 17, 2025, ni miaka minne imetimia tangu kifo chake, na kumefanyiwa misa ya kumwombea iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Yohana Muzey, Chato.
Mjane wa Magufuli, mama Janeth, ameiongoza familia kushiriki misa hiyo iliyoongozwa na Askofu Niwemugizi.
Akitoa mahubiri katika misa hiyo, Askofu Niwemugizi amemuelezea Magufuli kama kiongozi aliyewajibika na kuwahurumia wanyonge.
Amesema Magufuli aliishi maisha ya kuwahudumia watu, akihamasisha uwajibikaji, uadilifu na mapambano dhidi ya uovu kama rushwa na unyanyasaji.

“Magufuli amefanya mengi, ukiwa huyaoni wewe ni muongo; kwa muda mfupi nchi ilienda, tunaheshimu maisha yake kwa matunda ya kazi zake alizofanya.”
“Taifa limeguswa na maisha yake; alitutaka tutiane moyo, tuwe na huruma na tupendane kama ndugu. Tunaendelea kuomboleza na kutafuta uponyaji wa nafsi,” amesema Askofu Niwemugizi.
Kwa nini wanamkumbuka, kiongozi huyo wa kiroho amesema Kanisa Katoliki wana kitu kinaitwa matendo ya kiroho ya huruma, na miongoni mwa mambo yanayofanywa ni kuwaombea wafu. Leo wanamkumbuka na kumuombea hayati John Magufuli kwa sababu mbalimbali alizofanya wakati wa uhai wake.
Amesema Magufuli aliamini kwenye ufufuko, lakini pia ni kwa ajili ya kumuombea msamaha wa dhambi kwa kuwa alikuwa kiongozi wa nchi na katika nafasi yake anaweza kufanya mengi ambayo yalikuwa ya dhambi.
Sababu nyingine ya kumuombea ni kukumbuka maisha yake akiwa duniani na huduma aliyoitoa kwa Taifa toka akiwa mbunge, waziri na hadi nafasi ya kuwa Rais wa nchi.
Askofu Niwemugizi amesema Magufuli alifanya mengi, watu wanapaswa kuheshimu yale aliyoyafanya, kumkumbuka ni kuendelea kuomboleza na kutafuta uponyaji kwa kumpoteza mpendwa wao na kudumisha uhusiano na waliotangulia.
Amesema Magufuli alikuwa kiongozi aliyefundisha kuwajibika, kukataa mabaya, rushwa, unyanyasaji, uonevu, na kutaka watu watiane moyo, kuwa na huruma na upendo kwa wengine. Haya ni mambo ambayo hayatasahaulika katika maisha yake aliyoishi duniani.
“Watu wanajadili alitoa mchango gani? Tutaendelea kujadili, tutake tusitake, angalia makosa na mazuri, lakini tunataka kuendelea kujifunza kwenye mazuri yote aliyoyafanya.
“Alitaka maskini waangaliwe na aliwakimbiza watumishi wa umma kuwahudumia. Hizi ndio sababu kubwa za kumuombea,” amesema Askofu Niwemugizi.
Katika kumwelezea Magufuli, Askofu Niwemugizi amesema ni wajibu wa waumini na wananchi wote kumwombea marehemu, huku akisisitiza msamaha na kuendeleza mazuri aliyoyaacha.
“Kwa mabaya yoyote aliyofanya, tumsamehe, lakini yale mazuri tuyakumbatie na tujifunze kutoka kwake, tumuombee apumzike kwa amani. Asiye msamehe Magufuli huyo sio Mkristo. Wapo waliomchukia kwa yeye kulinda rasilimali za nchi, aliipenda nchi sana,” amesema.
Aidha, amewataka waumini kuendelea kuwaombea viongozi waliopo madarakani ili Mungu awajalie hekima, busara, na waongoze kwa upendo wakizingatia haki, na hatimaye ile nchi tunayotamani kuiona tuione.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, ambaye amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, amesisitiza Watanzania kuendelea kumuombea Magufuli apumzike kwa amani na kusema kwa hali ya kibinadamu sio rahisi kusahau, hasa jamii iliyoishi naye, na ndio maana kama familia na jamii wamekuwa na desturi ya kuwakumbuka waliotangulia kwa ibada na mambo mengine mengi waliyoyafanya wakati wa uhai wake.

Amesema Serikali imekuwa na utamaduni wa kuwakumbuka viongozi wa kitaifa, ambao kumbukizi zao huadhimishwa kwa utaratibu unaopangwa na familia.
Viongozi wakuu wa kitaifa, kumbukizi zao zinakuwa zikiadhimishwa kwa utaratibu unaopangwa na familia husika, na Serikali imekuwa ikishiriki na kuwataka Watanzania kuendelea kumuombea Magufuli ili apumzike kwa amani.
Lukuvi amesisitiza kauli ya Askofu Niwemugizi ya Watanzania kumsamehe Magufuli kwa lolote baya alilolifanya wakati wa uongozi wake na kuyaenzi yale mema aliyoyafanya.
“Nchi yetu imepata bahati ya kuongozwa na marais wanaojali utu na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele, kuanzia Nyerere, Mwinyi, Mkapa, na Magufuli. Tunawahesabia haki na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mazuri mengi waliyoyafanya kwa nchi yetu wakati wa uhai wao,” amesema.
Waziri Lukuvi amenukuu kauli ya Mzee Mwinyi aliyoitoa enzi za uhai wake aliposema “Maisha ya mwanadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni ndugu yangu; kuwa hadithi nzuri kwa watakaosimuliwa.”
Amesema kupitia kauli hiyo wanapata ujasiri wa kusema mazuri waliyoyafanya na kwenye kumbukizi ya hayati Magufuli hawana budi kuyasimulia mazuri yaliyofanya na Magufuli.

Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo mawaziri, William Lukuvi (Sera, Bunge na Uratibu) na Innocent Bashungwa (Mambo ya Ndani) wakishiriki Ibada ya kumwombea aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli.
Dk Magufuli alifariki dunia Jumatano ya Machi 17, 2025 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyoma jijini Dar es Salaam. Leo Jumatatu, Machi 17, 2025 imetimia miaka minne tangu kifo chake.
Waombolezaji hao wamejitokeza kwa wingi katika Parokia ya Mtakatifu Yohana Muzeyi Chato, Mkoa wa Geita inakofanyika Ibada hiyo kuungana na wanafamilia akiwemo mjane wa Magufuli, Mama Janeth.
Ibada hiyo inaongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge- Ngara, Severine Niwemugizi.
Amesema Magufuli alikuwa kiongozi toka mwaka 1995 na alihudumu kwenye nafasi mbalimbali za unaibu waziri, waziri kamili, na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa muda wote aliotumika alikuwa kiongozi mzalendo.
Amesema Magufuli alikuwa kiongozi anayejali watu, rasilimali za nchi, baba wa familia na muumini aliyekuwa na hofu ya Mungu, na kusema katika kumuenzi ni vema jamii ikaendelea kushirikiana na familia kumuombea na kutangaza aliyoyafanya.
Amesema wakati wa kifo chake, Taifa lilihuzunika, lakini Mungu alimuinua Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan, na kumpa mamlaka ya kuongoza kwa amani na utulivu.
“…Samia ameendeleza yale yote walioyaanza na mtangulizi wake, na tunashughudia miradi mingi ikikamilika, na pia ipo miradi mingi ameianzisha na inaendelea. Hii ndio maana ya ‘slogan’ Kazi iendelee,” amesema Lukuvi.
Amesema imezoeleka kiongozi anapoingia madarakani huanza miradi mipya na kuanza na watu wapya, lakini Rais Samia ameendeleza aliyoyaacha mtangulizi wake, ikiwemo ukamilishaji wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa reli ya kati na ya kisasa. Kazi zote zinaendelea kwa vitendo kama alivyosema.
“Ni azma ya Rais Samia kuhakikisha anawaenzi viongozi wote wakuu, na sisi tuwaenzi kwa vitendo uzalendo, bidii, na ufanisi ili kuandika hadithi nzuri ya maisha yetu,” amesema Lukuvi.
Akitoa salamu za familia, Jesca ambaye ni mtoto wa Magufuli, amesema ikiwa ni miaka minne toka waondokewe na baba yao wakiwa na majonzi makubwa, nyuso zao zina furaha kwa sababu ya kumbukumbu njema na urithi wa maendeleo aliouacha.

Amesema miaka minne iliyopita Rais Samia alipotembelea Chato aliahidi hatawaacha, na sasa wanashuhudia ni mtu wa kutimiza ahadi zake kwa kuendelea kuwa nao bega kwa bega.
“Kila tukio tunalolisikia linatufanya tutabasamu na kuona fahari ya kuwa sehemu ya urithi wake. Hayati Magufuli alikuwa mtu wa watu, kiongozi wa wanyonge, mchapa kazi na mpenda haki,” amesema na kuongeza;
“Maisha yetu ya dunia ni ya thamani kubwa, tunaishi mara moja na tunaondoka pia. Cha kusisitiza kuhusu maisha ni kwamba yana kikomo, na hakuna anayejua lini mwisho,” amesema Jesca.
Amesema kupitia maisha ya baba yake, yamemfungua macho na kumfanya atambue kwamba mwisho wa ghafla wa maisha unatupasa kuishi kwa kusudi, na kusudi hilo lazima liwe kubwa.
Amesema hayati Magufuli katika maisha yake ya uongozi alijifunza kutoka kwa viongozi waliomtangulia na kupata mafunzo ya uadilifu, uzalendo na dhamira ya dhati ya kulitumikia Taifa.
“Baba yetu alisema siku moja angeungana na malaika huko mbinguni kwa ajili ya kuongoza, na navaa tu jinsi anavyoweza kuwa na mazungumzo akiwa mbinguni na mzee wetu Nyerere, Mkapa na Mwinyi wakikumbushana nyakati walizoziongoza taifa kwa uzalendo wa dhati, na nafikiria wanamtakia Rais Samia Suluhu Hassan kila la kheri kwenye uongozi wake na kuwasisitiza Watanzania kuwa wamoja kama Taifa,” amesema.
Amesema licha ya Watanzania kumtambua Magufuli kama Rais, kwake alikua baba, na amejifunza kujitolea kwa ajili ya wengine, kuwa mwaminifu kwa Taifa lake, mzalendo na mchapa kazi, kulinda rasilimali za nchi, kutanguliza maslahi ya nchi na kumtanguliza Mungu.
Amesema baba yake alikuwa shujaa wa kisiasa, kiongozi mwenye dira na mtetezi wa wanyonge, na kuwataka Watanzania kuchagua moja ya yale maadili aliyoyaishi na kutaka wamuezi kwa kushika misingi aliyoyaanzisha na kuhakikisha aliyoyaanzisha hayaiishi njiani.
‘Chato kutoka kijiji hadi wilaya’
Akitoa salamu zake, mbunge wa Chato (CCM), Dk Merdad Kalemani, amesema hayati Magufuli atakumbukwa kwa mengi hasa kuitoa Chato kuwa kijiji hadi kuwa wilaya.
Amesema Magufuli alikuwa mcha Mungu, ameanzisha na kujenga makanisa mengi, na wana Chato tutamkumbuka kwa mengi aliyoyafanya.

Aidha, akiwa Rais amepeleka miradi mingi Chato ambayo sasa inaendelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan, na akitolea mfano Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato na Uwanja wa ndege Chato, vyote vimefanyika kwa uthubutu wake.
“Mambo yote aliyoyaanzisha akiwa Rais yameendelezwa na kukamilishwa na Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan. Tunasema baba alianzisha, mama ameyaendeleza na kuyatekeleza,” amesema.
Amesema Chato ina vijiji 115 na imejengwa shule 70, na hii ni kazi ya hayati Magufuli.
Katika misa hiyo, UVCCM imewakilishwa na Makamu Mwenyekiti wake, Rehema Sombi, ambaye kwenye salamu zao amesema kama vijana wanaendelea kuyaishi maisha ya Magufuli wakati wa uhai wake kwa kuwa alikuwa Rais wa Watanzania wote.
Amesema enzi za uhai wake, Magufuli alikuwa mtu mwema na alikimbilia wanyonge wakati wote, na kuwa kiongozi aliyeiishi katiba ya CCM kupitia ushirikiano aliouonyesha kwa makamu wake (Samia), ameweza kuyaendeleza yote aliyoyaacha.
“Tunashukuru kwa ushirikiano aliounyoesha kwa makamu wake, na leo tunaona kazi na utu kwa Rais wa awamu ya sita. Sasa tuna kilelezo kwenye Taifa, ametupa kiongozi mwenye upendo. Sisi vijana tutaendelea kuenzi na kuthamini kazi kubwa yote aliyoifanya,” amesema Sombi.
Ndoto ya ujenzi wa kanisa
Godfrey Charles, Mwenyekiti wa Parokia ya Mtakatifu Yohana Muzeyi Chato, amesema ilikuwa ndoto ya Magufuli kujenga Parokia hiyo. Amesema kabla ya kifo chake alimpigia simu na kumwambia ajiandae kwa ajili ya ujenzi, lakini wiki tatu baadaye walipata taarifa ya kifo chake.
Amesema katika kumbukizi ya mwaka jana iliyoongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, alianzisha harambee ya ujenzi wa kanisa hilo na kufanikisha kukusanya zaidi ya Sh200 milioni zilizowezesha jengo kujengwa hadi hatua ya kupauliwa.
Charles amesema ili kukamilisha kanisa hilo, zinahitajika zaidi ya Sh295 milioni. Leo imefanyika harambee na Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa, aliyeshiriki misa hiyo kama mwanafamilia, amechangia mifuko 200 ya saruji. Lukuvi amechangia Sh1 milioni. Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara, John Mongela, amesema CCM itachangia Sh50 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo.
‘Hakuna kama Magufuli’
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita enzi za uongozi wa Magufuli, Robart Gabriel, amesema kiongozi huyo bado yuko ndani ya mioyo ya Watanzania, sauti ya wanyonge maskini, na alifungua njia mpya ya uongozi wa utumishi wenye matokeo.
Amesema Magufuli alimtanguliza Mungu na alionyesha uzalendo kwa Taifa usio na shaka, na kutamani kuona Tanzania inakuwa na utajiri.
“Ni miongoni mwa viongozi wanamapinduzi. Alibadilisha mwelekeo wa siasa na fikra za watu na kuleta uwajibikaji mkubwa. Haya tunayaenzi na kuyakumbuka. Tunamuombea Mungu aendelee kumpumzisha,” amesema.
Amesema maneno yake na usia wake bado unaishi, na Magufuli amekuwa kiongozi wa mfano duniani, wote wanaofuata sera zake wataendelea kumuenzi.
“Alibadilisha maisha ya wengi. Alitufundisha namna ya kuishi kwa kutenda mema, aliwaonyesha wanyonge kesho mpya, alitufundisha kuwa watu wa haki, kumtanguliza Mungu na kuleta mapinduzi ya utendaji kwenye kazi za kila siku,” amesema.
Katika misa hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan. Pia, Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa, ameshiriki misa hiyo.

Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jumuiya ya Vijana wa chama hicho (UVCCM), na mbunge wa Chato, Dk Merdad Kalemani.
Novemba 5, 2015, Magufuli aliapishwa kwa mara ya kwanza kuwa Rais, akimrithi Jakaya Kikwete aliyemaliza muda wake wa miaka 10. Uchaguzi Mkuu wa 2020 alishinda tena kuendelea na muhula wake wa pili na wa mwisho.
Hata hivyo, alitumikia miezi minne pekee. Machi 17, 2021, tangu aapishwe kumalizika kwa muhula wake wa pili, alifariki dunia kwa tatizo la moyo. Samia, aliyekuwa Makamu wa Rais, akaapishwa kuwa Rais kwa mujibu wa Katiba na akawa Rais wa kwanza mwanamke kati ya watano waliomtangulia.
Marais waliopita kwa kuanza na awamu ya kwanza ni Julius Nyerere (1964-1985), Ali Hassan Mwinyi (1985-1995), Benjamin Mkapa (1995-2005), Jakaya Kikwete (2005-2015), na John Magufuli (2015-2021).
Dk Magufuli aliyekuwa na falsafa ya “Hapa Kazi Tu,” baada ya kuapishwa kwa Samia kuwa Rais, alitambulisha falsafa yake ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: “Kazi Iendelee.” Akimaanisha kuendelea na miradi mbalimbali aliyokuwa ameianzisha mtangulizi wake na kuanzisha mipya.