Miaka minne ya Magufuli kaburini, Chato kumkumbuka leo

Dar es Salaam. Jumatano ya Machi 17, 2021, Tanzania iligubikwa na wingu zito la kumpoteza Rais aliyekuwa madarakani, Dk John Pombe Magufuli maarufu JPM.

Ni kwa mara ya kwanza Taifa hilo la Afrika Mashariki kushuhudia Rais aliyekuwa madarakani akifariki dunia. Kifo chake kilitangazwa na Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa Makamu wa Rais.

Dk Magufuli aliyezaliwa Chato mkoani Geita, Oktoba 29, 1959 alihitimisha utawala wake wa miaka mitano na miezi minne aliouanza Novemba 5, 2015 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyoma jijini Dar es Salaam kwa maradhi ya moyo.

Leo Jumatano ni miaka minne imetimia tangu alipovuta pumzi ya mwisho dunia. Mwili wake, ulizikwa katika makaburi ya familia, nyumbani  kwao Chato, Machi 26, 2021.

Kutokana na kifo chake,  Samia Suluhu Hassan aliyekuwa Makamu wake wa Rais aliapishwa Machi 19, 2021, Ikulu ya Dar es Salaam na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kuwa Rais wa Tanzania, hivyo kuwa Rais wa kwanza mwanamke kati ya watano waliomtangulia.

Marais waliopita kwa kuanza na awamu ya kwanza ni Julius Nyerere (1964-1985), Ali Hassan Mwinyi (1985-1995), Benjamin Mkapa (1995-2005), Jakaya Kikwete (2005-2015) na John Magufuli (2015-2021).

Dk Magufuli aliyekuwa na falsafa ya Hapa Kazi Tu, baada ya kuapishwa kwa Samia kuwa Rais akaitambulisha  falsafa yake ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…Kazi Iendelee.

Akimaanisha kuendelea miradi mbalimbali aliyokuwa ameianzisha mtangulizi wake na kuanzisha mipya.

Miongoni iliyoachwa ni Bwawa la Umeme la Nyerere, Daraja la Tanzanite, Daraja la Kigongo- Busisi, ununuzi wa ndege ili kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na barabara mbalimbali nchini.

Dk Magufuli aliacha watoto na mjane, Janeth Magufuli.

Harakati za kisiasa za Dk Magufuli zilianza mwaka 1995 alipogombea kiti cha ubunge katika jimbo la Chato na baadaye kuteuliwa kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Ujenzi. Mwaka 2000, Magufuli aligombea na kushinda tena ubunge na kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Ujenzi.

Aidha, katika chaguzi za mwaka 2005 na 2010, aliendelea kuwania kiti hicho cha ubunge katika jimbo la Chato na kushinda na kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010. Mwaka 2010 alipochaguliwa tena kuwa mbunge wa Chato aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi.

Mwaka 2015, alikuwa miongoni mwa makada zaidi ya 40 wa CCM waliojitosa kuchukua fomu kuwania kumrithi Rais Kikwete aliyekuwa akimaliza muda wake madarakani.

Ni makada 38 pekee ndio walirejesha fomu, wakiwemo mawaziri wakuu wastaafu,  maofisa ngazi za juu za jeshi, mawaziri na makada wa kawaida. Baada ya michakato yote CCM ikampitisha  Magufuli kuwania urais na baadaye akashinda urais wa Tanzania.

Safari yake ya kielimu inaonyesha, Magufuli alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai – Desemba 1983), kisha akaenda kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi Machi 1984) na akamalizia katika kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni 1984). Mwaka 1985 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na alihitimu mwaka 1988.

Kati ya mwaka 1991 na 1994 alijiunga na masomo ya Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza na baadaye mwaka 2006-2009 alijiunga na masomo ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kutokana na taaluma yake Magufuli ameandika vitabu na machapisho mbalimbali.

Leo Jumatano, ndugu, jamaa na marafiki watamkumbuka kwa Ibada itakayofanyikia Chato ambayo imeandaliwa na familia yake.

Endelee kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea kutoka huko

Related Posts